WARAKA WA ‘KIMITI’ KWA TRA

Rai - - MBELE - NA PRUDENCIA PAUL KIMITI

NIMEGUSWA na jitihada za Rais Dk. John Magufuli za kukusanya mapato. Ukweli ni kwamba taifa lolote lenye maendeleo limefikia hapo lilipo kwa sababu ya kukusanya kodi.

Taifa lisilokusanya kodi, haliwezi kujiendesha na matokeo yake ni kuwa kichaka cha matajiri kuficha na kukimbiza magendo yao huko.

Mimi ni Mtanzania mwenye mapenzi mema na Taifa langu, pamoja na kuishi na kufanyakazi Uingereza, bado nimekuwa nikifanya jitihada za mara kwa mara kuhakikisha napata taarifa sahihi ya kile kinachoendelea nyumbani.

Hatua kubwa ya maendeleo inayopigwa sasa na Rais Magufuli imenisukuma kuandika waraka huu, ili angalau nitimize malengo yangu ya kuwa sehemu ndogo ya mafanikio ya nchi yangu Tanzania.

Kwa miaka 13 sasa nimekuwa nikifanya kazi katika Serikali ya Uingereza, kwenye mji wa Cardiff Kitengo cha Ushuru (HM Revenue and Customs – HMRC).

Nilianzia ngazi ya chini hadi kufikia ngazi ya Meneja Mwandamizi wa timu ya wataalamu wanaoshughulikia Kitengo Maalum cha Ushuru wa Biashara za Kimataifa (Customs International Trade Unit of Expertise).

Nimekuwa kwenye kitengo hiki kwa muda wa miaka mitano tangu nilipoondolewa Idara ya Mapato na kupanda ngazi ya kiuongozi.

Katika kipindi changu cha uongozi, nimefanikiwa kupandisha mapato yatokanoya na ushuru wa forodha na kodi zaidi ya viwango nilivyokuwa nimepangiwa.

Katika kipindi chote hicho, nimeendelea kuona na kujifunza njia mbalimbali za kupatikana kwa mapato kwa nchi ya Uingereza.

Uzoefu wangu huo mdogo umenisukuma kukitumia kipindi hiki cha likizo yangu fupi kuandika waraka huu mfupi kwa walipa kodi (Wananchi) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa lengo la kubadilishana uzoefu na si kufundishana. Niwe muwazi, navutiwa na jitihada za Rais wa sasa wa Tanzania, kauli, matendo na mwendendo wake unaakisi dhamira njema ya kuiacha nchi katika sehemu nzuri na salama.

Anachokifanya Rais Magufuli ni kukusanya kodi kwa nia na dhamira ya kuliletea tija Taifa na manufaa kwa Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa kama anavyopenda kusema mwenyewe.

Napenda ieleweke kwamba popote duniani, hata Uingereza, watoza ushuru huwa hawapendwi na watu wanaotakiwa kulipa kodi, hata Uingereza hali iko hivyo, pamoja na kuwa na elimu kubwa ya kodi .

Kwa mtozwa kodi hawezi kumpenda kiongozi yeyote anayesimamia ukusanyaji wa mapato.

Kiongozi anayethubutu kufanya hivyo huwa mwiba mkali kwa wafanyabiashara. Katika kuhakikisha kazi ya ukusanyaji kodi bila kumwonea mtu inafanyika mara nyingi tumekuwa tukitumia mawasiliano ya simu, barua au barua pepe.

Hatua hii inatokana na maridhiano ya wakusanya kodi na mteja kama mteja ameridhia.

Kulipa kodi ni jukumu la kila mwananchi, kamwe tusikubali kujivua jukumu hili kwa kudhani Serikali inaweza kuleta maendeleo, bila ya kuwa na fedha.

Fedha za kuendesha miradi ya maendeleo, hazitoki mifukoni mwa viongozi bali zinatokana na makusanyo ya kodi zinazolipwa na wananchi popote pale duniani, China, Uingereza na hata Marekani wamefika hapa walipo kwa sababu ya ukusanyaji wa kodi usio na mzaha wala huruma.

Kwa jitahada zinazofanyika na Serikali ya awamu ya Tano na mikakati inayoandaliwa, inaonyesha wazi ya kwamba sasa TRA imedhamiria kuungana na jitihada za Rais katika kukusanya mapato.

