Januari itakavyozijenga Barca, Madrid

Rai - - MICHEZO KIMATAIFA - HASSAN DAUDI NA MITANDAO

D

IRISHA dogo la usajili

la Januari limeshafunguliwa na tayari klabu mbalimbali barani Ulaya zimeshaanza kuzifukuzia saini za wachezaji waliokuwa ‘wakiwanyatia’.

Huku macho na masikio ya mashabiki wengi yakielekezwa Ligi Kuu ya England, makala haya yanakuchambulia namna klabu vigogo Hispania, Barcelona na Real Madrid, zinavyoweza kuviimarisha vikosi vyake Januari hii.

Barca wako kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 37 na ni nane zinazowatenganisha na Madrid wanaoshika nafasi ya nne wakiwa wamecheza mechi 16 na si 17 kama mahasimu wao hao.

Hata hivyo, licha ya makali yao, ukizitazama Barca na Madrid, unaweza kuona udhaifu mkubwa katika vikosi vyao, hivyo soko la usajili la mwezi huu linaweza kuzisaidia kujiimarisha.

Tukianza na Barca, kikosi hicho cha kocha Ernesto Valverde kinahitaji beki wa kati anayetumia mguu wa kulia na mlinzi wa kushoto.

Ni kweli mkurugenzi wa soka wa Barca, Eric Abidal, alimsajili beki wa kati anayetumia mguu wa kulia, Jeison Murillo, waliyemng’oa Valencia, akitumia kiasi cha Pauni milioni 25, lakini msimu huu amecheza mechi nne tu.

Akitarajiwa kuwa mrithi wa Gerard Pique, Murillo ameshindwa kuisaidia Barca na ni ngumu kumtegemea, hasa katika hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, yaani 16 bora.

Andreas Christensen wa Chelsea anaweza kuwa mtu sahihi wa kupewa kazi ya Mcolombia huyo katika eneo la beki wa kati na uzuri ni kwamba tayari viongozi wa Barca wameanza kuifukuzia saini yake.

Kwa upande wa beki wa kushoto, Jordi Alba anafanya vizur4i lakini msaidizi wake, Juan Miranda, amechemsha licha ya kupewa nafasi mara kwa mara.

Ukweli ni kwamba kuondoka kwa Lucas Digne kumeiacha Barca ikiwa na uhaba wa mabeki wa kushoto. Hakuna tetesi zozote za Barca kumtaka mchezaji wa eneo hilo lakini Jose Luis Gaya (Valencia) na Emerson (Chelsea) wanaweza kumsaidia kazi Alba.

Inashangaza kidogo kusikia kuwa Barca wanapoteza muda mwingi kuwafukuzia Frenkie de Jong (Ajax) na Adrien Rabiot kwa lengo la kuiimarisha safu ya kiungo, ambayo tayari ina Arthur na Arturo Vidal.

Mahasimu wao wakubwa katika historia ya La Liga, Madrid, wao wana shida ya mfungaji, kiungo wa ushambuliaji na beki wa kati.

Kuondoka kwa Cristiano Ronaldo kumeliacha eneo la ushambuliaji likiwa halina makali. Eden Hazard (Chelsea) na Mauro Icardi (Inter Milan) ni sehemu ya nyota wanaoweza kuipa Madrid aina au idadi ya mabao aliyokuwa akifunga Mreno huyo.

Pia, Luka Modric haonekani kuwa kwenye kiwango chake cha mwaka jana, hivyo eleo la kiungo mshambuliaji linahitaji sura mpya kipindi hiki cha usajili wa Januari.

Huku Isco akihusishwa na mipango ya kusaka makazi mapya nje ya Snatiago Bernabeu, bado kinda waliyemchukua mwaka 2016, Federico Valverde, si mchezaji wa kumtegemea kikosini.

Tetesi zilizopo kwamba Madrid wanataka kutoa euro milioni 20 kumchukua Brahim Diaz wa Man City zinaweza kuwa habari njema.

Mwisho, eneo la beki wa kati la Madrid ni majanga msimu huu chini ya Sergio Ramos na Raphael Varane. Hata wasaidizi wao, Nacho na Jesus Vallejo, nao hawana uzoefu wa kuilinda ngoma ya Madrid.

Beki anayetakiwa Madrid kipindi hiki cha usajili ni mzoefu, kwamba mwenye umri wa zaidi ya miaka 30. Wanaoweza kupatikana kirahisi ni Laurent Koscielny (Arsenal) na Gary Cahill (Chelsea).

Kama si hao, basi ni Matthijs de Ligt wa Ajax, ambaye mwaka jana ndiye aliyeinyakua tuzo ya Kinda Bora wa Ulaya (Golden Boy Award).

Kikosi cha Real Madrid

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.