NDANI YA JIWE IPO AINA FULANI YA UBWEGE!

Rai - - MBELE -

LEO tunalijadili jiwe ambalo wengi wetu bila ya shaka tunadhani na kuamini kwamba linatokana na mwamba. Basi uwe ni mwamba juu ya ardhi, chini ya ardhi au ndani ya maji, jiwe huwa ni jiwe tu. Mawe yana msaada mkubwa kwetu. Tunayatumia mawe katika ujenzi wa majumba, barabara, madaraja na kadhalika. Tunatumia mawe kutengeneza chokaa na mawe mengine ni madini yenye thamani kubwa.

Lakini pamoja na msaada mkubwa tunaoupata wanadamu kutokana na jiwe, na pamoja na thamani kubwa iliyomo ndani ya mawe ambayo ni madini na vito mbalimbali, jiwe lenyewe halinufaiki na thamani yake. Ndani ya jiwe ipo pia aina fulani ya ubwege. Ukiliweka jiwe mahali ujue limefika halisogei ila kwa kusogezwa. Jiwe limepewa sudi ya kumneemesha mwanadamu bila ya ujira wala shukurani.

Tunashuhudia pia kuwa wapo wanadamu ambao kwa sababu ya elimu yao, maarifa yao na nguvu zao, nao ni msaada mkubwa kwa wanadamu wenzao. Lakini kama jiwe wanadamu hawa hawanufaiki na msaada wao kwa wenzao, na wala hawanufaiki na thamani waliyonayo. Wanakuwa mithili ya punda kirongwe anayebebeshwa soji mgongoni na asifahamu kuwa kabebeshwa soji lenye mzigo wa thamani. Punda afe mzigo wa bwana ufike.

Na wewe ndugu yangu umehiari kujitoa fahamu ili uwe jiwe? Hapo ulipo ndiyo maskani yako ya kudumu na anuani yako ya utambulisho wako? Yaani hapo ulipo hujiongezi wala hujisogezi hadi usogezwe? Umejipweteka pwetepwete, jua lako na mvua yako! Hapana ndugu yangu! Wewe si jiwe bali ni mwanadamu uliyekirimiwa akili na fahamu. Zinduka, funua macho na uvute tafakuri. Ndani yako upo ukombozi.

Kuhiari kuwa mithili ya jiwe ni kuhiari kuwa mtwana wa kumtumikia bwana na kuhiari dhuluma dhidi yako. Jiwe hupondwa nyundo ili liwe kokoto za kumjengea bwana. Jiwe hukusanyiwa magogo na kuni likaripuliwa moto ili liwe chokaa ya kumneemesha bwana. Mawe aina ya madini na vito nayo hufikwa na misukosuko ili kuyaongezea thamani kwa maslahi ya bwana. Wewe hustahili dhuluma hizi kwa sababu wewe si jiwe.

Elimu na maarifa yako, akili na fahamu yako, na afya na nguvu zako ni mtaji muhimu kwako wa kukuondoshea dhiki na kukuletea faraja. Ukiamua kuutumia mtaji huu muhimu kwako kumnufaisha anayehitaji huduma yako, basi huyo hana budi kufidia kujitoa kwako kwake. Unapswa kuitambua thamani yako, uilinde kwa wivu mkubwa na uitumie kwa umakini wenye kumakinika.

Usikubali kuwa chombo cha kusafirisha wenye kusafiri ilihali na wewe unahitajika kusafiri. Usikubali kuwa daraja la kuvusha wavukao na wewe ukawa unavuka kwa macho tu. Usikubali kuwa ngazi kuwapandisha wapandao vileleni na wewe unabaki chini macho juu. Wala usikubali kuwa sabuni kuwatakatisha walimbwende na nguo zao na povu lako likawa linatiririka kwenye karo hadi mwisho wako.

Ni ujuha kuamini na kukubali kuwa ati maisha ni vyovyote. Hata kidogo! Lakini ni ukweli mtupu kuwa maisha ni popote. Ikiwa hapo ulipo maisha hayaendi basi nenda wewe bali usikurupuke. Hebu tafakari kwa kina ili utambue tatizo linalokukwaza hapo ulipo, zifikirie njia mbili hadi tatu zinazoweza kukukwamua, chukua moja iliyo bora zaidi, anza nayo hiyo sasa kwa utulivu mkubwa. Acha woga na acha ajizi.

