GEORGE WASHIGTON

RAIS ALIYEITENGENEZA MAREKANI KUWA TAIFA IMARA

Rai - - MBELE - NA MBWANA ALLYAMTU

Nilidhamiria kuandika makala hii katika kuadhimisha kumbukumbu ya Siku ya Washington (ambayo huadhimishwa 14/12/2017 Marekani kila mwaka).

Nimeona ni vema, angalau kwa kifupi, wasomaji waweze kumfahamu Gerorge Washington kwa uchache wake. Kutokana na umuhimu wake katika siasa za Marekani, yeye ndiye mwanzilishi wa wazo la kuunda taifa lenye mfumo wa shirikisho, na yeye ndiye aliyependekeza kuunganishwa kwa makoloni 13 ya awali na kuundwa taifa moja mara baada ya kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe (American Civil War) mwaka 1788. Niyeye aliyependekeza jina linalotumika sasa la Muungano wa Nchi za America—United States of America na ndiye aliyetoa wazo la mfumo wa namna ya kuwapata viongozi wao wa kitaifa—mfumo ujulikanao kama Mfumo wa Chaguzi kwa Kongamano yaani Electro College.

George Washington aliongoza kikosi cha wanamgambo kwenye vita ya ukombozi na baadaye kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la Katiba (Constitution Convention) huko Philadephia. Yeye ndiye muasisi wa utaratibu wa kupokezana vijiti katika utawala nchini Marekani.

Moja ya taratibu alizozipendekeza, ndizo zinazoendelea kutumika mpaka leo na kuifanya Katiba ya Marekani kuwa moja ya katiba bora dunia hadi sasa.

George Washington alizaliwa Februari 22, 1732. Alifariki Desemba 14, 1799 akiwa nyumbani kwake Mount Vernon, Virginia. Alikuwa mwanasiasa, kiongozi wa kijeshi, na rais wa kwanza wa Marekani kati ya 1789 na 1797. Washington pia hutambuliwa kama baba wa taifa la Marekani, pia ni miongoni mwa wasisi wa taifa hilo kati ya wasisi 22 wanaotajwa kwenye Agano la Uhuru (Independence Declaration).

Washington alikuwa mtoto wa pili wa mlowezi Augustine Washington, kule Virginia, koloni la Uingereza (lakini alikuwa ni mtoto wa kwanza wa Augustine Washington kwa mama yake Mary Ball Washington, ambaye alikuwa ni mke wa pili wa Augustine Washington).

Wazazi wake walikuwa na mashamba makubwa ya tumbaku yaliyolimwa na watumwa wa Kiafrika.

George alisoma shule miaka michache, hakuendelea sana kielimu. Baada ya shule alianza kazi ya upimaji ramani (surveyor).

Baada ya kifo cha kaka yake, alirithi shamba kubwa lilokuwa pamoja na watumwa. Akawa mkulima tajiri huko Virginia. Sehemu ya urithi ilikuwa ni pamoja na cheo cha Msimazi wa Wanamgambo, na kikosi cha kijeshi cha hiari ambacho kilisaidiana na wanajeshi wa Waingereza kutetea koloni lao dhidi ya majirani Waindio (Red Indians) na Wafaransa katika vita ya (French Indian War), ambao walikuwa wameenea Kusini ya Kanada-Quebec.

Wakati huo, Uingereza ilitaka kuyapokonya makoloni ya Ufaransa ya Amerika ya Kaskazini ambapo yalikuwa chini ya Ufaransa (sasa Canada). Jambo hili ndilo lilichochea chuki kwa Wafaransa na kuchochea hali ya Ufaransa kuja kuwasaidia askari wa makoloni 13 ya Marekani kama sehemu ya kulipiza kisasi.

Akiwa na umri mdogo wa miaka 22, Washington alijikuta ni mkuu wa wanamgambo katika vita ya Uingereza dhidi ya Wafaransa na Waindio iliyochukua miaka saba. Baadaye akaongoza kikosi chake dhidi ya maadui, akafaulu mara kadhaa.

Kwa kushirikiana na jeshi rasmi la Uingereza katika mapigano ya Monongahela na kuongoza mabaki ya jeshi baada ya kifo cha jemedari wa Kingereza. Mwaka 1755, akawa mkuu wa jeshi la koloni Virginia.

