Nnkomanile mpiganaji wa kike aliyeogopwa katika vita ya Maji Maji

Rai - - MAONI / KATUNI - NA FRANCIS DAUDI

Kwa kipindi kirefu, wanawake wa Afrika wamekuwa bega kwa bega na wanaume katika harakati mbalimbali za kulikomboa bara letu, lakini katika makala, vitabu, majarida ya kisiasa na hata ya kihistoria, yamekuwa hayawapi nafasi mashujaa wanawake.

Kwa kipindi kirefu, wanawake wa Afrika wamekuwa bega kwa bega na wanaume katika harakati mbalimbali za kulikomboa bara letu, lakini katika makala, vitabu, majarida ya kisiasa na hata ya kihistoria, yamekuwa hayawapi nafasi mashujaa wanawake.

Wakati wa vita vya kizalendo vya Maji Maji 1905 -1907 vilivyoongozwa na Watanganyika wa makabila mbalimbali dhidi ya wakoloni wa Kijerumani (Wadachi), wanawake walijitoa ili kupinga udhalimu wa wakoloni.

Vita vya Maji Maji viliunganisha makabila ya Wamakonde, Wangoni, Wangindo, Wamwera, Wabena, Wamatumbi, Wapogoro, Wambunga, Wazaramo na makabila mengine madogo madogo kati ya mwaka 1905 mpaka 1907. Ingawa mwisho wa harakati hizi Wafrika walishindwa vibaya na majeshi ya Wadachi, lakini kwa Watanganyika, ilikuwa ni mwanzo wa mapambano ya kutaka kujitawala.

Februari 27, 1906, ni siku ambayo baadhi ya viongozi wa vita hivi walinyongwa mpaka kufa mjini Songea mbele ya ndugu zao. Kati ya walionyongwa ni mwanamke mmoja tu mzalendo na shujaa aliyeogopwa na Wadachi kwa kuwezesha kufanikiwa kwa mapambano katika jamii ya Wangoni.

Nkomanile Mkomanile au Nkomandire, ni mwanamke pekee aliyenyongwa siku nyeusi katika historia ya Wangoni, maandishi na simulizi mbalimbali hutumia majina hayo yakimaanisha mtu mmoja.

Hakuna maandishi au simulizi za kutosha juu ya kihistoria ya maisha ya utotoni ya Mkomanile. Katika utangulizi wa kitabu cha ‘Utenzi wa Vita vya Majimaji’ kilichoandikwa na Abdul Karim bin Jamaliddini, ulioandikwa na Bi Margareth Bates, anaeleza kuwa Omari Kinjala alitumwa Ungoni( maeneo ya sasa ya Songea) toka Liwale akifuatana na mkewe ambaye Wadachi walimwita ‘Jumbess Mkomanire’ yaani Jumbe-waKike, Mkomanile yeye alikuwa Mngoni, jamaa wa Chabruma( Chifu wa Wangoni) huko Mashope.

Simulizi na maandishi yaliyopo, yanapinga hilo, kwani Nkomanile alikuwa Nduna wa Mashope na Kinjala hakuwahi kuwa mwenyeji wa Ungoni, bali alitumwa tu kutoka Liwale kupeleka ujumbe wa vita vya Majimaji.

Kitabu cha ‘The Majimaji War in Ungoni’ yaani ‘Vita vya Majimaji katika Ungoni’ kilichoandikwa Mapunda O.B na Mpangala G.P, wanaeleza kuwa Omari Kinjala alitoka Liwale na alipoingia maeneo ya Wangoni hasa Mshope yaliyokuwa chini ya Nkosi Chabruma, alishindwa kufikisha ujumbe kwa mtawala (Chabruma).

Hivyo aliwasiliana na msaidizi wa kike wa Chabruma (kwa cheo cha Nduna) aliyejulikana kama Nkomanile. Inasemekana yule mgeni (Omari Kinjala), alianzisha mahusiano na Nkomanile hata siku moja usiku wakiwa kitandani, Kinjala alitoboa siri ya nguvu ya maji na ujumbe aliotoka nao huko Liwale. Baadaye walienda kumshawishi Chabruma kupokea maji na ujumbe wa vita dhidi ya Wadachi ulioletwa. Hivyo ushawishi wa Nkomanile ndio hasa ulisababisha vita vya Majimaji kuingia rasmi katika jamii ya Wangoni kwa mara ya kwanza.

