Ukitaka kufaulu kataa kufeli

Rai - - MAONI / KATUNI -

Maisha ni mtihani na ndani ya maisha kuna kufaulu na kufeli. Mambo haya mawili hayakai wala hayaendi pamoja hivyo ukilitaka mojawapo huna budi kulikataa jingine. Kufaulu katika maisha ni kufanikiwa katika malengo yako hatua kwa hatua.

Maisha ni mtihani na ndani ya maisha kuna kufaulu na kufeli. Mambo haya mawili hayakai wala hayaendi pamoja hivyo ukilitaka mojawapo huna budi kulikataa jingine. Kufaulu katika maisha ni kufanikiwa katika malengo yako hatua kwa hatua. Kuyafikia malengo yako kunahitaji dhamira na ustahamilivu mkubwa. Na kuyalinda mafanikio kunahitaji fikra na matendo kuchukuzana na wakati.

Ndani ya maisha huibuka vitimbi usivyovitarajia, pambana navyo. Wapo sahihi waliyosema kujikwaa si kuanguka, na ikitokea umeanguka kitafute kilichokuangusha badala ya kuwatafuta waliyosababisha uanguke. Patazame unapokanyaga ili uepuke utelezi na weka akiba ya maneno ili uepuke kuteleza ulimi. Wenye hekima husema kuwa katika maisha ni afadhali ajali ya kuteleza mguu kuliko kiburi cha kuteleza ulimi.

Kuibadili hali ya maisha yako kutoka kwenye dhiki na karaha kwenda kwenye faraja na furaha kunahitaji kuibadili hulka yako katika mwenendo wako. Haiwezekani hata kidogo ikawa kila uchao unawaza na kufikiri namna ileile na ati ukataraji mabadiliko kitabia, kimatendo na katika mwenendo wako. Kwa mwenendo huo bila ya shaka utabakia kuwa yule yule na utaendelea kuwa vile vile.

Dhamira ya kubadilika kifikra juu ya maisha yako ndiyo siri ya kukataa kufeli. Inawezekana pengine ulifanya kosa fulani ambalo limekufikisha hapo. Usivurugwe na kosa hilo kwani wazee husema kutenda kosa si kosa ila kurejea kosa. Ukigundua umepotea njia chukua iliyo sahihi kabla hujafika mbali. Mwenye kufahamu aendako hapotei hata kama atachelewa kufika.

Kufaulu katika maisha kunahitaji kuogelea ndani ya malengo yako na mtiririko wake. Huna budi kuzielekeza fikra zako na mwenendo wako katika mambo yanayozunguka na kuchapua malengo yako, kwa namna iliyo bora katika kuyafikia malengo hayo. Ni lazima utabiri vitimbi vilvyopo katika safari yako ili kujiweka tayari katika kuzikabili ghafla na dharula mbele ya safari. Maisha ni mapambano.

Hapana chembe ya ubishi kuwa mara nyingi mwanadamu hufeli katika maisha kwa sababu ya ufahamu mdogo anaokuwa nao juu ya malengo yake. Mwanadamu anao udhaifu mkubwa wa kufanya uamuzi kwa kukurupuka kutokana na uchu wa utashi wake, matamanio yake na njozi zenye kuajabisha. Ni aina ya wazimu usiyo na kinga wala tiba. Haya ndiyo yale ya tamaa mbele mauti nyuma.

Nakumbuka yaliyomfika rafiki yangu wa karibu, msomi wa kwelikweli na ambaye alikuwa na wadhifa mkubwa kazini kwake. Alinifuata kuniomba ushauri juu ya nia yake ya kugombea ubunge. Nilimuuliza alichokuwa anakitaraji ndani ya ubunge ambacho kinakosekana ndani ya wadhifa wake kazini kwake. Jibu alilonipa halikuwa la kumumunya maneno. Kwa elimu yake atakuwa Waziri bila ya shaka. Unaonaee!

