Demokrasia ya dijitali, siasa za analojia

Rai - - MAONI/KATUNI - „ NA BALINAGWE MWAMBUNGU Kheri ya Mwaka Mpya.

Nilisoma kichwa cha habari hicho hapo juu kutoka habari moja kutoka Kenya iliyoandikwa na mwanaharakati Nanjala Nyabola. Sitarudia nini alikiandika, bali inatosha kwamba mwandishi huyu anaheshimika na vyombo vya habari ndani na nje ya Kenya.

Huko tulikotoka hakukuwa na kompyuta, tulitumia typewriter, badala ya simu za kiganjani, tulitumia simu za upepo na baadaye simu za mezani. WhatsApp, digital printing haikuwapo, na mambo mengine kadha wa kadha.

Enzi hizo, viongozi wetu katika nchi zinazoendelea au dunia ya tatu, walikuwa wanapiga kelele wakidai New International Economic Order (NIEO) na New World Information Order (NWIO), kwa kuwa nchi zao zilikuwa hazifurukuti kiuchumi.

Viongozi hao wa dunia walikuwa wanajua fika kwamba habari (information) ni kitu muhimu sana kwa maendeleo. Lakini nchi zao zilikuwa zinatawaliwa kihabari na mashirika ya habari makubwa matano—Informatsionnoye Agentstvo Rossi (TASS-Russia), Associated Press (AP-USA), Agence France Presse (AFPUfaransa), Reuters (Uingereza).

Kwa upande wa redio, kulikuwa na British Broadcasting Corporation (BBC), Radio France Internationale, Voice of America (VOA), Radio Deutsche Welle (DW-Ujerumani) na Radio Moscow (Urusi).

Kwa ujumla, vyombo hivi vya habari vilikuwa vikiandika habari za nchi zinazoendelea, na kuzirusha kutoka mamao makuu—London, Washington, Paris, Bonn na Moscow, kwa sababu viongozi wa nchi za Dunia ya Tatu, walikuwa wanavibana vyombo vyao vya habari—kwa sababu za kisiasa. Viongozi walipenda kuandikwa wao na mambo mazuri tu wanayoyafanya wao na serikali zao. Hawakupenda kukosolewa.

Waandishi wa habari waliishi katika hali duni na woga. Pamoja na kuwepo kwa vyombo vya habari huru katika baadhi ya nchi, waandishi walishindwa kutimiza ile dhana ya kwamba wao (wanahabari) ni sauti ya wananchi. Vyombo vya habari, kwa ujumla vikawa sauti ya watawala. Mabunge ambayo yanapaswa kuwa wawakilishi wa Wananchi, yakageuzwa kuwa ‘rubber stamp’ –yakawa yanapitisha hoja bila mijadala ya kina.

Kwa hiyo, wananchi walikuwa wanaamini sana habari za kwao zilizokuwa zinatangazwa na mashirika ya nje—ambayo kwa bahati mbaya sana, yalikuwa yakitangaza zaidi habari za matukio mabaya (negative news)—ndio maana viongozi wa nchi za Dunia ya Tatu wakawa wanadai mfumo mpya wa habari duniani (NWIO).

Wakati viongozi wetu wanadai mfumo mpya wa uchumi na habari, nchi za Magharibi—husan Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani Magharibi (wakati huo), zilikiwa zinapanga mpango wa kuleta mfumo mpya wa soko huria, teknolojia mpya (IT), na mfumo mpya wa vyama vingi vya siasa.

Kwa sehemu kubwa, nchi za Magharibi zilifanikiwa katika mipango hiyo. Ziliuvuruga mfumo msonge wa vyama tawala katika nchi za Dunia ya Tatu, na kuuvunja mfumo wa tawala za kimabavu za Ulaya Mashiriki na kusababisha kusambaratika kwa Shirikisho la Jamhuri za Kisoshakisti la Urusi (USSR).

Nchi ya Kenya kwa sasa, inaelezwa kwamba ndio nchi inayoongozwa kwa maendeleo ya kidijitali Kusini mwa Jangwa la Sahara katika maambo ya Twitter, WhatsApp, facebook na mitandao mingine kwa matumizi katika maisha ya kila siku ya Wananchi. Katika nchi za Magharibi, matumizi ya dijitali yamechukua nafasi kubwa katika maisha ya kijamii—kiasi kwamba mfumo wa mzima wa jamii umevurugika na kuleta ushawishi hasi katika mambo yote pamoja na siasa. Sakata la uchaguzi mkuu wa Marekani uliomwingiza Rais Donald Trump madarakani, ni ushahidi tosha.

Katika nchi nyingi za Kiafrika, watawala wamekubali kuukumbatia mfumo wa kiditali, lakini kuna kukatiza (resistance) ya kuendesha siasa kidijitali, wanajaribu kurudi kwenye mfumo wa kianajojia (analogue)—mfumo ambao dunia nzima imetambua kwamba umepitwa na wakati.

Tumeona hata hapa kwetu tuliachana na siasa za analojia zaidi ya miaka ishirini sasa. Lakini mwaka uliopita tumeshuhudia zikitumika mbinu chafu za kuendesha siasa kwa maelezo ya kipropaganda—eti Nyumbani Kumenoga. Nini kimenogesha na kuwafanya viongozi wa upinzani kurejea kule walikokukataa?

Watu wenye umri mkubwa tunaitwa kizazi cha analogue, vijana wanaitwa dijitali. Sasa najiuliza mbona wanasiasa— tena vijana, wanadai kwenye analojia kumenoga!

Tanzania ilikwisha sema kwa heri mfumo wa chama kimoja kwa zaidi ya miaka 20 sasa, nachelea kusema kwamba wanaopiga debe la nyumbani kumenoga, wapuuzwe. Sisi tuliotoka kwenye mfumo wa zamani wa chama kimoja, tunajua uzuri na ubaya wake. Tunapaswa kuwasaidia vijana wasiojua masaibu ya utawala wa chama kimoja. Tuwasaidie kuwafumbua macho na akili—wasishabikie na wasiende huko tulikotoka— analogue haitarudi tena. Nchi zinazoendelea hazitaweza tena kudai NIEO, uchumi wa kidigitali umeifanya dunia kuwa kijiji. Habari toka pande zote za dunia—mijini na vijijini, zinapatikana kiganjani mwa mtu wa kawaida—saa zote wakati wote. Anachagua angalie nini na asome nini. Hakuna tena madai ya NWIO.

Vijana wapiganie kujenga misingi yao (kizazi kipya) ya jamii inayovumiliana, inayoshindana kwa hoja, inayokubali kukosoa na kukosolewa—inayokiri pale inapobidi—kwamba imekosea na inayosikiliza sauti za makundi yote.

Muhimu zaidi, vijana wajue na waelewe kwamba Tanzania sio nchi ya kundi, au chama fulani. Ni ya wananch wote na makundi yote. Hakuna mwenye Tanzania yake. Vijana wasiruhusu kumwachia mtu, au kundi, kufanya mambo yanayo ondoa umoja na mshikamano waliotuachia waasisi wa Taifa letu.

Demokrasia ya Dijitali, Ndiyo, Siasa za Analojia, HAPANA. Huu ndio uwe mwelekeo wa Tanzania tunayoitaka.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.