Filamu ya Diamond, Basata inaanzia WCB

Rai - - MICHEZO - NA HASSAN DAUDI

SEKESEKE la wanamuziki Nassib Abdul ‘Diamond Platinum’ na Raymond Shaban Mwakyusa ‘Rayvanny’ kufungiwa kufanya maonyesho ndani na nje ya nchi ndilo lililozungumziwa zaidi kweye tasnia ya burudani kwa siku za hivi karibuni. Kwamba hiyo ndiyo habari ya mjini, kama wasemavyo vijana wa kisasa.

Adhabu hiyo ya Baraza la Sanaa la Tanzania (Basata) ilitokana na wasanii hao kutumbuiza wimbo wa ‘Mwanza’, ambao tayari ulishafungiwa kutokana na madai ya kukiuka maadili.

‘Filamu’ hiyo ilichukua sura mpya wiki hii, baada ya Basata kujitokeza kukanusha kile alichodai Diamond kuwa Baraza hilo limeifuta adhabu yao.

Msanii huyo aliyasema hayo akiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Nairobi, Kenya, akisisitiza kuwa waliiandikia barua Serikali na wamesamehewa.

Binafsi sina tatizo na Basata, Diamond, wala lebo yake ya Wasafi Classic Baby (WBC), ila kwa jicho la tatu naliona ‘jipu’ nyuma ya msanii huyo na kama halitatafutiwa suluhisho, basi huenda akaendelea kukumbwa na majanga ya aina hii na kushindwa kupiga hatua katika mafanikio aliyonayo.

Ndiyo, bila kuwataja majina, ipo mifano mingi ya waliowahi kuwika katika muziki wa ‘Bongo Fleva’ lakini leo hii wameporomoka na hawasikiki tena, wakikiri wazi kuwa hawakuwa na watu makini wa kuwaongoza, hivyo kujikuta wakishindwa kuendeleza umaarufu wao.

Huku hapa nchini akiwa kwenye kiwango cha kuwanyima raha wapinzani wake kwenye soko la muziki wa kizazi kipya ‘Bongo Fleva’, ukweli ni kwamba Diamond ni mmoja kati ya wanamuziki wanaofanya vizuri Afrika Mashariki, Afrika na katika baadhi ya nchi za nje ya Bara hili.

Lakini je, aina ya watu alionao kwenye menejimenti yake wanalitambua hilo? Wanatambua kuwa wanamsimamia msanii wa levo za Wizkid, Davido, D’Banj, na wengineo wenye majina makubwa Afrika?

Hivi, hao wanaokuwa naye karibu wakijitaja mbele ya waandishi wa habari kila uchwao kuwa ni mameneja na washauri wanatekeleza majukumu yao ipasavyo?

Inafikirisha na hatimaye kutotoa majibu ya kueleweka kuona nyuma ya uongozi wa watu wenye busara zao kama Said Fella, Hamisi Shaban Taletale ‘Babu Tale’ na Salam SK, wimbo kama Mwanza ulipata nafasi ya kumchafua staa wao Diamond. Hapo ndipo ninapokuwa na wasiwasi na wanaomsimamia.

Kama ambavyo wao wenyewe husema kuwa kabla ya kutoa wimbo huwa wanashauriana, nilitarajia kusikia ‘Mwanza’ ilitakiwa kutoka lakini mmoja kati ya hao amegoma, akisema utaiharibu taswira ya Diamond kitaifa na kimataifa.

Kuonesha umakini mdogo uliopo nyuma ya usimamizi wa Diamond, wimbo ukaachiwa, ukafungiwa na sasa ni doa kwa Diamond, msanii wake, Rayvanny, na lebo yake ya WCB.

Nikikumbushia, unaweza kuona ni hadithi ile ile ya nyimbo za ‘Waka Waka’ na ‘Halleluja’, ambazo video zake zilifungiwa na Basata kutokana na kukiuka maadili.

Kama si wenyewe kujithamini, kuamka na kuanza kuweka mikakati ya kuilinda taswira ya Diamond, basi yeye ndiye anayepaswa kugeuka nyuma na kuangalia aina ya watu alionao.

Uzuri ni kwamba Fela na Tale ni wazoefu, wana uwezo mkubwa wa kuwabana wasanii kama walivyowahi kufanya wakiwa na TMK Wanaume Family na Tip Top Connection (TTC).

Watambue na hata kumwambia kuwa kwa kiwango chake kwa sasa kwenye soko la muziki barani Afrika, Diamond si msanii wa kutegemea ‘kiki’ zisindikize wimbo wake mpya.

Hata hivyo, huenda nao wanahofia kumshahuri hata anapokuwa anaamua jambo la kipuuzi kwa sababu tu yeye ndiye bosi, jambo ambalo ni hatari pia kwake.

Godfrey Mngereza

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.