Unene, ufupi mateso kwa raia Marekani

Rai - - AFRIKA - HASSAN DAUDI NA MITANDAO

UTAFITI mpya wa Kituo cha Tiba na Udhibiti wa Magonjwa Marekani (CDC) umebainisha kuwa raia wa taifa hilo wanakabiliwa na changamoto hiyo. Kwamba watu wake wataongezeka uzito na kuwa wafupi kadiri miaka inavyozidi kusogea.

Ripoti ya utafiti huo imeeleza kuwa idadi ya ‘vibonge’ imekuwa ikipanda kwa kasi kwa miaka 10 iliyopita na hiyo ni licha ya kampeni na mikakati ya Serikali katika kuiboresha sekta ya afya.

Ikionesha mfano, wataalamu wa CDC walisema mwaka 1990, ni chini ya asilimia 15 ya waliokuwa wakisumbuliwa na unene lakini muongo mmoja baadaye, kwa maana ya mwaka 2010, idadi yao ilifikia robo ya watu wote.

Kuonesha ni kwa kiasi gai tatizo hilo limekuwa likisambaa kwa kasi, kufikia mwaka huu, tayari theluthi (1/3) ya wananchi wa Marekani wanasumbuliwa na tatizo hilo.

Katika matarajio yao kutokana na takwimu hizo, CDC wanaona baada ya miaka michache ijayo, mwanaume wa Marekani atakuwa na urefu uziozidi futi 5 na inchi 9 tu na uzito wake utakuwa kilo 89. Mwanamke hatavuka futi 5 na inchi 4 na atakuwa na uzito wa kilo 77.

Kwa mujibu wa utafiti wao, kuanzia mwaka 1999-2000 na 2003-2004, mwanaume wa Marekani walikuwa warefu, tofauti na si kwa miaka ya hivi karibuni.

Hivi sasa, watu wawili kati ya watatu huko Marekani wanahaha kusaka tiba ya unene na kila mmoja amekuwa akitumia Dola 1,429 kwa mwaka (gharama za kujinasua), huku wanawake wakiumia zaidi.

Aidha, wajuzi wa masuala ya afya Marekani wanayaona majanga hayo kuwa ni matokeo ya utafiti uliowahi kufanywa na jarida la Mayo Clinic Proceedings (MCP) lililobaini kuwa ni asilimia 97 ya watu nchini humo wanaishi maisha hatarishi kwa afya zao.

Wanaongeza pia kwamba hiyo inaweza kuchochea kasi ya magonjwa kama kansa, moyo, kisukari, kiharusi.

MCP waligundua kuwa ni asimilia tatu pekee ya Wamarekani wanaofanya mazoezi walau dakika 150 kwa wiki moja, wasiovuta sigara, wasiokunywa pombe na vilevi vingine, na wanaokula vyakula vya asili.

Inaelezwa pia kuwa ongezeko la kazi zisizo kuwa na utumizi mkubwa wa nguvu zimechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la vibonge, tofauti na mwaka 1960 ambapo asilimia 50 ya shughuli za kujiingizia kipato zilikuwa hivyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.