Ndoto ya Ufaransa kuitawala dunia ilivyoshindwa

Rai - - MAKALA - NA MBWANA ALLYAMTU GALLIA

Ufaransa ni moja wapo ya nchi zinazounda Bara la Ulaya, pia ni mwanachama mwanzilishi wa Umoja wa Ulaya. Mji wake mkuu ni Paris. Eneo lake lina ukubwa wa km² 674,843 huku likiwa na idadi ya wakazi ni 63,044,000. Nchi hiyo imepakana na Ubelgiji, Luxemburg, Ujerumani, Uswisi, Italia, Monako, Andorra na Hispania.

Ina pwani ndefu kwenye bahari ya Atlantiki pande za kaskazini na magharibi, Mediterranean upande wa kusini. Kiuchumi ni taifa la tatu barani ulaya kwa ukubwa wa uchumi huku likiwa taifa la sita kwa uchumi mkubwa duniani kwa kuwa na GDP ya Dola za Marekani trilioni 1.6449.

Ufaransa pia ina maeneo mengi ya ng’ambo yaliyokuwa makoloni yake zamani, lakini kwa sasa ni sehemu rasmi za Jamhuri ya Ufaransa na wakazi wao ni raia wenye haki zote kutoka Ufaransa. Kati ya maeneo haya kuna visiwa katika Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kusini, Bahari ya Caribian, Afrika, Bahari Hindi pia na Bahari ya Pacific.

Lugha ya taifa ni Kifaransa lakini kuna lugha za maeneo kama vile Kibaski, Kibretoni, Kikatalani, Kikorsika, Kijerumani, Kiholanzi na Kioxitania. Wahamiaji kutoka nchi zilizokuwa koloni za Ufaransa walileta pia lugha zao, hasa Kiarabu na Kiberber kutoka Afrika ya Kaskazini.

Ufaransa haina dini rasmi lakini wakazi walio wengi asilimia 75 ni Wakatoliki. Takriban milioni nne mpaka tano hivi ni Waislamu kitu kinachoifanya kuwa nchi ya kwanza ulaya kuwa na waislamu wengi ambao ni raia. Pia wakazi wengi ni wahamiaji kutoka koloni za zamani katika Afrika ya Kaskazini au Magharibi pamoja na watoto wao. Wafaransa wanapenda sana michezo hasa mpira wa miguu. Ufaransa ilikuwa kati ya nchi zenye makoloni mengi duniani ikasambaza lugha yake kote duniani na kutunza uhusiano wa pekee kabisa na nchi hizo zinazotumia Kifaransa hadi sasa.

Na mnara wa Eiffel ulipo jijini Paris ni moja ya vivutio vikubwa na alama ya taifa hilo.

HISTORIA YA DOLA YA GALLIA (GALLIC)

Ufaransa ilikaliwa na watu tangu muda mrefu sana. Utafiti wa akiolojia umeonyesha vifaa vya mawe vyenye umri wa miaka 100,000 iliyopita (rejea kitabu cha “The history of Gallic”- Kelvin Shillington)

Watu wa Ufaransa waliingia katika historia andishi kupitia taarifa za waandishi wa Roma ya Kale walioeleza habari za majirani wao Wagallia katika Italia ya kaskazini na Ufaransa wa leo. Hao Wagallia walikuwa Wakelti na mara kwa mara katika hali ya vita kati yao na Waroma. Kuanzia mwaka 58 BC Juliasi Caesar mwasisi na mwanzilishi wa dola la Roma (Holy Roma Empire) aliteka na kutawala Gallia yote kwa niaba ya Dola la Roma kwa zaidi ya miaka 300 hivi.

Gallia ikaendelea kuwa moja ya majimbo tajiri ya Roma na wakazi wengi walitumia lahaja za Kilatini kilichopata kuwa mama wa Kifaransa ya kisasa hapo baadae. Lahaja za Kikelti zilibaki katika maeneo ya kando tu, kwa mfano Bretagne. Polepole wakazi wengi walipata kuwa Wakristo wa Kanisa Katoliki.

KUANZA KWA MILIKI YA FRANKI

Wakati wa kuporomoka kwa Dola la Roma makabila ya Kigermanik yaliingia katika eneo la Ufaransa na kuchukua utawala wa nchi mikononi mwao. Kabila la Kigermanik la Wafaranki lilitawala sehemu kubwa ya Ufaransa pamoja na Ujerumani ya magharibi mnamo mwaka 500 AD. Mfalme wao Chlodwig (tamka klod-vig) alipokea Ukristo wa Kikatoliki kama dini rasmi ya milki yake. Lakini pia Mfalme wao Karolo Mkuu alipanua mipaka ya milki hadi Ujerumani ya kaskazini na Italia na mwaka 800 akapokea cheo cha Kaisari wa Roma kutoka mikono ya Papa Leo III.

