TUMESALITI AZIMIO, SASA UHURU NA UCHUMI UNAYOYOMA

Rai - - MBELE -

Ukiondoa dhana ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, hakuna dhana nyingine iliyotuchukulia muda na fikra nyingi katika kipindi cha miaka 52 ya Uhuru, kama dhana ya Ujamaa na Kujitegemea. Hadi leo tungali tunaimba “Ujamaa” wakati tukicheza ngoma ya kibepari

Misingi ya utekelezaji wa “Ujamaa” imefafanuliwa vyema katika Azimio la Arusha. Madhumuni ya Azimio hilo, yanashinda ukinzani wowote, kama linavyosema kwa kifupi: “Tumeonewa vya kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha na tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Ni unyonge wetu ambao umefanya tuonewe, tunyonywe na tupuuzwe. Sasa tunataka Mapinduzi kuondoa unyonge wetu, ili tusinyonywe, kuonewa au kunyanyaswa tena”. Endelea..

Mpango wa kwanza wa miaka mitano wa 1964 ulioandaliwa na mchumi wa Benki ya Dunia, ulizingatia mkakati huu; na ulianza kutelekezwa mwaka 1966 na kutujengea utegemezi, hivyo kwamba ulikuwa hautekelezeki. Misaada iliyotarajiwa kutoka nje haikupatikana, na ziada kidogo iliyokuwepo iliwekezwa kwenye vitega uchumi visivyo na faida kwa umma kwa njia ya uwekezaji usiojali.

Azimio la Arusha la mwaka 1967 lilikuwa tofauti . Mwalimu Julius Nyerere aliweka wazi kuwa, uwekezaji wa wageni ungezipa Serikali za kigeni na Mashirika binafsi, nguvu ya kudhibiti uchumi wetu na kuwageuza wananchi kuwa “watwana” ndani ya nchi yao. Alisema, Mkakati huo ungehatarisha pia uhuru wa nchi na kukiukwa kwa misingi ya usawa katika jamii, mambo ambayo Tanzania iliahidi kuyapiga vita tangu harakati za uhuru mwaka 1954, chini ya Chama cha Tanganyika African Association [TAA] na hatimaye TANU.

Mwalimu alikataa katakata, shinikizo la kambi ya “Ujamaa” wa Kisayansi, la kurekebisha uchumi kwa kuanzisha haraka Viwanda vikubwa na vya kati, na kilimo cha kisayansi cha kutumia Matrekta na mitambo ya kuvuna mazao [Combined harvesters], kwamba muda wa teknolojia hiyo ulikuwa bado kuwadia.

Akihutubia Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako fikra za kisoshalisti zilikuwa zimeota mizizi, Agosti 5, 1967, Mwalimu alifafanua maana ya kujitegemea kuwa ni Maendeleo yatakayoletwa na sisi wenyewe kwa kutumia rasilimali zetu, ambazo ni Watu, Ardhi,Siasa safi na Uongozi bora.

Alisema, ni ndoto ya mwendawazimu kudhani kwamba Tanzania ilivyokuwa wakati huo, ingeweza kuendelea kwa njia ya Viwanda vikubwa, kama ilivyokuwa kosa kufikiria kwamba mkulima mdogo angeweza kukombolewa kwa trekta, badala ya kukombolewa na jembe la Plau kabla ya Trekta.

Kuhusu biashara ya kimataifa, alisema, ni vile vitu muhimu tu kwa Watanzania, na visivyopatikana au kuzalishwa hapa nchini, ndivyo viagizwe kutoka nje kwa matumizi ya wengi na kulinda akiba ya fedha za kigeni ya ndani kwa matumizi muhimu tu.

Kwa mtizamo wa kambi ya kibepari, tafsiri ya Nyerere ya “Kujitegemea” ilikuwa kikwazo kwa maendeleo kwa kudumaza uchumi na kuufanya kuwa tegemezi. Kambi hiyo iliimba “Ujamaa” lakini ikiwa na fikra tofauti na Mwalimu juu ya utekelezaji wake. Ilikuwa ni ‘’kikulacho ki nguoni mwako’’.

Kufikia hapo, Mwalimu alikuwa anakabiliwa na ukinzani wa kambi tatu zenye kutaka kuhujumu utekelezaji wa fikra zake za “Ujamaa na kujitegemea”. Kambi ya kwanza ilikuwa ni ile ya ubepari mkongwe ikiwakilisha masalia ya Taifa la ukoloni. Kambi ya pili ilikuwa ni ile iliyoona ukombozi pekee wa Mtanzania ni kwa njia ya“Usoshalisti”; kwa kuanzia na ujenzi wa Ubepari kabla ya kufikia Ujamaa, hatua ambayo Mwalimu aliapa kutoifuata kwa hofu ya kugeuka “Jiwe”, hata kusikia tu neno “Ubepari”.

Kambi ya tatu ilikuwa ni ile ya “Ujamaa” wa Kisayansi iliyouona kuwa ndio mkombozi pekee wa mwananchi, lakini ilitofautiana na Nyerere juu ya namna ya utekelezaji wake, ikimtuhumu kwamba alikuwa anaipeleka nchi pole pole mno kuelekea kwenye Ujamaa huo akihofia “mashambulizi” ya kambi mbili za kwanza. Ilidai kuwa kwa mwendo huo wa dana dana, huenda Tanzania isingeweza kufika “Kanaani” kwa kushambuliwa na Mabedui jangwani. Hii ilikuwa ni kambi ya kina Abdulrahman Babu, Ngombale Mwiru na wengine.

