Rais Magufuli avunja mwiko

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

LICHA ya kutimiza miaka mitatu madarakani, Serikali ya Awamu ya Tano imedhihirisha uthubutu kwa kutekeleza miradi mbalimbali mikubwa ya maendeleo ambayo awali ilikwama au kusuasua kutekelezwa na Serikali za awamu zilizopita. RAI linachambua.

Hatua hiyo inatokana na ahadi zilizotolewa na Rais John Magufuli wakati anaingia madarakani Novemba 5 mwaka 2015.

Tangu alipoingia madarakani, Rais Magufuli ameonesha nia kwa kutekeleza ahadi mbalimbali zilizofanikisha pia kupaisha uchumi wa Tanzania kukua kwa wastani wa asilimia 7.1 (2017) ikilingananishwa na asilimia 7.0 mwaka uliotangulia.

Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilometa 1,219, inayotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh trilioni 7.6.

Ununuzi wa ndege tano huku nyingi mbili zikitarajiwa kuwasili mwaka huu, ujenzi wa barabara za juu ‘flyover’ pamoja na barabara kuu, ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme wa Megawati 2,100 katika Maporomoko ya Maji ya Mto Rufiji (Steigler’s Gorge) na ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria na Nyasa.

Ujenzi wa reli (SGR)

Katika ujenzi wa reli ya kisasa, Rais Magufuli ameonesha udhubutu kwa kujenga reli ya kisasa itakayotumia treni za umeme jambo ambalo lilionekana kutotekelezwa katika awamu zote zilizopita na kubakiwa na reli iliyojengwa na wakoloni zaidi ya miaka 100 iliyopita.

Maamuzi hayo ni tofauti na awamu iliyopita ambapo, Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliwahi kukiri kuwa alitarajia kuanza ujenzi wa reli hiyo lakini si ya kutumia umeme kama ambavyo ujenzi wake unaofanyika sasa.

Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli nchini (RAHCO) ndiyo inatekeleza mradi huo kutoka Dar es salaam kwenda Isaka na Mwanza.

Ujenzi huo umegawanyika katika awamu ndogo nne ikiwemo Dar es salaam hadi Morogoro, Morogoro hadi Makutupora, Makutupora hadi Tabora na Tabora hadi Mwanza.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa RAHCO, Mhandishi Masanja Kadogosa jumla ya makandarasi wanne wanaendelea na kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi wa reli hiyo yenye upana wa mita 1.345 na ambao utaruhusu treni kutembea kwa spidi ya kilomita 160 kwa saa.

Mradi huu mkubwa unatarajiwa kuchochea maendeleo katika sekta ya kilimo, biashara, madini na viwanda hususan maeneo ambapo reli hiyo itapita ikiwemo nchi jirani ya Rwanda ambayo imekubali kujenga aina hiyo ya reli toka Isaka hadi Kigali.

Ujenzi wa reli hiyo unaotarajiwa kuongeza ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam inayotegemewa na nchini mbalimbali za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ikiwamo Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ulianza kutekelezwa Mei mwaka 2017 kwa awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro urefu wa kilometa 300.

Ujenzi wa reli kwa awamu hiyo ya kwanza ambayo treni yake itaendeshwa kwa kutumia umeme unajumuisha kilomita 205 za njia kuu ya treni na kilometa 95 za kupishania treni, uzio wa reli na vivuko vya watembea kwa miguu na wanyama na unatarajiwa kukamilika Novemba mwa huu na utagharimu Sh trilioni 2.6.

Ikumbukwe kuwa ujenzi wa reli hiyo unaotekelezwa na kampuni za Yapi Merkenzi Instant Ve Sanayi A.S ya Uturuki na Mota-Engil, Engenharia E and Construcao S.A ya Ureno utaiwezesha Tanzania kuwa na treni inayokwenda kwa kasi ya kilometa 160 kwa saa na kuifanya kuwa nchi ya pili barani Afrika kuwa na treni inazokwenda kasi baada ya Morocco.

Ufufuaji wa ATCL

Serikali zote za awamu zilizopita zilishindwa kulifufua Shirika la Ndege nchini (ATCL) kutokana na sababu mbalimbali, lakini hali imekuwa tofauti katika Serikali ya Awamu ya Tano ambapo hadi sasa imekwishanunua ndege tano.

ATCL kwa sasa ina ndege sita, baada ya kununuliwa ndege tano chini ya mpango wa kufufua shirika hilo lililoanzishwa mwaka 1977.

Kuna Bombardier DASH8 Q400 tatu, mbili ambazo zilifika Tanzania Septemba 2016 na moja Aprili 3 mwaka 2018; Boeing 787 Dreamliner ilitua Tanzania Julai 8, 2018 na Airbus 220-300 ametua Desemba 23 mwaka huu.

Shirika hilo lilikuwa na Bombardier DASH8 Q300 moja ambayo ilikuwa ikihudumu tangu 2011, alipoingia madarakani Rais Magufuli amebadilisha giza nene lililokuwa limetanda ndani ya shirika hilo ambapo Disemba 23, Rais Magufuli alipokea ndege mpya ya tano aina ya Airbus 220300 ‘Dodoma Hapa Kazi Tu’, yenye uwezo wa kubeba abiria 132 na kati yao 12 wa Daraja la Biashara (Business Class) na 120 kawaida.

Julai 7 mwaka huu, ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262 ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (JNIA) ikitokea, Seattle Marekani.

Kwa mujibu wa mtandao wa HYPERLINK “http://www. boeing.com” www.boeing.com, ndege hiyo inakadiriwa kuwa na thamani ya Sh bilioni 516.3 lakini pia taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Ikulu ya Rais, ndege hiyo ilikuwa ni ya nne kuwasili nchini kati ya saba zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya kuliwezesha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuimarisha huduma zake.