Mara nyingi moto wa maisha huchochewa na mazoea. Aliyeajiriwa kufanya kazi fulani ya kulipwa mshahara kila mwezi hata ikiwa kazi hiyo ana weledi nayo kwa kiasi kikubwa, hathubutu kujiamini kuwa anaweza kujiajiri kwa kufanya kazi hiyo hiyo. Tatizo la mwanadamu huyu ni mazoea ya kuajiriwa. Ni mpishi mahiri aliyezoea kuajiriwa hivyo kujiajiri kama baba au mama lishe kwake si hoja yenye mashiko.

Wapo watu wenye afya na nguvu za kutosha wanaofanya vibarua vya kupiga ngwamba kwenye mashamba ya wenzao miaka nenda miaka rudi hali wenyewe hawanayo hata robo eka. Laiti mtu angezitumia nguvu hizi walau kupanda migomba au mikorosho yake katika ekari zake tatu hivi bila ya shaka angejilaumu kwa nini alichelewa kufanya hivyo. Lakini ndiyo hivyo unapoamua kuwa jiwe utasubiri uchimbuliwe kwa mitaimbo.

Mazoea ya kuajiriwa na kutumikishwa ni tatizo kubwa linalowagubika wasomi wa nadharia na wasomi wenye fani za amali. Mtaalamu wa kilimo hana hata tuta moja la mchicha. Mtaalamu wa mifugo hana hata bata wa kuchinja atapotembelewa na wakwe zake. Kutwa wapo maofisini na bahasha yenye vyeti kwapani wanatafuta ajira. Sisemi kuwa hii ni sudi ya jiwe lakini hali inashawishi maswali.

Lipo jambo ambalo pengine nilitakiwa nilitolee indhari mapema. Sikusudii hapa kutamani kila mmoja wetu amiliki jumba kubwa na gari la kifahari. Ninachokusudia ni kila mmoja wetu amudu kujikimu katika mahitaji muhimu yeye na ahali yake. Familia ipate chakula, iishi kwenye makaazi yenye sitara na watoto waende shule. Haya hayapatikani kwa urahisi hadi kwanza mja akatae kuwa jiwe

Ikiwa unayo hali au jambo ambalo linakunyima furaha na bado hujaamua kuachana nalo basi unachojiundia bila ya shaka ni karaha. Ikiwa kutoka kumekulazimu bali ya njiani huyafahamu usifanye ajizi toka uende ila uwe na hadhari. Ukiamua kubakia papo hapo huko ni kukosa nadhari hivyo isubiri hatari na izara. Usije kulia na mtu kwani ukijipiga kofi mwenyewe usilie.

Usitamani kufika juu kileleni kwa macho. Kupanda juu mtini sharti uanzie shinani. Huko juu kuna matawi yenye kutinga pepo zikivuma na nyakati nyingine huko huwepo nyoka na manyigu. Unaowaona wapo juu walianzia chini kwa kujifunga na dhamira zao. Kumbuka kwamba ukiacha kujishughulisha na lenye manufaa kwako basi lisilo na manufaa kwako litakushughulisha.

Jiwe ni zana ya ujenzi kwa mwanadamu. Wewe ndugu yangu si jiwe bali ndiye mjenzi mwenyewe. Kataa kuwa jiwe na kutumiwa kama zana ya kutengeneza kwa wenzako na kwako kwaporomoka. Dhamira yako ikiiongoza akili yako hapana shaka mikono yako itakamata utakacho na miguu yako itaelekea utakako. Tumia elimu na maarifa yako, na tumia akili na fahamu yako utafanikiwa.

Kalamu ya muungwana inakukumbusha kuwa dira ya malengo yako ni mahitaji yako hivyo kigezo cha mafanikio yako kisiwe mafanikio ya wengine. Kumbuka kila mmoja wetu ana ndoto zake.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.