Valium dawa za maumivu makali zinazozalisha ‘mateja’ wapya

Rai - - HABARI -

LICHA ya juhudi kubwa zilizopo, hasa katika Serikali hii ya Awamu ya Tano, bado vita dhidi ya dawa za kulevya imeendelea kuwa ‘pasua kichwa’.

Si tu Tanzania, ni janga ambalo limekuwa likitikisa ulimwenguni kote, huku mataifa ya Afrika yakionekana kuathirika zaidi.

Sambamba na sababu nyingine zinazohusihwa na uwepo wa biashara hiyo haramu, hali ngumu ya uchumi waliyonayo watu wake, imekuwa ikitajwa kuchangia kwa kiwango kikubwa.

Hapa nchini, Serikali kupitia vyombo vya dola, imekuwa ikihaha kutokomeza biashara hiyo, mapambano ambayo kwa upande mwingine yanaongezewa nguvu na taasisi binafsi.

Lakini, changamoto kubwa iliyopo ni Serikali na taasisi hizo kuchelewa, au kushindwa kabisa kudhibiti mikakati waliyonayo watumiaji na wafanyabiashara wa dawa za kuevya.

Leo nizizungumzie dawa aina ya Valium, ambayo kinyume cha makusudio ya utengenezwaji wake, imekuwa ikitumiwa ndivyo sivyo, hivyo kuwa chanzo cha ‘uteja’ (urahibu wa dawa za kulevya).

Kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu wa afya, Valium ni dawa ya kukabiliana na maumivu makali, yakiwamo yatokanayo na ugonjwa hatari wa kansa.

Aidha, taaluma hiyo inaitambua pia Valium kwa msaada wake wa kutokomeza haraka maumivu yanayoibuka baada ya mgonjwa kufanyiwa upasuaji.

Hata hivyo, ambacho huenda wengi hawakifahamu, dawa hiyo hutumiwa na vijana kama chanzo cha ulevi kama zilivyo dawa za kuevya.

Ikumbukwe kuwa Valium ina uwezo wa kusababisha usingizi kwa haraka, hivyo wanapoitumia huanza kusinzia kana kwamba wamelewa aina zingine za dawa za kulevya au pombe.

Utafiti wangu mdogo wakati wa maandalizi ya safu hii ya ‘Macho Yameona’ ulibaini kuwa sehemu kubwa ya vijana hao ni wanaochipukia katika utumizi wa dawa za kulevya.

Ingawa wapo wanaotumia Valium wanapokosa fedha za kununua dawa za kulevya kama cocaine, wengi ni wale waliokuwa wakitumia bangi tu hapo awali.

Hivyo, baada ya kuuzoea ulevi wa mmea huo ambao ni chakula katika baadhi ya jamii, hawaoni kama kuna kitu kipya wanachokipata na ndiyo maana wameamua kutafuta ‘starehe’ kubwa zaidi.

Juu ya namna ambavyo vijana hao wamekuwa wakiipata Valium, utafiti wangu ulionesha kuwa wapo baadhi ya wahudumu wa maduka ya dawa wanaoshiriki kwa kiasi kikubwa kuwauzia dawa hiyo kinyemela.

Kama tatizo la weledi au tamaa ya fedha, wamekuwa wakifanya hivyo licha ya kujua wazi kuwa inakwenda kutumika ndivyo sivyo, hivyo kuendeleza changamoto ya nguvu kazi ya taifa kupotea kutokana na utumizi wa dawa za kulevya.

Katika hilo la weledi, niseme tu wazi kuwa wahudumu hao wameamua kukinzana na sheria na miiko ya kazi yao hiyo ya uuguzi. Wanastahili kuchukuliwa hatua.

Pia, kama kulivyo na mikakati ya kila uchwao ya kukabiliana na dawa za kulevya kama cocaine na bangi, hili la Valium nalo linahitaji uangalizi wa karibu.Shaka kubwa inatokana na ukweli kwamba huenda wanaotumia Valium sasa wakawa mateja miaka michache ijayo. Kama nilivyoeleza hapo awali, bado wengi wao si wazoefu wa mihadarati, ni hatua yao ya pili baada ya kuona bangi haziwasisimua tena.

Je, kitakapofika kipindi cha kuiona Valium haiwapi ‘mzuka’ wa kutosha, nini kitafuta kama si kujaribu cocaine au aina zingine za dawa za kulevya?

Na kama hiyo itakuwa ndiyo hatima ya vijana hao, nani atakayepaswa kubeba mzigo wa lawama kati ya jamii iliyowazunguka, au Serikali yenye mamlaka ya kulimaliza tatizo hilo mapema?

Kama tatizo la weledi au tamaa ya fedha, wamekuwa wakifanya hivyo licha ya kujua wazi kuwa inakwenda kutumika ndivyo sivyo, hivyo kuendeleza changamoto ya nguvu kazi ya taifa kupotea kutokana na utumizi wa dawa za kulevya.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.