Afrika imekuwa jalala la tamaduni za nje

Rai - - MAONI / KATUNI - NA HUSSEIN SIYOVELWA

Afrika ndilo bara lenye majaliwa ya maliasili nyingi zaidi. Utajiri wa maliasili, ardhi kubwa yenye wakazi wachache sana, hali ya hewa yenye kuruhusu shughuli za uzalishaji kwa kipindi chote cha mwaka na halikabiliwi sana na majanga makubwa ya kiasili.

Hata hivyo, Afrika ndilo bara linalokabiliwa zaidi na majanga ya kiutu kama umasikini, maradhi, ujinga, njaa, vita, utumwa, ukoloni, nk.

Kadiri siku zinavyosonga, Afrika inazidi kupoteza kabisa utamaduni wake. Afrika limekuwa jalala la tamaduni za nje—hasa zile zinazokuja kwa sura ya kidini. Takribani miaka 60 Afrika ilijitoa katika ukoloni wa moja kwa moja—lakini bado imekumbatia kwa nguvu zote mawakala wa ukoloni hasa dini.

Katika Afrika kuwa Mkristo au Muislamu ni fahari kubwa, na ndio kustaarabika. Kinyume chake unaambiwa humwamini Mungu. Yaani kama huko katika dini hizo, basi humwamini Mungu.

Nina hakika hakuna Wafrika katika dini za Kihindu, kwa vile tu wenyewe hawataki. Wakifungua milango leo, kesho utakuta mapateli kibao miongoni mwa Wangoni—tena watajifanya wao wana imani kuliko Wahindu wenyewe.

Matokeo ya yote hayo, ni confusion (kuhamanika) tu katika jamii za Kiafrika. Tunatafuta ufumbuzi wa changamoto zetu katika majukwaa ya kisiasa, hali tatizo ni la kijamii zaidi.

Vitabu vya dini tunavyo vikumbatia vinatuambia sisi ni kizazi cha laana. Nasi tunaridhika na upuuzi huo na kuutangaza— kwamba sisi ni wahanga wa laana ya baba yetu Nuhu. Wapi na wapi.

Nimejitahidi kwa miaka yote kutafuta uhusiano wangu na Nuhu, sijawahi kuiona. Binafsi naamini Afrika haiwezi kuwa na laana ya Nuhu, lakini dalili za laana zibaonekana katika Afrika.

Rasilimali zetu zinaporwa kirahisi kabisa, huku wenyewe tukishangilia. Vipaji vyetu hatuvitumiii, lakini mbaya zaidi, tunawezesha mafanikio ya wenzetu kwa namna mbali mbali, huku wenyewe tukizidi kuangamia katika majanga ya kujitakia. Lazima tuna laana.

Binafsi naamini kusaliti mila na tamaduni zetu, ndio msingi wa laana yetu. Angalia kama ni ukoloni, hata Wahindi na Warabu walitawaliwa—tena kwa vipindi virefu zaidi. Lakini walimudu kubaki na utambulisho (identity) wao hata leo.

Mwafrika ukimtawala leo, kesho atakuwa amebadili kila kitu chake kumfuata bwana wake. Binafsi natangaza rasmi kujitoa katika dini zote, ili nipate kumjua na kumwabudu Mungu kwa usahihi zaidi, na nijitoe katika laana ya Uafrika. Laana ya Uafrika Afrika ni sehemu pekee duniani ambapo kiongozi wa nchi anaweza kusema hadharani kwamba wanapigana vita na nchi jirani, au vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya nchi, kwa vile wanachonganishwa na Wazungu. Yaani mtu mzima anakiri upumbavu wa kuchonganishwa hadharani, halafu wananchi wanamshangilia.

Eti “wanatuchonganisha tupigane ili watuuzie silaha. “hebu pima hiyo kauli. Halafu imekuwa ya kawaida kabisa katika midomo ya wasomi wetu, wanasiasa wetu, wanahabari wetu, na hata viongozi wetu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.