Baada ya kifo cha Karolo na mwanawe, milki iligawiwa kati ya warithi kwenye mkataba wa Verdun wa mwaka 843. Miaka 100 baadaye mtemi wa Paris Hugo Capet alichukua nafasi ya wajukuu wa Karolo na wafuasi wake waliendelea kuimarisha mamlaka ya kifalme.

Ugawaji wa mwaka 843 ulikuwa chanzo cha Ufaransa kama nchi ya pekee. Mwanzoni ilijulikana kama “milki ya Wafaranki wa magharibi” ilhali sehemu za Ujerumani ziliitwa “milki ya Wafaranki wa mashariki”. Lakini Wagermanik katika Ufaransa walikuwa wameshaacha lugha yao asilia na kutumia kile KilatiniKifaransa cha siku zile. Wafalme wa sehemu hizo walikuwa dhaifu mwanzoni na mamlaka kubwa ilikuwa mikononi wa makabaila katika majimbo ya ufalme.

UFARANSA NA UINGEREZA KATIKA SURA MPYA

Kwa karne kadhaa historia ya Ufaransa ilikuwa na ugumu wa kipekee kutokana na mchanganyiko wake na historia ya Uingereza.

Mwaka 1066 mtemi William wa Normandi (Willium Mshindi) aliyekuwa chini ya mfalme wa Ufaransa alivamia Uingereza na kuwa mfalme huko lakini yeye pamoja na warithi wake waliendelea kuwa watemi wa jimbo la Normandi. Kwa njia hiyo watemi wa Normandi waliingia mara nyingi kwa nguvu katika siasa ya Ufaransa. Baada ya kifo cha mtawala wa mwisho kutoka ukoo wa Hugo Capet Wanormandi walidai cheo cha mfalme wa Ufaransa na hii ilikuwa chanzo cha vita ya miaka 100.

Mwishowe Waingereza walipaswa kuacha karibu mali yote kutoka urithi wa Wanormandi. Hata hivyo kilele cha ufalme hadi mapinduzi ya 1789, milki ya Ufaransa iliendelea kuwa nchi yenye nguvu Ulaya ambapo ilivutana na mataifa mengi.

Katika vita ya miaka 30 (1618 - 1648) iliweza kujipatia nafasi ya mwamuzi katika siasa ya Ulaya. Wakati huohuo matengenezo na kuenea kwa dini ya Kiprotestanti yalikuwa yameshaenea na watemi Waprotestanti walitawala maeneo makubwa ya Ufaransa. Mfalme Louis XIV wa Ufaransa aliona hali hiyo kama hatari kwa mamlaka yake, akafuta ahadi zote kwa Waprotestanti walioondoka nchini kwa wingi.

Baada ya Louis XIV, waandamizi wake waliongeza madeni ya serikali kwa vita vingi dhidi ya Uingereza na ujenzi wa majumba makubwa. Matatizo makali ya kiuchumi pamoja na mawazo mapya ya zama za mwangaza yalisababisha mapinduzi ya Kifaransa ya mwaka 1789.

Mamlaka ya mfalme iliondolewa na baada ya kipindi jamhuri kutangaziwa ilhali mfalme alishtakiwa kuwa msaliti na kupewa adhabu ya mauti.

MAPINDUZI YA UFARANSA MWAKA 1789

Mapinduzi ya Ufaransa (kwa Kifaransa: Révolution française) ni jina linalojumlisha matukio muhimu ya siasa kwa kipindi cha miaka 10, tangu 1789 hadi 1799, yaliyobadilisha uso wa Ufaransa na utamaduni wa Ulaya kwa jumla, kiasi cha kuhesabiwa kati ya matukio makuu ya historia yote. Kupitia vita mbalimbali vilivyofuata sehemu mbalimbali za dunia, taarifa zake zilieneza kote duniani fikra za haki za binadamu, uhuru na maendeleo zilizotetewa na falsafa ya mwangaza zilitamalaki duniani kote. Dhana ya kuwa mamlaka juu ya dola ni haki ya raia wote, si ya wafalme wala watawala wengine, imeenea polepole pande zote za dunia. Itaendelea wiki ijayo. MWANDISHI WA MAKALA HAYA ANAPATIKANA KWA SIMU NAMBA +255679555526, +255765026057.

Ufaransa pia ina maeneo mengi ya ng’ambo yaliyokuwa makoloni yake zamani, lakini kwa sasa ni sehemu rasmi za Jamhuri ya Ufaransa na wakazi wao ni raia wenye haki zote kutoka Ufaransa. Kati ya maeneo haya kuna visiwa katika Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kusini, Bahari ya Caribian, Afrika, Bahari Hindi pia na Bahari ya Pacific.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.