ATCL chungu kwa vigogo

Rai - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

UAMUZI mzito uliochukuliwa na Rais Dk. John Magufuli wa kulifufua Shirika la Ndege nchini (ATCL) unatajwa kuwa na tija kubwa kwa nchi, lakini ni mchungu kwa baadhi ya vigogo serikalini. RAI linachambua.

Uchungu kwa vigogo hao, wakiwamo mawaziri, maofisa na watumishi wengine wa Serikali umeanza kuonekana mwanzoni mwa wiki hii, baada ya Rais Magufuli, kuwatemea cheche vigogo hao.

Akiwa katika mwendelezo wa kupokea ndege za Tanzania zinazolirejeshea uhai shirika hilo, Rais Magufuli aliwataka watumishi wote waliokatiwa tiketi za ATCL na serikali na kisha wakakacha kusafiri na ndege za shirika hilo, warudishe fedha hizo haraka.

Rais akitoa hotuba baada ya kuipokea ndege kubwa ya kisasa ya Airbus A220300 ikiwa ni ya tano tangu aingie madarakani mwaka 2015, alitaka apatiwe orodha ya watendaji wanaokadiriwa kufikia 100 wa Serikali ambao wanakatiwa tiketi kisha hawasafiri na ndege za ATCL, hali inayozifanya ndege hizo kusafiri zikiwa tupu.

Alisema baadhi ya watendaji wamekuwa wakikatiwa tiketi kwa fedha za serikali bila kusafiri na kuisababisha hasara.

“Baadhi ya tiketi zinakatwa na watendaji wa serikali halafu hawasafiri matokeo yake ndege inakwenda tupu. Niletewe orodha yote ya watendaji wa serikali ambao hawakusafiri ili tuwakate hizo fedha kwenye mishahara yao. Nina uhakika kufikia wiki ijayo nitapata majina yao.

“Ndege inakwenda tupu na fedha ya serikali imetumika. Ambao hawakusafiri na walikatiwa tiketi kwa fedha za serikali wajiandae kurudisha fedha ili kusudi mambo yaishe,” alisema Rais Magufuli.

RAI limeelezwa kuwa kauli hiyo ta Rais imekuwa mwiba mkali kwa vigogo hao, ambao majina yao tayari yako kwenye mamlaka husika.

Pamoja na kuelezwa wazi kuwa watakatwa mishahara, lakini lolote linaweza kutokea dhidi yao hasa ikizingatiwa kuwa Rais Magufuli si mtu wa kujaribiwa kama ambavyo amekuwa akisema mwenyewe.

Uchungu huo unaonekana kuwagusa pia baadhi ya watumishi wa shirika hilo, ambao wanaonekana kulihujumu hasa katika eneo la ukatishaji wa tiketi na malalamiko yanayohusu eneo la huduma.

“Tiketi zinazotolewa na mawakala zinauzwa kwa bei ya chini kuliko zinazotolewa na shirika. Wanaotaka kusafiri na ndege wanaambiwa imejaa lakini wanapoingia ndani inakuwa haijajaa.

“Baadhi ya makawala wanatumia kadi za benki kukata tiketi, kugushi kwa kutumia kadi za watu wengine. Naambiwa wako polisi washughulikiwe kwa sababu ndio wanahatarisha juhudi za kujenga uchumi wa Watanzania,” alisema.

Aliwataka wafanyakazi wa shirika hilo walinde dhamana ya Watanzania katika kutunza ndege hizo.

“Shirika hili lilikuwa limepotea, nitasikitika kama bodi na menejimenti ya ATCL watajisahau na kuturudisha tena kule tulikotoka, itakuwa ni aibu kwa Watanzania wote.

“ATCL wameazimwa ndege za Serikali, zimenunuliwa kwa kodi ya wananchi, wasipozalisha tunawanyang’anya, vya kupewapewa bure watu wanasahau.

“Tutaendelea kuwabana watendaji ambao wanafikiri kila kitu ni sikukuu. Hakikisheni hizi ndege zinaendelea kuzalisha, mwelekeo uwe wa kufanya biashara na si kufanyiwa biashara,” alisema.

Rais Magufuli alisema usafiri wa anga ni huduma na ni biashara yenye faida hivyo aliwataka wafanyakazi hao kufanya kazi kwa bidii, kuwa wabunifu na kuboresha huduma.