Mungu alimtangulia akafanikiwa kuwa mheshimiwa Mbunge, lakini hakujaaliwa alichokitamani. Hakuteuliwa uwaziri wala unaibu waziri na kama wasemavyo waswahili kuwa baada ya kisa mkasa, kura zake hazikutosha katika uchaguzi uliyofuata. Hapana shaka kuwa kuongozwa kwa utashi, matamanio na njozi kukipindukia mipaka hutukwaza wengi katika namna na mazingira tofauti bali maisha lazima yaendelee.

Baadhi yetu wamekwama kimaisha kutokana na makosa ya wasaidìzi wao. Wengine wametolewa kafara kutokana na nia zao njema katika kufanya maamuzi ya kutengeneza jambo. Na wapo waliyoteleza kijinai au kimaadili na kuwafika yaliyowafika. Hawa wote wanatakiwa kuleta fikra mpya ili maisha yaendelee. Dunia imesheheni fursa na mwenye malengo yake ni suala la wakati tu.

Kukataa kufeli katika maisha ni kufanya uamuzi sasa wa kubadilisha mtazamo wako wa maisha na wa kuishi. Je! Mfanyakazi wa kiwango cha mshahara wako ni sahihi kujirusha kwa kiasi hicho? Wewe mjasiriamali na mtaji wako wa kuungaunga kwa mtindo huo wa maisha utayafikia malengo yako? Wewe msanii na mwanamichezo unafahamu kuwa dunia haisimami na wakati hausubiri?

Kanuni ya kufaulu katika maisha ni kujitambua na kujituma. Elimu, maarifa, ujuzi, wadhifa ni vipaji na zana tu za kutafutia maisha. Maisha yenye mafanikio yatajengwa na wewe. Wapo waliyomaliza vifungo magerezani na sasa ni mafundi waliyoajiri wasaidìzi. Wapo waliyoshindwa shule na vyuo kwa sababu mbalimbali na sasa wameajiri wasomi wenye vyeti, astashahada na shahada. Maisha ni malengo.

Tumedurusu kwa kina mifano ya dhiki tunazokutana nazo katika maisha. Tumejaribu pia kujadili mifano ya zinavyochimbuka dhiki zetu. Na tumejaribu kukumbushana juu ya mambo ya kufanya ili kuepuka kufeli na ili kupata kufuzu. Swali tunalojiuliza wengi ni iwapo hawa waliyofanikiwa ni matokeo ya kujituma, wizi, dhuluma au nguvu za giza?

Swali hili lina majibu mengi. Ni kweli wapo waliyotajirika kwa nguvu za ufisadi, na dhuluma ya mali za watu na hata kuzing’oa roho za wenzao. Lakini vigezo tunavyovihitaji hapa ni waja waliyobadili fikra zao na mienendo yao kwa shabaha ya kuyafikia malengo yao. Tunazungumzia watu wanaomudu maisha, wanaothamini wenzao na wanaomtanguliza Mungu mbele. Ni watu wenye amani na furaha ndani ya nafsi zao.

Kufanikiwa kimaisha ni kujitambua kuwa thamani ya utu wako haipimwi kwa vigezo vya kujikweza na kiburi kwa sababu ya kipato chako. Watu watayapima mafanikio yako kwa mwenendo wako wa kiungwana na matendo yako yenye ubinadamu. Kufanikiwa kwako kimaisha kutapimwa pia kwa kigezo cha uvumilivu wako wa dhiki katika kuitafuta faraja. Mtihani hukweza na kushusha mtu.

Istahamili dhiki katika kutafuta mafanikio. Wanasema wahenga kuwa mchumia juani hulia kivulini. Mafanikio yanahitaji kuichosha akili na kuumiza mwili. Kwani hujapata kusikia watu wakisema kuwa bila mavune hakuna mavuno! Unataka kuilalia bahati ya mwenzako mlango wazi! Unaitamani bahati ya mtende kustawi jangwani! Ukitamani uangukiwe na dodo chini ya msonobari utakesha.

Kalamu ya muungwana inakushauri kuwa unalolitaka ndiyo tatizo liache. Au ikiwa tatizo ni namna ya kulipata ulitakalo basi badilisha mbinu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.