Mugabe okolea kwenye penzi la Sally kabla ya Grace- 5

Rai - - AFRIKA - NA MPOKI BUYAH [email protected] Simu: 0762155025, 0624027362

Mwana mama Grace Ntombizodwa ni mmoja wa wanawake wenye asili ya ukali asiye na unafiki mbele za watu.

Grace ni mwanamke shupavu na mwenye akili, lakini pia anazo kasoro kadhaa, licha ya kwamba wapo watu wanaompenda kuliko kawaida pengine kulingana na namna anavyojiamini pale anapotatua na ku-deal na mapungufu yake.

Grace Mugabe ndiye aliyewachanganya Wazungu na kumpa majina mengi ikiwemo “Gucci Grace” na wengine walimwita Dis-Grace, lakini majina hayo alipewa kutoka na matumizi makubwa na ya kutisha pale alipokuwa akiingia kwenye maduka ya gharama huko Ulaya katika majiji makubwa kama Paris.

Hakika anapenda makubwa na namfananisha na akina Marie Antoniette, na Alexandria Victoria Melanova wa kule Urusi, na wanawake wengine wengi waliothubutu kuonesha makucha yao pasina hiyana wala uwoga wowote.

Kulingana na umaarufu na utashi wa Grace Mugabe alibadili kabisa sura ya Mugabe na Taifa la Zimbabwe kwa ujumla wake, akavua ukondoo na kuvaa ngozi ya chui. Hakika hakuwa mtu wa kawaida tena wala hakutaka kuona mchezo mchezo unafanyika. Kuna ambao wanamuona kama mwanamke mwenye nguvu na shujaa barani Afrika.

Wanasema kila mtu ana utamu wake na kila mtu ana uchungu wake vilevile ili uvifahamu vyote hivyo ni pale mtu anapopanda cheo ama kupata pesa kwa maana kwamba kutajirika.

Grace ambaye amezidiwa umri wa miaka 41 na Gabriel Mugabe, baada ya ndoa alijiingiza kwenye biashara ya madini, ambapo mpaka leo anamiliki mgodi mkubwa wa dhahabu unaojulikana kama Chiadzwa ambao unamuingizia pesa nyingi. Kutokana na pesa nyingi ambazo amekuwa akizipata kupitia biashara zake, alifanikiwa kujenga majumba makubwa ya kifahari mawili, moja alimuuzia Muammary Colonel Gaddaf mwaka 2007, japo watu walianza kulalamika, lakini Mugabe alimtetea kwamba majumba hayo amejenga kwa hela zake.

Grace Mubage ni moja ya wanawake ambao wanapenda kupewa heshima, lakini vilevile anapenda umaarufu na pesa. Mwishoni mwa mwaka 2007, alikamilisha kujenga jumba lingine la kifahari ambalo liligharimu Dola za Kimarekani milioni 26. Pia anamiliki majumba katika nchi za Malaysia, China na Hongkong, mbali na majumba hayo, anamiliki pia mashamba makubwa nchini Zimbabwe. Mali zote amezipata kwa kupitia mgongo wa Mugabe.

Grace Mugabe ni mwa mama ambaye amewahi kusoma China katika chuo cha Ruminia miaka ya 2007-2008, ambapo huko alijifunza Kichina maana kuna wakati alitaka kwenda kuishi kulingana na hali ya kisiasa iliyokuwa ikiendelea Zimbabwe, japo aliwahi kusema kwamba hata baada ya kumaliza kusoma Kichina, haijui lugha hiyo kiufasaha.

Ukirudi nyuma, miaka ya 2002 aliwahi kwenda Ufaransa kufanya manunuzi ya maana, ambapo alitumia Dola za Kimarekani zaidi ya 12,000 mpaka Wazungu wakashangaa kwamba ametoa wapi fedha nyingi hivyo, licha ya Zimbabwe kuwa kwenye kundi la nchi masikini duniani. Hali hiyo ilisababisha nchi hiyo kuwekewa vikwazo na Bara la Ulaya na kupiwa marufuku ya kuingia katika nchi za bara hilo sambamba na mume wake huku mali zao zikizuiliwa.

Hata hivyo, Grace hakuishia hapo kufanya maajabu yake. Mwaka 2004 alienda Benki Kuu ya Zimbabwe na kutoa pesa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 5.7 kitendo ambacho kiliwashangaza wengi.

Lakini mwa mama huyo wala hakujali na kutokana na matumizi makubwa ya pesa wazungu walimpa jina Gucci Grace maana mwanamke mwenye kupenda vitu vya gharama kubwa kuliko kawaida lakini kulingana na mwenendo wake wa kuwa na matumizi makubwa nchi ya Marekani nayo ilimwekea vikwazo yeye na wafuasi wengine kwamba hakuna kukanyaga Marekani akiwemo Emmason Mnangagwa (Rais wa sasa), Costantino Chiwenga na maafisa wengine wa ngazi juu serikalini.

Grace Mugabe pia ametajwa katika kitabu cha Dinner With Mugabe, kwamba amekuwa na utamaduni wa kuchepuka ama kwenda kutoka nje ya ndoa kwa muda mrefu, kwamba Grace aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Zimbabwe, Gideon Gono.

Kashfa hiyo ilivuma zaidi mwaka 2010 kuwa wawili hao walidumu kimapenzi kwa zaidi ya miaka mitano kutoka mwaka 2005, na waliutumia ukaribu wao kufuja rasilimali za umma, huku wakiwaacha raia maskini wakifa kwa njaa.

Mtandao wa Zambian Observer uliwahi kutaja wanaume wawili, Peter Pamire ambaye alifariki dunia kwa ajali tata ya gari, vilevile James Makamba, aliyetoroka nchi hiyo, kwamba ni wanaume waliowahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Grace.

Aidha, dada yake Mugabe, Sabina ndiye alibaini vitendo vya wifi yake na Gono, na kumweleza Mugabe, kitu ambacho kilizua tafrani ndani ya familia ya Mugabe juu ya tuhuma hizo nzito, ingawa yeye amekuwa akipinga vikali tuhuma hizo na kuwatishia waliokuwa wakivujisha siri hizo kuwapeleka mahakamani.

Grace Ntombozodwa Mugabe, mbali na kuwa mwanamke mkali na mkorofi kama wengi wanavyomtazama, lakini upande wa pili ni mwanamke mwenye upendo wa hali ya juu katika familia yake.

Upande wa pili, mama huyo anaijali familia yake katika kuwaandalia na kuwalea watoto wake katika maadili, isipokuwa anapenda ufahari na maisha ya kitajiri, hivyo na watoto wake wanaishi maisha ya hali ya juu kwa kuishi katika nyumba ya kifahari huko Afrika kusini, Zimbabwe, Hongkong, China pamoja na Malaysia ambako ana makazi huko.

Hata hivyo, hapendi kuona watoto wake hao wanaguswa ndio maana September 11 mwaka 2017 aliingia katika tuhumu nzito ya kumshushia kipigo mwanamitindo Gabriella Engels katika hotel moja maarufu kama Sandton inayopo Johannesburgy. Gabriella Engel hapo awali hakujua kama aliyempiga alikuwa ni First Lady wa Zimbabwe lakini hata alipoona haki imekuwa ngumu kutendeka alisikika akisema “Mimi namuachia Mungu”.

Robert Mugabe akimbusu Grace

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.