Inaelezwa kuwa baada ya Chabruma kupokea na kukubali ujumbe ule, Mkomanile alitumwa katika maeneo mbalimbali ya Ungoni kupeleka ujumbe wa mapambano dhidi ya ukandamizaji na uonevu uliofanywa na Wadachi.

Alitembea usiku na mchana kwenda tawala za mbalimbali ndani ya Ungoni; ili kurahisisha mapigano dhidi ya Wadachi, Mkomanile alitumika kuandaa vituo vinne vilivyotoa ‘Dawa na Maji’ kwa wapiganaji toka eneo la Mshope lililokuwa chini ya Chifu Chabruma, vituo hivyo inaelezwa kuwepo Namabengo, Lwegu, Uwereka (karibu na Gumbiro ya zamani) na Lukuyu ambapo palikuwa ni makao makuu ya Chifu Chabruma.

Mkomanile pia alipeleka taarifa toka kwa Chabruma kwenda kwa manduna (watawala waliokuwa chini ya Chifu Chabruma (kama wasaidizi) na kwa machifu wengine waliokuwa na tawala zao, mfano Nkosi Mputa Gama wa Njelu. Nkosi Mputa alifika na wapiganaji wake makao makuu ya Chifu Chabruma katika sherehe za unywaji wa Maji ili kujikinga na risasi za Wadachi wakati wa mapambano.

Simulizi nyingine zinamuelezea Mkomanile kama mwanamke aliyekuwa na nguvu kubwa ya uhamasishaji mapambano, ieleweke kuwa wapiganaji wa Kiafrika katika vita hivi, walikuwa ni wanaume tu ambao walijifisha maporini na kuwavamia Wadachi. Walitoka tu nyakati za usiku na kufika vijijini kupata taarifa za Wadachi. Baadaye majeshi ya Wadachi yaligundua kuwa wanawake na vyakula vilivyokuwepo, ndio viliwasaidia wapiganaji wa msituni kuendelea na vita. Hivyo waliharibu mashamba na vyakula kwenye maghala. Hata hivyo, Mkomanile aliweza kwenda kwenye maficho kuhamasisha na kupeleka siri za Wadachi bila kugundulika.

Margareth Bates katika maelezo ya awali ya kitabu cha ‘Utenzi wa vita vya Majimaji’, anaeleza kuwa ‘yule mke wa kinjalla (Omari Kinjala) yaani Bi Mkomanire aliyehofiwa sana na Wadachi, mwishoni alikamatwa pia na kunyongwa kama walivyonyongwa wale viongozi wengine wa Maji Maji( au Hongo Hongo)’. Hii inathibitisha kuwa Mkomanile alifanya kazi kubwa sana katika kuwezesha vita vya kuwakomboa Watanganyika wengine, huu ni ushujaa mkubwa na wa kuigwa na Watanzania wa leo.

Bila shaka hatuna tena vita vya kwenda msituni, bali tunapaswa kusimama imara kupambana na umasikini unaochangiwa hasa na rushwa, mikataba mibovu na uongozi mbaya.

Hadi mwisho wa vita ya Maji Maji katika jamii ya Wangoni, wanawake wengi walishiriki kwa namna moja ama ingine katika kusaidia harakati hizo, ingawa jina la Mkomanile ndio linabaki kama alama ya uzalendo na ushujaa kwani alinyongwa tarehe 27, Februari 1906 na mashujaa wengine wa wanaume waliojitolea maisha yao ili kuondoa utawala wa Kidachi.

Kwa kuhitimisha makala haya, namnukuu msomi maarufu na mwandishi wa vitabu vya kiharakati Frantz Fanon katika kitabu chake kinachoitwa ‘Black Skin, White Masks’, anasema kwamba ‘Hoja sio kujua mambo ya ulimwengu, bali kuyafanyia mabadiliko’. Hivyo kwa sisi Watanzania na Waafrika kwa ujumla, haitoshi tu kujua matatizo yanayotusumbua, bali kupambana nayo na kuleta mabadiliko ya kweli.

+919513833624

Mnara katika kaburi la mashujaa

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.