Wakionesha uchungu unaowakabili vigogo wa serikalini kutokana na kufufuliwa kwa shirika la Ndege nchini baadhi ya wasomi wamewaonya watumishi hao wa umma kwa kuwataka kuacha utendaji wa kubabaisha na badala yake wawe wabunifu ili kuliletea tija kusudiwa shirika hilo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaama, Dk. Benson Bana alisema kitendo cha vigogo hao wa serikali kukatiwa tiketi na kuacha kusafiri kimeiathiri serikali nzima.

Dk. Bana aliongeza kuwa adhabu ya kuwakata mishahara kurudisha gharama za tiketi hizo haitoshi, bali vigogo hao wanapaswa kupewa barua kali za onyo kwa kuwa kitendo walichofanya ni sawa na ufujaji wa mali ya umma.

“Kwa sababu ni hela ya walipa kodi, na wanaturudisha zamani tulikotoka… nadhani hata agizo la rais kuwa warudishe hizo fedha kutoka kwenye mishahara yao haitoshi, ingetakiwa iende na barua ya onyo.

“Sio kurudisha nauli tu…ni ufujaji wa mali ya umma pasipo na sababu za msingi, hata sisi abiria wa kawaida kama unafuta safari yako unatoa taarifa ili urudishiwe fedha au ubadilishe ratiba. Sasa hawa hawajafanya yote mawili, hawa hawatufai, wapewe barua ya karipio. Ningekuwa rais wale wote nilio na uwezo nao ningewalima barua ya karipio,” alisema.

Kuhusu ni namna gani ATCL ifanye ili ijiendesha kwa faida, Dk. Bana alisema serikali isione haya kukodisha watalaam wa masuala ya masoko kutoka nje pale kunapohitajika.

“Pale ambapo wanaona wanapwaya hawana utaalamu wa kutosha, wasisite kutafuta utaalam kutoka nje ya nchi, pale ambapo tunafikiri utaalamu wetu hautoshi tusilazimishe kutumia watu wetu ambao uzoefu wao ni mdogo.

“Tumpate mtaalam tumpe mkataba wa miaka miwili au mitatu, atutengenezee miundombinu ya kuendesha biashara ya ndege. Hili la muhimu na Rais hajalisemea. Ila asiogope kusema pale ambapo tunapwaya kwa mfano upande wa masoko hatujalowea na kupata mtalaam wa kupenya kwenye masoko makubwa,”alisema.

Alisema kiujumla Taifa lina matumaini makubwa na ATCL hasa kwenye sekta ya utalii ambayo inaingiza mapato makubwa nchi.

“Wajitahidi ndege hizi zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa hasa kuinua utalii, wahakikishe Zanzibar, Katavi, Arusha wanafika na hii iendane na ujenzi wa miundombinu ya viwanja katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Dodoma na Kigoma.

“Tatu watangulize uzalendo, ulaji upungue matumizi yasiyo ya lazima yapungue ili watanzania waone faida kama alivyosema Rais Magufuli kwamba watanzania wanataka kuona faida. Hayo ndio matarajio ya watanzania. Ndege nyingine ijayo inunuliwe kwa faida ya shirika hilo,” alisema.

Hoja hiyo pia iliungwa mkono na Mkurugenzi wa Kampuni ya ushauri wa masuala ya Benki na masoko ya fedha (Bankable Tanzania Ltd), Lawrence Mafuru ambaye alisema kitendo kilichofanywa na watumishi hao kimeitia hasara serikali.

Mafuru ambaye alikuwa Msajili wa Hazina katika serikali ya awamu ya nne na hata ya tano alisema “Naona mambo mawili, kwamba kama umekatiwa tiketi na hukusafiri maana yake umeitia hasara serikali.

“Kwa kuwa shirika lililipwa halafu mtu hakusafiri hapo aliyepata hasara ni serikali, kwa hiyo mkuu anaposema anataka kukata mishahara analenga kurudisha hela yake.

“Lakini ubaya wa hicho kitu ni kwamba abiria wengine wakitaka kusafiri wataambiwa ndege imejaa huku ukweli ni kwamba kuna watu hawajasafiri. Lakini ikiwa wamekata tiketi lakini hazilipiwi hapo ATCL itarudi ilipotoka, na hatua zilizotangazwa kuchukuliwa na Rais ni hatua muafaka, alisema.

Aidha, aliushauri uongozi wa ATCL kutambua kuwa sekta ya usafiri wa anga ni ya ushindani mkubwa hivyo ili uweze kustahimili lazima wafuate maelekezo waliyopewa na Rais John Magufuli.