Aprili 3 mwaka 2018, ndege aina ya Bombardier Dash 8 Q400, ambayo ilikuwa imezuiliwa Canada kwa amri ya mahakama na ambayo Rais Magufuli alimuandikia barua waziri mkuu wa nchi hiyo na kumtuma mwanasheria mkuu wa serikali kuifuatilia mwishoni mwa mwaka 2017, iliwasili nchini.

Septemba 28, 2016 Rais Magufuli alizindua ndege mbili mpya aina ya Bombadier Q400 NextGen na Bombadier Dash 8 Q400 zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL). Ndege hizo zina uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja.

Ndege hizo tano zimewasili tangu Serikali ilipoanza mikakati ya kulifufua shirika lake, itafuatiwa na nyingine aina Airbus 220-300 itakayowasili mapema mwezi ujao na ndege nyingine aina ya Boeing 787-800 dreamliner itakayo kuja mwishoni mwakani na kisha Bombardier Dash 8 Q400.

Itakumbukwa kuwa mwaka jana, Rais mstaafu Jakaya Kikwete pia alikiri kuwa Rais Magufuli ni jasiri kwa kuwa amedhamiria kulifufua shirika hilo.

“Rais jasiri, sisi tumeshughulika sana na ATCL tumetumia fedha nyingi za Serikali kuendesha lile shirika, ni kazi ngumu kweli inafika mahali mnakata tamaa maana mnapeleka fedha kama vile unachota maji unapeleka kwenye pipa lililotoboka.

“Sasa Rais huyu amekuwa Rais jasiri kununua ndege mpya! Kazi ngumu sasa pale ni kusimamia uendeshaji wa shirika la ndege maana shirika lile kazi kubwa ni usimamizi, nakumbuka wakati ule wa Mzee Nyerere lilifikia ndege 14 lakini zimekwenda zimepungua mpaka tukawa tena hatuna, lakini tatizo kubwa pale ni ‘management’ (usimamizi).

Umeme Mto Rufiji

Licha ya kupigwa vita na jumuiya za kimataifa, Rais Magufuli amefanikiwa kuanza ujenzi wa mradi wa bwawa la kuzalisha umeme wa maji katika bonde la Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge).

Mradi huo ambao kwa muda wa zaidi ya miaka 40, ulikwama kuanza, Serikali ilitia saini Disemba mwaka jana na kampuni ya Arab Contractors ya Misri ambayo itautekeleza na unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,100 na kugharimu Sh trilioni 6.558.

Mradi huo ulikwama kutekelezwa tangu miaka ya 1970, baada ya Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere kukumbana na vikwazo mbalimbali kutoka kwa mashirika na wadau mbalimbali wa masuala ya mazingira.

Ujenzi ‘Flyover’

Serikali ya awamu ya tano imejipambanua zaidi katika ujenzi wa miundombinu tofauti na awamu zote ambapo kwa mara ya kwanza kumekuwapo na ujenzi wa barabara za juu ‘flyover’ zaidi ya nne katika jiji la Dar es Salaam.

Hadi sasa ujenzi wa flyover Tazara uliogharimu zaidi ya Sh bilioni 95 umeshakamilika, ujenzi wa flyover Ubungo ambao unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh bilioni 188.71 unaendelea, wakati tayari uzinduzi wa ujenzi wa daraja jipya la Salender na barabara za njia nane Kimara – Kibaha ukiendelea.

Ujenzi huo wa barabara ya njia nane kati ya Kimara Dar es Salaam na Kibaha Mkoa wa Pwani yenye urefu wa kilometa 19.2, ujenzi ambao utagharimu Sh bilioni 141.56.

Pia utahusisha ujenzi wa barabara za juu ‘flyover’ katika eneo la Kibamba CCM kwenye makutano ya barabara inayokwenda Bunju na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tawi la Mloganzila.

Miradi ya maji

Katika kuendelea kuandika historia Disemba mwaka jana Rais Magufuli alizindua ujenzi wa mradi wa maji wa thamani ya zaidi ya Sh bilioni 520, unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).

Miradi mingine ni pamoja na Nansio Ukerewe uliogharimu Sh bilioni 10.9, Mbinga mkoani Ruvuma Sh bilioni 1.2, Kiluvya, Salasala, Kimara na Goba bilioni 74.46 na ule wa Bagamoyo unaotarajiwa kuhudumia wakazi wa mji wa Bagamoyo na baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa zaidi ya bilioni 133.2.

Meli, vivuko

Tofauti na awamu zilizopita, awamu ya tano pia imefanikisha kuanza ujenzi meli mbili kubwa mpya na za kisasa Ziwa Viktoria na Tanganyika ikiwamo yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo. Ujenzi ambao unatekelezwa na Kampuni kutoka Jamhuri ya Watu wa Korea.

Meli hiyo pia inatajwa kuwa kubwa zaidi katika maziwa makuu barani Afrika pamoja na kukarabati meli tano ambazo ni Mv Victoria, MV Butiama, MV Liemba, MV Umoja na MV Serengeti.

Viwanja ndege

Pia Serikali imetekeleza ujenzi na ukarabati wa viwanja mbalimbali vya ndege ukiwamo wa Uwanja wa ndege wa kisasa wa Chato mkoani Geita unaogharimu Sh bilioni 39, huku baadhi ya viwanja ukiwamo wa Musoma vikitengewa fedha za ukarabatiwa.

Kodi

Katika kuleta mapinduzi ya kikodi, serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kuongeza ukusanyaji mapato, kutoka Sh trilioni 9.9 wakati wa Serikali awamu ya nne hadi trilioni 14 kwa mwaka.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.