BASHE: Maamuzi ya Rais Magufuli yana maumivu makubwa

Rai - - MBELE - NA VICTOR MAKINDA, MOROGORO

Mbunge wa Nzega mjini, Hussein Bashe,(CCM), amesema maamuzi na sera za kiuchumi za serikali ya awamu ya tano, chini ya uongozi wa Rais John Magufuli

MBUNGE wa Nzega mjini, Hussein Bashe,(CCM), amesema maamuzi na sera za kiuchumi za serikali ya awamu ya tano, chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, yana maumivu makubwa kwa kuwa yanakinzana na matarajio ya walio ambao huchagua kula mbegu baada ya kupanda mbegu hiyo kwa faida ya kesho. Bashe aliyasema hayo wakati wa hafla ya kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Mzumbe mjini Morogoro mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Alisema kuwa uamuzi wa Rais Magufuli kuwekeza kweye miradi mikubwa, una tija kubwa kwa Taifa lakini una maumivu makubwa kwa kuwa unachagua kati ya kula mbegu au kuipanda mbegu hiyo ili izae na kuleta mavuno makubwa kesho.

“Tujiulize sasa ikiwa una mahindi kidogo je utayatumia kula au utakwenda kupanda ili yaote kwa ajili kupata mavuno? Anachokifanya rais John Pombe Magufuli ni kuhakikisha kuwa kidogo tulichonacho tunakiwekeza ili kiweze kuzalisha kwa ajili ya faida kubwa ya kesho.

“Tunafunga mkanda leo na kujinyima ili tuweze kujijengea uwezo wa kesho nzuri yenye neema. Mara zote maamuzi ya kujinyima na kuwekeza yana maumivu makubwa kwa watu waliozoea kula bila kujijengea misingi ya kesho,” alisema Bashe.

Bashe alitolea mfano kuhusu uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika kulifufua shirika la ndege la ATCL kwa kununua ndege mpya kuwa sio lazima ndege zinazonunuliwa zilete faida ya moja kwa moja, bali ndege hizo zitaleta faida katika kuinua sekta ya utalii nchini ambapo kwa kuinua sekta ya utalii nchi itapata fedha nyingi za kigeni ambazo zitatumika kuboresha hali za maisha ya watanzania.

Akizungumzia kuhusu namna ambavyo amekuwa akichangia bungeni na katika majukwa mbalimbali huku akionekana wakati fulani kwenda kinyume hata na chama chake CCM, Bashe alisema kuwa katika maisha yake hakulelewa katika misingi ya kufuata maelekezo kutoka juu bali anayo misimamo yake ambayo huwa anaisimamia ikiwa tu anaamini kuwa ni sahihi kwa maslahi mapana ya Taifa.

“Nina misimamo yangu binafsi, wakati mwingine ina waumiza wakubwa, huwa ninafanya kile ninachokiamini kuwa ni sahihi, sjakulia katika utamaduni wa kufuata maelekezo ya wakubwa’’ alisema Bashe.

AOMBA NZEGA KIJENGWE CHUO KIKUU

Aidha, Mbunge huyo aliuomba uongozi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kujenga kufungua tawi la chuo hicho Wilayani Nzega mkoani Tabora ili kuwarahisishia wanafunzi wanaotoka kanda ya Magharibi na kanda ya Ziwa kupata elimu ya juu.

“Makamu Mkuu wa chuo, pamoja na mengi mazuri ambayo chuo chako kinafanya, ninaomba Uongozi wa chuo hiki kufikiria kufungua tawi la chuo cha Mzumbe Mkoani Tabora, tena ni nitafurahi zaidi ikiwa kitajengwa wilayani Nzega jimboni kwangu. Sisi kama Halmashauri tutawapa ardhi bure ile chuo kijengwe Nzega na kuleta unafuu mkubwa kwa wanafunzi wa mkoa wa Tabora na mikoa jirani.``

Aidha, Bashe aliwataka wasomi wa Chuo hicho kuwa wabunifu, kusoma kwa bidii na wawe na majibu mujarabu kuhusu hali ya umaskini wa watanzania.

``Ninyi mliopata nafasi ya kuja hapa kusoma, someni kwa bidii lakini kubwa zaidi mkimaliza chuonielimu yenu ondokeni nendeni kwa watanzania mkiwa na majibu juu ya umaskini unalolikabili Taifa hili na mkasaidie kupata ufumbuzi wa namna gani kama Taifa litatimiza malengo yake ya kuondoa umaskini`` Alisema Bashe.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Lugano Kusiluka, akizungumza katika halfa hiyo, alisema kuwa kama chuo wanajivunia kuwa na mhitimu wa aina ya Bashe.

``Hussen Bashe ni mwana familia wa hapa. Amesoma hapa Shahada yake ya Usimamizi wa Biashara na Masoko. Ni mwanasiasa, Mbunge mwenye hoja nzito ambazo zina maslahi kwa Taifa.

“Binafsi ninaposikia Bashe akizungumza mahali iwe Bungeni au mahali popote huwa nasimama kumsikiliza nikiamini kuwa mara zote huwa anajiandaa kabla ya kuzungumza na hoja zake huwa zinaegemea kwenye utetezi wa wanyonge. Hakika Mzumbe kama Chuo, kinajivunia kuwa na product aina ya Bashe”alisema Profesa Kusiluka.

Hussein Bashe

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.