Lakini baada ya ushindi, Waingereza walikataa kumpa cheo katika jeshi la Mfalme, hivyo akajiuzulu na kuamua kurudi kwenye shamba lake na kuanza kujishughulisha na siasa kwenye bunge la Virginia.

Mwaka 1759, Washington akavunja ukapera, akamuoa mjane tajiri Martha Dandridge Custis, akawa kati ya matajiri wakubwa kabisa wa jimbo la Virginia.

Baada ya vita, uhusiano kati ya Uingereza na walowezi Waingereza katika koloni zake 13 za Amerika ya Kaskazini, ukazorota sana. Tangu 1773 Waingereza walitumia sheria ya dharura na nguvu ya kijeshi mjini Boston na yakatokea mauaji makubwa yanayojulikana kama Boston massacre. Mauaji hayo baadaye yalikuwa chachu ya mapinduzi na harakati za kudai uhuru katika majimbo 13 yaliyokuwa yakitawaliwa na Uingereza. Hivyo kufuatia mauaji hayo, wawakilishi wa makoloni yote 13 wakakutana kama bunge la Amerika Bara na Washington alikuwa miongoni mwao.

Baada ya mapigano ya kwanza kati ya wanajeshi Waingereza na wanamgambo wa walowezi, bunge likaamua kuunda jeshi la pamoja la koloni zote (Continental army), na Washington akateuliwa kuwa jemadari mkuu.

Aliongoza jeshi la Marekani katika vita ya uhuru dhidi ya Uingereza hadi mwaka 1783 Waingereza walipokubali kushindwa vita na kukubali kukabidhi uhuru kwa walowezi wa Kiingereza.

Baada ya vita hiyo, Geroge Washington akarudi shambani kwake kuendelea na shughuli zake za kulima, lakini akachaguliwa kuwa mwakilishi wa Virginia katika Bunge Maalumu la Katiba la Marekani mwaka 1787 ambapo alichaguliwaa kuwa mwenyekiti. Bunge hilo ndilo lililoandaa Katiba ya Marekani.

Februari 4, 1789, Washington alichaguliwa kuwa rais wa kwanza wa Marekani. Akarudishwa tena madarakani mwaka 1793 mpaka mwaka 1797. Baada ya kipindi chake cha pili kumalizika, alikataa kusimama tena kuwania urais na akaunda utaratibu kwamba rais na marais wote watakaomfuata, wanaweza kurudishwa mara moja tu na hawatoweza kuendelea zaidi.

Utaratibu huo uliheshimika na kuendelea kutumika kwa warithi wake wote waliomfuata, mpaka utaratibu huo wa ukomo wa urais wa miaka minane kwa mihula ya miaka minne ulipokuja kuingizwa rasmi kwenye katiba yao mwaka 1940 katika kile kilichoitwa marekebisho ya 22 ya katiba (22nd amendment).

Mwaka 1797, Washington akarudi tena shambani kwake kwenda kusimamia kilimo kilichoendeshwa na watumwa 390 aliokuwa akiwamiliki.

Mnamo majira ya baridi, majira ya saa nne asubuhi ya siku ya Jumamosi ya Disemba 14, Washington alifariki dunia kwa ugonjwa wa kansa ya koo (epiglottises) akiwa na umri wa miaka 69.

Ulimwengu ulitangaziwa kifo chake na mwandishi wake binafsi na msemaji wake, Tobias Lear. Kabla ya kuaga dunia, Washington aliamuru katika usia wake kwamba watumwa wake wote warudishiwe uhuru baada ya kifo chake, yeye pamoja na mke wake. Washington hakubahatika kupata mtoto katika maisha yake yote.

Mji mkuu wa Marekani, Washington, D.C. na jimbo la Washington linalopatikana Magharibi mwa Marekani, vimepewa majina kutokana na yeye. Kwa heshima yake, picha yake iko kwenye noti ya Dollar moja. Huku yeye akitambulika kama baba wa taifa na ikiwa pamoja na tarehe ya kifo chake kuwa siku ya kitaifa nchini Marekani.

Simu+255679555526.

GEORGE WASHIGTON

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.