Siku ya Krismasi, masimulizi na uhalali wake

Rai - - MAKALA - NA MWANDISHI WETU

MWANZONI mwa wiki hii mamilioni ya Wakristo Duniani, walisheherekea siku kuu ya Krisimasi ambayo inatajwa kama siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Hata hivyo kumekuwa na maswali, mijadala na masimulizi mbalimbali juu ya baadhi ya sikukuu za kidini, hasa sikukuu ya Christmass (Krisimasi), ambayo inaelezwa kuwa ni maalum kwa maadhimisho ya kuzaliwa kwa mkombozi wa Wakristo, Yesu.

Wadadisi na wafuatiliaji wa mambo, wanaieleza siku ya Desemba 25, kuwa si sahihi na rasmi kuipa hadhi ya kusheherekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Hoja hiyo inatazamwa na ushahidi wa Kibiblia ambao hauoneshi Yesu alizaliwa mwezi gani wala tarehe gani na hata ushahidi wa kihistoria unatanabaisha kuwa Yesu Kristo alizaliwa katikati ya mwaka 5 kwenda wa 6.

Kwa muktadha huo historia inaonesha Yesu Kristo alizaliwa miezi ya katikati ya mwaka na wala si mwishoni mwa mwaka kama inavyoadhimishwa sasa.

Pamoja na mapokeo ya sikukuu hiyo ambayo kwa mwaka huu imeadhimishwa Jumanne ya wiki hii ni vema wakristo tukakumbushana baadhi ya mambo muhimu.

Katika Injili zote ndani ya Biblia Takatifu hakuna mahali popote palipoandikwa kuwa Yesu Kristo alizaliwa majira yapi wala tarehe ipi, badala yake tunaona ushuhuda wa Yesu Kristo ambaye inasimuliwa kuwa ni Mungu aliyeuvaa mwili kisha akazaliwa kwa mfano wa mwanadamu.

Kuzaliwa kwa Yesu Kristo kunaelezwa wazi wazi katika Injili ya Mathayo 2:1-16, na katika Injili ya Luka 2:1-7.

Tangu kuzaliwa kwa Yesu, hata wakati wa utoto wake, wakati wa huduma yake hapa duniani, wakati wa mitume na hadi kufika mwaka wa 349 AD hapakuwa na sherehe ya kuzaliwa kwa Yesu.

Si kwamba maadhimisho hayo hayakufanyika Desemba 25, pekee bali hayakuwahi kufanyika kabisa.

UJIO WA SIKUKUU HII

Umekuwa ni utamaduni wa kimapokeo, kila inapofika mwishoni mwa mwaka watu husheherekea siku ya Krismasi.

Utaratibu huu unatajwa kuanza kupewa nafasi mwaka 350 AD, wengi huamini kuwa ndiyo tarehe ambayo Yesu Kristo alizaliwa.

Swali la kujiuliza ni je, Yesu alizaliwa katika tarehe hiyo? Ukweli ni kwamba kabla ya mwaka 350 AD, sherehe ya Krismasi haikuwepo kabisa, na wala hapakuwepo na maadhimisho ya Yesu kuzaliwa katika hadi ulipofika mnamo mwaka 350 AD wakati ambao papa wa kanisa la Roman Catholic (RC) aliyejulikana kwa jina la Julius I alipotangaza rasmi kuwa tarehe 25 Disemba ndiyo itakuwa siku ya kusheherekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Julius I alifanya hivyo kwa lengo la kuifuta na kuifidia siku ambayo wapagani walikuwa wakisherehekea kuzaliwa kwa “mungu” wao (JUA) na mwanzo wa majira ya “Spring” (kipupwe). Kipindi ambacho mimea huchipua.

Katika majira hayo pia kulikuwa na sikukuu ya wapagani wa Kirumi ijulikanayo kwa jina la “Roman Saturnalia” ambayo pia Warumi walikuwa wanampa heshima “mungu” wao “Saturn” (sayari ya Satan), ambaye wao walikuwa wanamwabudu kuwa ndiye “mungu” wao wa mavuno.

