Uraibu wa kubeti unawamaliza vijana

Rai - - HABARI - NA THADEI OLE MUSHI Ole Mushi 0712702602

Kama hujawahi kushiriki mchezo wa bahati nasibu maarufu kama ‘kubeti’, basi utakuwa umewahi kuusikia. Kubeti kama wenyewe wanavyouita, ni kitendo cha kufanya ubashiri wa matokeo ya mchezo fulani kabla haujachezwa.

Mchezo huo unaweza ukawa mpira wa miguu, mashindano ya magari, riadha mingineyo, japokuwa kwa hapa Tanzania wachezaji wengi wa kamari hii hutabiri matokeo ya mpira wa miguu katika ligi mbalimbali.

Kama tujuavyo, kubeti ni kamari iliyohalalishwa na kamari ni kitendo cha ‘ku-risk’ fedha au kitu cha thamani kwa kutegemea kushinda ili upate zaidi.

Kwa maana hiyo, kamari hii inakwenda na ‘option’ mbili kubwa; kupoteza au kupata. Unachopoteza hapa ni fedha au kitu chako cha thamani ulichokitumia kuchezea kamari hiyo.

#Kwa sasa madhara ya moja kwa moja hayajaonekana juu ya mchezo huu ambao umejumuishwa kwenye michezo ya bahati nasibu nchini.

#Kwa siku za karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa sana la vituo vya uchezeshaji wa mchezo huu... na unachezwa na rika zote kwenye jamii.

Pamoja na kwamba vitabu vya dini vinakataza kwa pande zote, nikilenga zaidi Uislamu na Ukristo, vijana wake wamekuwa ndio wachezaji wakuu wa mchezo huu.

Cha ajabu hata viongozi wetu wa dini wanahalalisha uchezaji wa kamari kwa kuwa wala hawakemei. Nasema wamehalalisha kwa kuwa hawakatazi na wala hawajaweka nguvu yoyote kupambana na swala hili kiimani.

Madhara ya kubeti ni mengi, ingawa kampuni zinazoendesha michezo hii inajiingizia fedha nyingi.

Kwa kuwa mchezo huu umekuwa ukichezwa sana na vijana, ambao wengine wapo shuleni na wengine ndio wazalishaji mali basi wamekuwa wakipoteza muda mwingi huko.

Ili uweze kuucheza mchezo huu vizuri itakulazimu kujifunza na kuelewa mambo mengi ya msingi katika mchezo husika. Mfano itakulazimu kuzielewa ‘odds’ zinazotolewa za matokeo mbalimbali.

Uwe ‘up to date’ na takwimu zote kuhusiana na mechi husika kama vile wachezaji majeruhi, walio katika fomu, waliosimamishwa, hali ya hewa, ubora wa wapinzani, itakakochezwa mechi na mambo mengine mengi ambayo yatakulazimu kushinda mitandaoni au kwenye vijiwe vya soka ili kupata taarifa zote hizo muhimu.

Kama ni mwanafunzi, huyu moja kwa moja ataathirika kitaaluma na kama ni mzalishaji mali ataathirika kiuchumi kutokana na upotevu mkubwa wa muda na uvivu.

Athari nyingine ni kuongezeka kwa magonjwa ya presha kwa wachezaji. Kwa sasa athari hii haijaonekana moja kwa moja ila huko tuendako itajitokeza.

Wachezaji wengi wa mchezo huu wamekuwa wakiishi maisha ya wasiwasi na presha, wakisubiri timu zao walizobeti zishinde ili wapate fedha za chapchap.

Kama mchezaji kamari hii atakuwa anafuatilia mchezo husika na timu aliyotabiri kushinda haielekei kushinda basi huwa na wakati mgumu kiafya.

Pamoja na hayo, mchezo huu kwa vijana unachochea ujambazi na wizi. Kama ilivyokuwa kwa vijana waliokuwa na uraibu wa dawa za kulevya, basi mchezo huu nao umeanza kuelekea kuwa na walevi wake.

Binafsi nimeshawahi kufuatwa na vijana zaidi ya sita wakikopa fedha za kwenda kubeti. Yaani kuliko aache bora akope! ‘what if’ akiikosa fedha hiyo? Basi ataanza udokozi na baadaye atakuwa mwizi kabisa.

Kwa watu wazima wamekuwa wakitumia fedha za familia kwenye mchezo huu. Badala ya kupeleka mahitaji ya msingi nyumbani, anaona ni bora atumie fedha hizo kujaribisha kama anaweza kuambulia chochote kitu.

Tanzania ijiandae kuwa na vijana wengi walioathirika kiafya kutokana na mchezo huu.

Kwa hii kasi ya ueneaji wa mchezo huo kwa hapa nchini, tuanze kufikiria kuanzisha taratibu za ‘rehabilitations’. Kwa wenzetu wazungu, wameshaanza kukumbwa na matatizo makubwa ya kubeti na wameshaanzisha vituo vya kufanya rehabilitations.

Kama hujaanza kucheza mchezo huu, usifikirie kucheza na viongozi wetu wa dini waseme waziwazi kuwa ni kinyume cha taratibu za dini zetu.

Serikali ione namna inavyoweza kuwanasua vijana hawa kwenye uraibu huu na kuwaelekeza kwenye maswala ya uzalishaji mali zaidi. Hawa kina Tarimba Abbas wanatumalizia nguvu kazi, huku wao wakineemeka.

Na kwa sasa kila mtu anawaza kuanzisha mchezo wa bahati nasibu nchini, akijua tumeshapata uraibu wa kutosha, hivyo ni rahisi kuamini tunaweza kupata fedha za haraka.

Wachina nao wamekuja na mashine zao za kutumbukiza mia mbili mia mbili. Nendeni kwenye hivi vituo muone utitiri wa vijana ambao hawana kazi.

Niliiandika mwaka jana, tarehe kama ya leo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.