Ubora wa barabara kichocheo cha utalii

Rai - - MAKALA -

Hifadhi ya Ruaha ni ya kwanza kwa ukubwa nchini ikiwa na kilomita za mraba 20,226 na imetambaa katika vijiji 64 vya mikoa ya Iringa, Mbeya na Dodoma.

Hifadhi ya Ruaha inatajwa kuwa kivutio bora kutembelewa duniani kwa muda wote kutokana na kutawaliwa na aina mbalimbali za wanyama, ndege, mimea na hata samaki wanaopatikana muda wote wa mwaka.

Ruaha inasifa ya kuwa hifadhi yenye Simba wanaokusanyika kwenye makundi makundi huku kila kundi likiwa na kati ya Simba nane hadi 25.

Aidha ndiyo hifadhi inayoweza kukufanya uwaone wanyama wengi kwa urahisi tofauti na maeneo memngine ya hifadhi duniani. Pamoja na uzuri na ubora wa hifadhi hiyo, bado ipo changamoto kubwa ambayo inaweza kurudisha nyma kabisa jitihada za kuchochea utalii nyanda za juu Kusini.

Changamoto iliyopo ni badabara na hasa daraja la Idodi, ambalo linaiunganisha Idodi na hifadhi hiyo. Badarabara ya kuelekea Hifadhini kutokea Iringa mjini imegawanyika katika maeneo mawili.

Enao moja la barabara hiyo ambalo ni dogo limepambwa kwa lami, ambayo utakutana nayo mwonzoni mwa safari yako na itaishia kwenye kijiji cha Ibangamoyo.

Baada ya kumaliza kijiji hicho, utasafiri kwa umbali mrefu mno ukitumia barabara ya vumbi, ambayo itakupitisha kwenye vijiji kadhaa vikiwemo Mangalali, Mzihi, Kidamali, Nyamhuu, Mgwasi na Mgwasi.

Katika eneo hili la Mgwasi zipo kona kali na za hatari zilizonakshiwa na miteremko ambayo inahitaji umakini mkubwa kupambana nayo.

Mbali na hali hiyo, lakini pia yapo maeneo ambayo yanaweza kuwa kikwazo cha kufanikisha nia ya utalii, kutokana na barabara ambayo ni ya vumbi kutawaliwa na vituta vidogo vidogo vingi.

Shemu ya pili ambayo utakutana tena na lami ni kijojo cha Tungamelnga, ambacho ndicho kinakukaribisha hifadhini, lami iliyopo si ya umbali mrefu hata hivyo ujenzi wake unaendelea, hili ni jambo jema.

Vituta hivi si vya kutengenezwa, bila shaka vimejitengeneza kutokana na mazingira ya barabara yenyewe, vinakera na kuchosha mwili.

Ipo haja kwa wahusika iwe ni Hifadhi, TANROAD au Tarura kuangalia namna sahihi ya kushughulikia hali hii kwenye barabara yote ya kuelekea hifadhini.

Ili kufika Ruaha kutokea Iringa, kuna njia moja ambayo inakupeleka mpaka ilipo njia panda ya kuingia hifadhini.

Njia moja kati ya mbili zilizopo njia panda, inaurefu wa Kilomita 59 na inakupitisha kwenye vijiji vya Idodi, Mapogoro na Tungamalenga na njia ya pili ina urefu ya kilomita 70 na haipakani na kijiji chochote kile. Hii inamaanisha kuwa njia salama na yenye kufikika kwa haraka ni hii ya kupitia Idodi, ukweli wa hili unatoa ishara kwamba ipo haja ya kuitazama njia hii na madaraja yalimo ndani yake kwa jicho pana zaidi ili ilete tija kusudiwa.

Wananchi waishio pembezoni mwa hifadhi hiyo, wamewaeleza Waandishi wa Habari wa Mazingira waliofanya ziara kwenye hifadhi hiyo chini ya mwavuli wa JET kuwa ipo haja ya makusudi ya kuliboresha daraja la Idodi.

Ukiliangalia daraja hilo utabaini kuwa mbao zinazotumika kupitia magari, baiskeli na hata watu, zimechoka na kuanza kujiachia huku vyma vilivyoshikilia mbao hizo vikiwa imara na madhubuti.

Danny Salum, mkazi wa Idodi alisema katika mambo mazuri yanayofanywa hifadhi kwa kushirikiana na wananchi yanaweza kukosa maana kama hakutakuwa na namna sahihi ya kulishughulikia daraja hilo.

“Tunashirikiana sana na hifadhi, lakini tunashangazwa na hatua hii ya kutoshughulikiwa kwa daraja hili la Idodi, kiukweli hatuelewi tatizo liko wapi, maana njia hii ndio fupi na salama kwa mtalii kufika hifadhini,”alisema.

Kwa upande wake Edifonce Singo, alisema anafurahia hatua ya mlaka husika kuzifuatilia hifadhi za Taifa, lakini bado anaamini hakuna mkazo katika kuangalia barabara na madaraja hasa yanayoelekea hifadhini.

Michael Kindimbo aliweka wazi kuwa anaamini hali ikiendelea kama ilivyo sasa ni wazi daraja hilo litafikia hatua ya kutokupitika kabisa.

“Hivi mtu anawezaje kufikiria kwenda hifadhini kwa kupitia njia hii wakati daraja ni bovu, sisi tunaamini kitendo cha watalii kupita njia hii ya Idodi, kitatusaidia hata sasa kujiongezea kipato kwa maana biashara zetu ndogo ndogo zitapata wateja wa uhakika, tunaiomba Serikali ilitazame daraja hili,” alisema.

Kwa upande ake Afisa Tarafa ya Idodi, Yakub Kiwanga, alikiri kuwapo kwa ubovu kwenye daraja hilo, hata hivyo alisema anaamini serikali imeliona tatizo hilo na italifanyia kazi.

Mwezi Aprili mwaka jana, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu aliwahi kutoa ahadi ya kuiboresha barabara hiyo ili ilete tija kusudiwa. Alitoa kauli hiyo katika mkutano wake na viongozi wa hifadhi hiyo na wa Mkoa wa Iringa baada ya kufanya ziara fupi katika hifadhi hiyo pamoja na kujionea utiririshaji hafifu wa maji katika Mto Ruaha uliosababishwa na shughuli za kibinadamu hasa kilimo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mama Samia alisema serikali itahakikisha barabara hiyo inajengwa kwa awamu kwa kiwango cha lami kama hatua ya kuongeza maradufu idadi ya watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambako kutokana na ubovu wa barabara kuelekea hifadhini hapo, idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo imeendelea kupungua kila uchao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.