Pamoja na hatua hii nzuri, najiona ninalo jukumu la kutoa ushauri kwa TRA. Mamlaka hii inayojukumu la kuendelea bila kuchoka kutoa elimu kwa walipa kodi na wananchi kwa ujumla.

TRA haipaswi kuogopa kutumia mapato yake katika kuelimisha Watanzania, jamii inapaswa kuujua umuhimu wa kodi. Kwa mataifa yaliyoendelea umuhimu wa kodi unaaza kutolewa tangu shule za awali na ndio maana nchi nyingi duniani huwa hazina misamaha ya kodi.

Hata hivyo siipingi misamaha ya kodi kwenye baadhi ya maeneo, lakini ipo haja huko tuendako kuachana na utaratibu huu, badala yake ukawekwa utaratibu rafiki, utakaomwezesha mlipa kodi kulipa deni lake polepole.

Natambua wazi kwa sasa idadi kubwa ya wananchi wanauelewa mdogo wa masuala ya kodi hali inayoibua malalamiko ambayo yanamsingi kwa sababu hawana elimu ya moja kwa moja ya umuhimu wa kulipa kodi.

Nchini Uingereza wao hawasemehe kodi na katika kufanikisha hilo, wanaeleza wazi kuwa kutokujua umuhimu wa kodi hakukupi nafasi ya kusamehewa kodi, kwa lugha nyepesi wanasema ‘ignorance is not a reasonable excuse’.

Nashauri matangazo ya umuhimu wa kulipa kodi yaendelee kila sehemu. Kwa mfano, Uingereza miaka michache iliyopita, tuliweka matangazo hadi kwenye mashine za pesa (ATM Machine) wakati unaingiza kadi yako kutoa hela, unapewa ujumbe wa kulipa kodi.

Ni vizuri TRA ikaangalia mifumo mbalimbali inayotumika katika nchi nyingine na kuona haja ya kuipandikiza nchini kama itaonekana kuwa yenye tija.

Aidha, wananchi wanapaswa kujua kuwa jukumu la kuujua umuhimu wa kulipa kodi si la TRA pekee, bali ni letu sote.

Wananchi wanatakiwa wawe na utayari wa kushirikiana na TRA katika kuwafichua au kutoa taarifa za wakwepa kodi ambao TRA inaweza kuwa haiwafahamu.

Nahitimisha waraka wangu kwa kutoa pongezi zangu kwa Rais na Serikali kwa ujumla wake.

Nimefurahishwa na maendeleo niliyoyakuta katika nchi yetu katika kipindi hiki ambacho nimekuja kupumzika.

Nimeshuhudia uboreshwaji wa miundo mbinu. Kuna ujenzi wa barabara, madaraja, ujenzi wa reli ya kisasa ya (standard gauge), uboreshaji wa afya, elimu, maji na ununuzi wa ndege, vyote hivi havikuja vyenyewe, ni kwa sababu ya kodi na jitihada za serikali katika kuhakikisha inakusanywa.

Kwangu mimi naamini haya yopte ni kielelezo cha dhamira njema ya Serikali ya sasa katika kuiondoa nchi kwenye makucha ya utegemezi na hatimae kusimama yenyewe siku moja.

Kama tukiwekeza fikra zetu kwenye kutegemea misaada, mambo haya mazuri yatachukua muda mrefu kukamilika kutokana na kusaidiwa huku unapewa mashariti magumu ambayo yangetupunguzia uhuru wa kuamua mambo yetu wenyewe.

Natamani wakati mwingine nitakaporejea nyumbani kwa mapumziko, angalau kidogo nipate nafasi ya kushirikiana na ndugu zangu wa TRA, tubadilishane uzoefu zaidi. Natamani kujifunza mengi kutoka kwa wataalamu wa mamlaka yetu. Naamini nitaacha kitu ambacho kinaweza kutusaidia zaidi.

Uingereza wao hawasemehe kodi na katika kufanikisha hilo, wanaeleza wazi kuwa kutokujua umuhimu wa kodi hakukupi nafasi ya kusamehewa kodi, kwa lugha nyepesi wanasema ‘ignorance is not a reasonable excuse’.

Prude akiwa na baba yake Paul Kimiti

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.