Rekodi 3 zinazoisubiri Liverpool EPL 2018-19

Rai - - MBELE -

MANCHESTER City kutandikwa mabao 3-2 na Crystal Palace, tena katika Uwanja wake wa nyumbani wa Etihad, mwishoni mwa wiki iliyopita ilikuwa habari njema kwa mashabiki wa Liverpool. Ikumbukwe kuwa wao walishashinda mabao 2-0 wakiwa ugenini dhidi ya ‘wabishi’ Wolves, wafungaji wao siku hiyo wakiwa ni

Huko Etihad, bao la kiungo raia wa Ujerumani, Ilkay Gundogan, liitanguliza Man City katika dakika ya 27, lakini Palace walisawazisha kupitia kwa nyota wao wa kimataifa wa Ghana, Jeff Schlupp (dk. 33).

Hadi dakika ya 51, tayari Man City, ambao mabingwa watetezi, walishakuwa nyuma kwa mabao 3-1, wafungaji wa Palace wakiwa ni Andros Townsend (dk 35) na Luka Milivojevic (dk. 51), kabla ya De Bruyne kuipachikia Man City bao la kufutia machozi (dk. 85).

Katika kile kinachoweza kuwapa presha mashabiki wa Man City, kufikia Sikukuu ya Krismasi mwaka jana, tayari walikuwa wanaongoza ligi kwa tofauti ya pointi 14, lakini safari hii wapo nafasi ya pili, wakiwa wanadaiwa pointi nne.

Kwa matokeo hayo, Liverpool wamebaki kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England kwa pointi zao 48, hivyo Man City wenye 44 wanahitaji nne ili kuwafikia ‘Majogoo’ hao wa Anfield.

Inafahamika kuwa Liverpool ndiyo timu pekee EPL msimu huu, ambayo hadi sasa haijapoteza hata mara moja katika mechi zake 18, ikiwa imeshinda 15 na kutoa sare tatu.

Hiyo inawafanya vijana hao wa kocha Jurgen Klopp kupewa nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa, huku pia ikitabiriwa kuvunja rekodi kibao za Ligi Kuu hiyo. Ni rekodi zipi hizo? Makala haya yanakuchambulia.

Liverpool inaweza kuwa timu pekee kuruhusu mabao machache. Rekodi hiyo inashikiliwa na Chelsea, ambao wakati wanachukua ubingwa msimu wa 2004-05, nyavu zao zilikuwa zimetikiswa mara 15 pekee.

Uwepo wa beki kisiki, Virgil Van Dijk, umakini wa kipa raia wa Brazil, Alisson, umeifanya safu ya ulinzi ya Liverpool kuwa kwenye kiwango kizuri. Hadi sasa, wamefungwa mabao saba pekee, ikizizidi Man City (13), Tottenham (16), na Chelsea (15), ambazo ndizo zinazoikamilisha ‘top four’.

Kucheza mechi nyingi bila kuruhusu bao. Rekodi hiyo nayo inashikiliwa na Chelsea, ambapo katika msimu wa 2004-05 chini ya kocha Jose Mourinho nyavu zao hazikuwa zimetikiswa katika mechi 24.

Kufikia raundi ya 18 msimu huu, Liverpool ndiyo timu pekee ambayo imecheza mechi nyingi bila kipa wao kuokota mpira nyavuni (11), wakifuatiwa na Chelsea (8). Unapouzungumzia ubora wa eneo la ulinzi la Liverpool kwa sasa, utawataja Alisson, Van Dijk, Joel Matip na Dejan Lovren.

Endapo ataendelea kuwa kwenye kiwango alichonacho, Allison mwenye umri wa miaka 26, aliyetua Liverpool akitokea Roma ya Ligi Kuu ya Italia ‘Serie A’, anaweza kuipiku rekodi ya kipa mkongwe, Petr Cech, ambaye alikuwa langoni mwa Chelsea wakati timu hiyo ikicheza mechi 24 bila kuruhusu bao katika msimu wa 2004-05.

Kuchukua ubingwa kwa pointi nyingi. Kwa sasa, ni Man City ndiyo inayoishikilia rekodi hiyo na waliiweka msimu uliopita, walipolitwaa taji la Ligi Kuu wakiwa na jumla ya pointi 100.

Haitashangaza kuiona rekodi hiyo ikihamia kwa Liverpool baada ya kumalizika kwa msimu huu kwani hadi sasa wana pointi 48, huku ikiwa imebakiza michezo 20. Hivi karibuni, kocha wao, Klopp, alisema haitakuwa rahisi, lakini ukweli ni kwamba hilo ni jambo linalowezekana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.