Mugabe akolea kwenye penzi la Sally kabla ya Grace- 6

Rai - - AFRIKA - NA MPOKI BUYAH

WIKI iliyopita tuliangazia namna Mwana mama Grace Ntombizodwa Mugabe alivyo na asili ya ukali lakini pia asiye na unafiki mbele za watu.

Aidha, licha ya ushupavu wake pia tulidadavua namna anavyoipenda familia yake jambo lililodhihirishwa na kisa alichokifanya Septemba 11 mwaka 2017, baada ya kumshushia kipigo mwanamitindo Gabriella Engels katika hotel moja maarufu kama Sandton inayopo Johannesburgy. Endelea…

Gabriella Engel hapo awali hakujua kama aliyempiga alikuwa ni First Lady wa Zimbabwe lakini hata alipoona haki imekuwa ngumu kutendeka alisikika akisema “Mimi namuachia Mungu”.

Mwanamitindo huyo alikuwa ameumizwa vibaya katika paji la uso wake na kuvuja damu nyingi. Vyombo vya Usalama vilianza kumsaka Grace kwa lengo la kumkamata na kumtia hatiani, makundi ya haki za binadamu yalipaza sauti juu ya kile kilichofanywa na Grace Mugabe kwamba hakikuwa cha kiungwana lakini hata hivyo baadae Grace Ntombizodwa Mugabe hakuonekana popote lakini taarifa zilikuja kutoka kwamba Mwana mama huyo alikwisharejea Zimbabwe salama salimini yeye na familia yake.

Taarifa kutoka Usalama wa Taifa- Afrika Kusini ni kwamba mwana mama GraceNtombizodwa Mugabe alipewa kinga ya kiusalama na ndio maana hakukamatwa na yote hayo ni kutokana na heshima kubwa aliyonayo Mugabe. Baada ya muda kidogo, Grace alijitetea kwamba mwanamitindo Gabriella Engles alikuwa hana adabu kwani aliingilia party ya watoto wake wawili yaani Chitunga Mugabe na Robart Peter Mugabe Jr. ndiyo hata alivyomuhoji mwanamitindo huyo alimjibu vibaya na kumshushia kipigo mpaka kupelekea kumjeruhi vibaya usoni.

Vijana wengi nchini Zimbabwe na ndani ya chama cha ZANUPF walimpenda sana kulingana na ujasiri na ushawishi mkubwa aliokuwa nao na hawa vijana ni lile kundi lililojulikana kama G40 yaani kizazi kipya (New Generation). Vijana hawa walimpenda mwana mama kwani alikuwa anamwaga pesa na kuwatengenezea nafasi mbalimbali katika Serikali ya Robert Gabriel Mugabe.

Grace Mugabe aliandaa vita ndani ya chama na kuanzisha Operation fukuza wazee na kuweka damu changa Serikali. Kundi hili lilikuwa linaongozwa na mwana mama Grace na kupelekea kuibuka kwa mtafaruku mkubwa ndani ya Chama cha ZANUPF na mpaka mwisho wa siku kupelekea kufukuzwa ndani ya chama yeye, mume wake Roberty Mugabe na vijana wengine wengi kutimuliwa kwa kile kilichoitwa kwamba vijana hao na mama yao ni wavurugaji wakubwa wa amani nchini humo hivyo ilikuwa ni lazima wafukuzwe ndani ya chama haraka ili kuepuka ukosefu na uvunjifu wa amani nchini Zumbabwe.

Mwaka 2014 Grace alilizua lingine alipotangazwa kuhitimu shahada ya uzamivu PhD (Socialogy) kwa muda miezi miwili tu pekee katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe (University of Zimbabwe). Hata hivyo ilileta tafrani katika Taifa la Zimbabwe kwamba kutakuwa na rushwa imetembea lakini kwa wakati huo Mugabe alipokuwa madarakani hakuna kilichofanyika, sakata hilo likapotea kimya kimya. Baada hapo alivamia na kujiingiza kwenye siasa, akawa mkuu wa jumuiya ya wanawake chama cha ZANU-PF kisha kuingizwa jopo kuu la uamuzi kwenye chama (Politburo). Septemba 12, 2014, Grace alimponda hadharani, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Joice Mujuru kuwa anahujumu Serikali kisha Mugabe akamfukuza kazi Makamu wake na baada Mujuru aliteuliwa Emmerson Mnangagwa ambaye Agosti mwaka 2017, alilalamika kutaka kuuawa kwa sumu na Grace .

Hata baada ya Mnangagwa kuteuliwa na Mugabe bado Grace alimtuhumu Mnangagwa kwamba ni mchawi anamroga Mugabe na akaenda mbali zaidi kwamba ni bora yeye angekuwa Makamu wa Rais na siyo Mnangagwa kauli hiyo ilikuwa nzito maana ilipekea Mugabe kumfukuza kazi Mnangagwa tarehe 6/11/2017 kitendo ambacho kilileta machafuko makubwa nchini humo na kupelekea kuanzisha kwa Operation Sari iliyopelekea Mugabe kuachia nafasi hiyo kwa shingo upande huku akidai kwamba amefanyiwa uhuni na vijana aliowalea mwenyewe ikiwa ni baada ya kukaa madarakani kwa miaka 37.

Baada ya Mugabe kung’olewa madarakani Novemba 21, 2017 na serikali mpya kuingia madarakani, mambo mengi yalibadilika mpaka kwenye mambo ya utawala na mkuu wa Chuo Kikuu cha Zimbabwe aliyefahamika kama Levi Nyagura ambaye alimpa Grace PhD ambayo haikukidi vigezo alikamatwa Januari 22 mwaka jana na kuwekwa ndani.

Kulingana na maadui ambao Mugabe alikuwa nao nje na ndani ya nchi, kuanzia mwaka 20022007 na kuendelea, ameonekana mbaya kwa sababu ya uzalendo uliopitiliza, kila jambo ambalo lilifanywa na familia yake ama yeye mwenyewe lilipewa uzito wa pekee na kusambaa katika vyombo habari kwa kasi ya ajabu na kila mtu alikuwa mwepesi na kutoa mawazo ama shutuma nzito kwa Rais huyo lakini yote haya ni kutoka na jina kubwa na mambo mengi ambayo Mugabe aliyafanya akiwa madarakani ikiwemo kufukuza wazungu na kuongoza nchi kwa mkono wa chuma.

Wataalamu na wachambuzi mbalimbali wanafafanua kwamba Mugabe wa miaka ya 80s kipindi yupo na Sally Hyfon ni tofauti na Mugabe wa miaka ya 1990s pindi tayari amefunga ndoa na Grace Ntombizodwa.

Binadamu wamekuwa wepesi wa kuzungumza mengi juu ya Mugabe na familia yake pengine ni kwa sababu ya uongozi wake ambao ulijaa mambo mengi lakini pia ikumbukwe kwamba walikuwepo watendaji wake wa chini ambao pia walimuangusha mzee katika utendaji mpaka nchi kufikia hapo ilipo kwa sasa ila mbali na yote hayo Mugabe atabaki kuwa mkombozi na Afrika itampa heshima yake katika uzito ule ule.

Rais Mugabe na mkewe Grace Mugabe

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.