Alisema Rais ametoa maelekezo katika wakati muafaka, kuwa ATCL wako kwenye biashara ya kutoa huduma.

“Kuna maneno mawili, ‘Biashara na Huduma’.

Biashara maana yake kutakiwa kuakikisha unazalishaji mapato ya kutosha huku unafanya matumizi yenye tija, hapo utapata faida.

“Lakini huduma maana yake ni kwamba ili upate mapato ni lazima mteja aliyepanda ndege leo apange kupanda tena kesho kutokana na huduma unayompa leo. Kwa hiyo ikiwa mimi nimepanda ndege leo nikapata huduma mbaya kesho sipandi tena, ila nikipanda nikapata huduma nzuri nitapanga safari ijayo kupanda tena.

“Wakilielewa hilo na kulishikilia kiujumla bado nchi yetu ni kubwa sana kuna maeneo ya kufika, watanzania watatumia ndege za ATCL, hivyo wazingatie yale ya Rais kuwa wakumbuke wapo kwenye huduma na biashara. Hilo wakizingatia watakuwa kwenye nafasi nzuri,” alisema.

Mwenyekiti mstaafu wa Jukwaa la Wakurugenzi wa Sekta Binafsi (CEOrt), Ali Mufuruki aliipongeza ATCL kwa kupata ndege ya tano ambayo ni kielelezo bora cha ufanisi.

“Mimi bahati mbaya nimeshawahi kufanya kazi ATCL kama Mwenyekiti wa bodi, wakati wangu mambo hayakwenda vizuri kwa hiyo nasita kutoa ushauri nini cha kufanya, lakini nawapongeza kwamba wamepata miundombinu ya kazi na Mungu awaongoze mambo yaende vizuri,” alisema.

Aidha, alisema suala la watumishi zaidi ya 100 ambao walikatiwa tiketi na serikali ili wasafiri lakini hawakusafiri haliwezi kuliteteresha shirika hilo.

“Sijui kwanini hawakusafiri, lakini siku zote kwenye biashara ya ndege wapo abiri wanaokata tiketi na hawasafiri, mambo yanabadilika, hivyo sio tatizo la ATCL pekee,” alisema.

Ndege mpya aina ya Airbus 220-300 ‘Dodoma Hapa Kazi Tu’, iliyotua mwanzoni mwa wiki hii nchini ina uwezo wa kubeba abiria 132 na kati yao 12 wa daraja la biashara na 120 kawaida.

Ujio wa ndege hiyo unalifanya shirika hilo kwa na ndege sita, ndege tano zikiwa zimenunuliwa chini ya mpango wa kufufua shirika hilo lililoanzishwa mwaka 1977.

Miongoni mwa ndege hizo ni Bombardier DASH8 Q400 tatu, mbili ambazo zilifika Tanzania Septemba 2016 na moja Aprili 3 mwaka 2018; Boeing 787 Dreamliner ilitua Tanzania Julai 8, 2018 na Airbus 220-300 ametua Disemba 23 mwaka huu.

Shirika hilo lilikuwa na Bombardier DASH8 Q300 moja ambayo ilikuwa ikitoa huduma tangu mwaka 2011.

Disemba 23, Rais John Magufuli alipokea ndege mpya ya tano aina ya Airbus 220-300 ‘Dodoma Hapa Kazi Tu’, yenye uwezo wa kubeba abiria 132 na kati yao 12 wa daraja la biashara na 120 kawaida.

Julai 7 mwaka huu, ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262 ilitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam ikitokea mjini Seattle Marekani.

Kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa na Mkurugenzi wa mawasiliano katika Ikulu ya rais, ndege hiyo ilikuwa ni ya nne kuwasili nchini kati ya saba zilizonunuliwa na serikali.

Aprili 3 mwaka 2018, ndege aina ya Bombardier Dash 8 Q400, ambayo ilikuwa imezuiliwa Canada kwa amri ya mahakama na ambayo Rais Magufuli alimuandikia barua waziri mkuu wa nchi hiyo na kumtuma mwanasheria mkuu wa serikali kuifuatilia mwishoni mwa mwaka jana, iliwasili nchini.

Septemba 28, 2016 Rais John Magufuli alizindua ndege mbili mpya aina ya Bombadier Q400 NextGen na Bombadier Dash 8 Q400 zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL). Ndege hizo zina uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja.

Septemba 20, 2016, Ndege mpya ya kwanza iliyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kutumiwa na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K. Nyerere Jijini Dar es salaam ikitokea nchini Canada ilikotengenezwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.