Warumi walikuwa wanaadhimisha sherehe hiyo kila Desemba 19 na ilikuwa inaadhimishwa kwa siku saba mfululizo na kilele chake kilikuwa ni Desemba 25.

Hata katika Ulaya kaskazini, pia nao walikuwa wanaadhimisha sherehe ijulikanayo kwa jina la “Yule” ambayo pia waliifanya kwa heshima ya “mungu” wao kwa kuwa katika majira hayo ndipo wakati ambao majira ya baridi yalikuwa yanamalizika na jua lilianza kuchomoza.

Siku ya Christmas hayamo ndani ya Biblia, kwa maana hiyo ni sikukuu ya kimapokeo yaliyowekwa na wanadamu, na kwamba si tarehe sahihi ambayo Yesu Kristo alizaliwa.

Ndio maana yapo mataifa yanayoadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Januari, na mengine wanaadhimisha miezi mingine kulingana na mtazamo wao.

Ukweli wa Desemba 25, kuadhimishwa kama sherehe ya kuzaliwa kwa Yesu yametokana na fundisho la Julius I wa kanisa la RC ambaye aliliweka kulingana na mitazamo yake yeye mwenyewe japokuwa neno “Christmas” likinyambuliwa unapata jina “Christ - Mas” ambalo maana yake inakuwa “Christ” “Kristo”, na “Mas” ambalo linatazamwa kwa maana mbili moja ni Misa na pili ni kusanyiko.

Kutokana na ukweli huo, Wakristo wanapaswa kusheherekea siku ya kuzaliwa kwa mkombozi wao kila siku kwani hakuna mahali popote panapoonesha siku rasmi ya kuzaliwa kwa Yesu.

Uthibitisho wa Yesu Kristo kuzaliwa katikati ya mwaka wa 5 kwenda wa 6 b.C (K.K) pia unatibitishwa na Biblia inayojulikana kama Life Application Study Bible, katika ukurasa wa “A20”.

Kwa takwimu hizo, hata mwaka wa kwanza A.D (b.K) Yesu Kristo tayari alikuwa na umri wa miaka mitatu unusu! Na hapo pia panapingana na ile dhana inayosemwa kuwa Yesu alipozaliwa ndipo miaka ikaanza kuhesabiwa kwa mfumo wa A.D.

Pamoja na mambo mengine wakristo wanatakiwa kuutafuta wokovu na si kuitafuta tarehe ambayo Yesu alizaliwa kwani kila siku inapaswa kuwa kukumbuku ya kuzaliwa kwa Yesu na thamani ya wokovu.

Masimulizi mbalimbali yanaonesha kuwa Desemba 25, ni tarehe aliyozaliwa “Tammuz” ambaye wapagani waliamini kuwa ni mungu wao wa mimea na mazao.

Wapagani waliazimisha kuzaliwa kwa Tammuz kila inapofika tarehe hiyo. Hata hivyo wapo wanaodai kua Kanisa chini ya kiongozi Constantine likaamua kuingiza siku hii kama siku ya kuzaliwa Yesu ili kuwavuta wapagani wajiunge na kanisa ili kuongeza mapato ya kodi.

MATAWI YA MITI

Masimulizi ya kale yanaeleza kuwa mti wa Christmas ni ishara ya kuzaliwa kwa Tammuz ambaye wapagani waliamini kuwa ndiye mungu wa mimea na mazao.

Hali hiyo inasababisha matawi ya mti huo kutumika kwenye kupamba siku kuu hiyo, ambapo wakristo hutumia mapambo ya kila aina kupamba matawi ya mti huo.

Hata hivyo tahadhari inatolewa kwa wakristo kote duniani kuifanya biblia kuwa mwongozo wao na si kufuata mambo ya kimapokeo.

Hata katika Ulaya kaskazini, pia nao walikuwa wanaadhimisha sherehe ijulikanayo kwa jina la “Yule” ambayo pia waliifanya kwa heshima ya “mungu” wao kwa kuwa katika majira hayo ndipo wakati ambao majira ya baridi yalikuwa yanamalizika na jua lilianza kuchomoza.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.