HASIDI HUUNDA UHASIMU, PASIPO NA UHASAMA

Rai - - MBELE -

Hasidi hana sababu ni msemo uliotamalaki kitakita ndani ya jamii ya Kiswahili. Maana yake nini? Inaaminika ndani ya Waswahili kuwa hasidi hasubiri kuchokozwa au kudhulumiwa ati ndipo amwage upupu wake. Hasidi huunda unda uhasimu hata pasipo na uhasama ndugu na marafiki wakahasimiana. Husuda ya hasidi haionekani kwa macho kwa sababu nje yake ni tabasabu na ulimi wa kuvuta maongezi, lakini ndani yake ni roho ya kwa nini na nyongo chungu kabisa.

Ukimtazama kwa macho yenye kuona basi utatambua mara moja kuwa hasidi anao uhusiano wa karibu wa kinasaba na shetani, au kwa kuchangia damu au hulka. Hasidi haji na uadui wa kukunja uso na macho mekundu. Hasidi hutabasamu nawe, hula nawe, na kulala nawe lakini dhamira yake daima ni kukutumbukiza katika misiba na misukosuko. Husemwa pia kuwa hasidi hasira yake haipo kwa mhusudiwa bali kwa neema aliyojaaliwa nayo. Husuda ni kijicho na maya. Mwenyezi Mungu aliwaamrisha malaika wamsujudie Adam kwa neema ambayo alimruzuku. Malaika wote walitii isipokuwa ibilisi na kwa hili akalaaniwa na moto wa Mungu unamsubiri akhera. Hapa tunaona nini! Mungu anamruzuku Adam neema; ibilisi anaona maya na anakataa amri ya Mungu ya kumsujudia Adam; ibilisi analaaniwa na kuandaliwa moto wa akhera.

Tukio hili la ibilisi tukilitaamali kwa umakini tunaona kuwa kwa yakini isiyo na shaka ibilisi hakuwa amemkosea Adam bali Mwenyezi Mungu. Kwa nini! Mungu ndiye aliyemruzuku Adam hivyo kijicho cha ibilisi kwa Adam mzizi wake ni neema ni mwenye kuhusudiwa. Sikusudii kusema hapa kuwa mahasidi ni mashetani bali mwenye neema hana sababu ya kuvunjika moyo vinapomgubika visa na vituko. Mti wa kupopolewa ni wenye matunda.

Kwenye sherehe za harusi utawasikia akina mama wanaghani, “jicho la hasidi mwanangu lisimuone.” Kumbe jicho limeumbwa na husuda. Alaa! Ulikuwa hufahamu? Ole wetu! Laiti na miguu yetu ingekuwa inaweza kufika kila yanakofika macho yetu, basi mikono yetu ingenyakua vyetu na vya wenzetu; na amani ingeadimika. Bali tusisahau kuwa na sikio lina wivu. Neema zenye mayowe nazo huwavuta mahasidi kuja kuicheza ngoma yao.

Ndivyo hivyo ndugu yangu. Lenye kutokeza hadharnai hilo ni la bayana kwa kuonekana kwa macho au kusikika kwa masikio. Hufichika jambo katika uchanga wake bali likipea na kupevuka, asiyeliona atalisikia. Simshawishi mwenye neema kupoteza muda wake kupambana na mahasidi. Ni heri kwa maoni yangu kutumia busara na hekima kudhibiti mafanikio yake kuliko kuyatumia mafanikio yake kupambana na mahasidi wake.

Nimevutiwa na dhamira yako ya kujikwamua. Hiyo mipango yako tayari ni mafanikio bali hiyo ni neema change inayohitaji kulindwa dhidi ya jicho la hasidi. Mipango yako ifumbate fumbatoni na yakishajiri watu watayaona wenyewe. Kumbuka macho yakeo yatatazama mengi ila jishughulishe na unalotaka kuliona. Masikio yako yatasikia vicheko, vilio, nyimbo na mazungumzo. Vyote hivyo ni kelele unayoitaka. Utafanikiwa.

Kalamu ya muungwana inakubali kuwa hasidi hana sababu kwa mwenye neema. Hasidi anayo sababu kwa neema ya mwenzake na hiyo ni roho ya kwa nini. Fumbata mipango yako fumbatoni na husuda utaidhibiti.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.