Kama ilivyokuwa mwanzo, kwa mara nyingine, Nyerere alibaki njia panda bila kufungamana kikamilifu na kambi yoyote; Ujamaa wake wa njozi ukadumaa bila kupiga hatua mbele hadi kung’atuka kwake mwaka 1985. Hata hivyo, historia imethibitisha kwamba, kambi ya tatu, ya Ujamaa wa Kisayansi, ilikuwa sahihi juu ya ujenzi wa “Ujamaa” wa kweli, na kwa wakati muafaka na bila ya kuhofu kuyumbishwa na itikadi zingine. Hiyo ndiyo njia Korea Kaskazini iliyochukua kwa mafanikio.

Tatizo la Mwalimu lilikuwa moja, kwamba aina ya “Kujitegemea” aliyopendelea ndiyo hiyo hiyo iliyopendelewa na Washirika, wahasimu wetu hatari wa kibiashara: Benki ya Dunia, IMF na GATT, kiasi kwamba Rais wa Benki hiyo, Robert McNamara, alifurahishwa na “dana dana” hiyo, akaipandisha hadhi Tanzania eti kuwa mfano wa kuigwa na nchi zinazoendelea. Hiyo ilikuwa ni kuvikwa kilemba cha ukoka, wakati huo huo tukihujumiwa.

Ni Benki hiyo ya Dunia pamoja na IMF waliopiga vita Azimio la Arusha miaka 19 baadaye, na hatimaye kufanikisha kifo chake kwa njia ya Azimio la Zanzibar mwaka 1992. Ni wazi kwa mtazamo wa kambi ya Ujamaa wa Kisayansi kwamba, kama Viwanda nchini ni duni; kilimo pekee, sekta inayobeba zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania, hakiwezi kuendelea, na kinyume chake. Hali hiyo haiwezeshi kuzalisha ziada kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu, afya, elimu na uchumi.

Kama kwa upande mwingine, gawiwo kwa sekta ya huduma za kijamii litazidi uwezo wa uchumi wa nchi [kama ilivyotokea], hapawezi kuwapo ziada kuendeleza kilimo na viwanda, na nchi itaendelea kuwa mdaiwa daima. Mwalimu hakuyaona haya mapema kuweza kuyarekebisha. Woga huu ulitokana na hofu yake ya kuitwa “Mkomunisti” na kupoteza sapoti ya nchi za Magharibi alikosomea na kutamadunishwa. Matokeo ya yote haya ni kwamba, tulibinafsisha umaskini, tukaendelea kugawana umasikini; tulijua kutetea haki zetu zaidi, tukasahau wajibu na uwajibikaji, na kwa siasa kutawala uchumi, badala ya uchumi kutawala siasa. Ule utabiri wa Kwame Nkrumah kwamba “Utafuteni kwanza Ufalme wa Kisiasa, na mengine yote mtazidishiwa”, haukutimia; matokeo yalikuwa kinyume chake.

Yote haya yalitokana na mitizamo tofauti ya dunia ndani ya kambi ya Ujamaa yenyewe. Wakati Nyerere alibeba na kutetea dhana ya mzalishaji mdogo, iliyopewa nguvu na “ukale” kwa kushirikisha mazingira asilia kana kwamba dunia ilifungwa miguu; wenzake ndani ya kambi yake [kina babu] walipendelea uzalishaji mkubwa, kudhibiti na kuyabadili mazingira asilia kwenda sambamba na mahitaji ya kijamii yenye kubadilika daima. Huo ni mtizamo wa kimaendeleo, wa kuangalia mbele, badala ya kuangalia nyuma.

Nchi nyingi zinazoendelea zilizochagua njia hii, zimeweza kuendelea kwa kasi nzuri; nasi, kama tungefanya hivyo, pengine hali yetu isingekuwa mbaya kiasi hiki leo.

Miaka kadhaa baada ya kustaafu, Mwalimu aliulizwa na Wanahabari, ni kwa lipi angependa akumbukwe na Watanzania? Naye alijibu kwa kifupi: “Kwa [kuthubutu] kujaribu”.

Kuhusu Azimio la Arusha alisema, asingependa kubadili hata [alama] nukta, lakini akasema, angelitekeleza tofauti na alivyofanya katika maeneo yafuatayo: juu ya utaifishaji, angetaifisha kwa makini sana, au angeingia ubia na wenyewe badala ya kutaifisha moja kwa moja. Na kuhusu maendeleo Vijijini alisema, angeliweka kando Azimio la Iringa [Siasa ni Kilimo] lililozaa “Vijiji vya Ujamaa,” na kusisitiza kilimo cha kifamilia na watu kufanya kazi kwa pamoja.

Mwalimu alikiri kwa kusema: “Tulipoteza muda mwingi na nguvu nyingi kujaribu kuendeleza kilimo cha kijamaa; hilo ningeliangalia upya, lakini kwa madhumuni yale yale ya kujenga Ujamaa.

Pamoja na kwamba Ujamaa haukuweza kutuvusha jangwa la “Sinai” kwenda “Kaanani” ya Tanzania iliyokusudiwa, lakini ni kutokana na siasa hiyo ya Ujamaa na Kujitegemea tumeweza kujenga umoja imara wa kitaifa kwa misingi ya Uhuru, Usawa, haki, udugu, na amani, mambo ambayo nchi nyingi hazina. Tunu hii sasa inaanza kupotea kwa kuendekeza na kukumbatia ufisadi na ubepari ulio vuka mipaka.

Ni kwa hilo, kwamba Katiba yetu bado inatambua siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, licha ya kwamba tunachezeshwa ngoma ya kibepari. Tatizo ni umamluki na usaliti miongoni mwa Viongozi, na kwa ujinga wetu tumekubali kutendewa hivyo.

Mwalimu Julius Nyerere

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.