Wateule wa Rais wavurugana

Mihimili ya dola nayo moto

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

LICHA ya Rais John Magufuli kufanya mabadiliko ya nafasi mbalimbali za wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala na wakurugenzi wa halmashauri na miji, baadhi ya wateule hao wameendelea kuvurugana na kusababisha malalamiko lukuki kwa mamlaka iliyowateua. RAI linachambua

Katika siku za karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la kuripotiwa kwa matukio ya wateule hao wa Rais, kutoelewana kati yao huku baadhi yao wakitoa adhabu kwa viongozi wenzao hadharani.

Hatua hiyo inayoonekana kumea siku hadi siku imeonekana pia katika mihimili ya dola kati ya Bunge na Serikali ambapo mapema wiki hii Spika wa Bunge Job Ndugai aliagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Musa Assad kufika mbele ya kamati ya maadili ya Bunge kujieleza kuhusu kauli aliyoitoa wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Uamuzi huo wa Ndugai pia umetasfiriwa kuleta migongano kati ya mihimili hiyo kwa mujibu wa Katiba na sheria.

Aidha, katika siku za karibuni, wakuu wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro wamekumbwa na zahama hiyo ya kutoelewana kati na wasaidizi wao hali iliyomlazimu Makamu wa Rais, Samia Suluhu kukemea hali hiyo huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa naye akikemea na kutoa maagizo.

Disemba 3, mwaka jana Waziri Mkuu aliwaagiza mawaziri wawili Ofisi ya Rais kwenda mkoani Kilimanjaro kuimarisha uhusiano kati ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira na wakuu wa wilaya za mkoa huo.

Mawaziri waliopewa maagizo hayo wakati Majaliwa akifungua mafunzo ya wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa ya Tanzania ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika.

Majaliwa alisema wakati mwingine kauli na hatua ambazo si muhimu zinaweza kuifanya Serikali kuonekana si sekta muhimu.

“Mheshimiwa waziri ameeleza hapa juu ya matumizi ya adhabu ya kuweka watu ndani. Tumeona mabishano haya kati ya kiongozi wa mkoa na wakuu wa wilaya wanapochukua hatua lakini bado kuna shida. Nataka niagize waziri wa Tamisemi kwenda mkoani Kilimanjaro. Kuna shida ya mahusiano kati ya mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya tena wengi sio mmoja,” alisema

Alikwenda mbali na kumuagiza Mkuchika kwenda kuendesha semina ya wakuu wa wilaya juu ya itifaki na kuheshimu mamlaka ya watu wengine ili kuwezesha kazi zifanyike vizuri.

Aidha, Mawaziri Jaffo na Mkuchika walitekeleza agizo hilo ambapo walikwenda mkoani Kilimanjaro na kujifungia katika kikao cha faragha kwenye ukumbi wa mkuu wa mkoa mjini Moshi kwa saa 10 kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12.05 jioni.

Viongozi waliokutana na mawaziri hao ni mkuu wa mkoa, katibu tawala wa mkoa, wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na manispaa.

Hata hivyo, baada ya kikao hicho Jaffo aliwaambiwa waandishi wa habari kuwa “Tumefanya kazi maalumu ya kimahusiano. Sitaki kusema kazi hiyo tumeifanya vipi, lakini imani yangu ni kwamba baada ya kikao chetu kirefu kila kitu kitaenda vizuri.

“Tumekuja kwa ajili ya mahusiano maana haya ni maelekezo kwamba Mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa haufanyi vizuri, kwani tulipokuja hapa na Makamu wa Rais alizungumza wazi Kilimanjaro una shida”.

Hata hivyo itakumbukwa pia kuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akiwa wilayani Rombo naye alikemea uwepo wa uhusiano mbaya wa watendaji wa Serikali.

Ingawa Samia hakueleza wazi, lakini taarifa zinaeleza upo uhusiano usioridhisha kati ya mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya; wakuu wa wilaya na makatibu tawala na wakuu wa wilaya na wakurugenzi.

Pia Februari 24, mwaka jana Mama Samia aliwaonya viongozi na watendaji wa Mkoa wa Simiyu kuacha kufanyiana fitina na majungu na zaidi kushtaki mambo madogo madogo kwa Rais Dk. John Magufuli, pindi wanapotofautiana katika utendaji wa kazi zao.

Samia ambaye alikuwa akizungumza katika kikao cha majumuisho kilichofanyika katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki mjini Bariadi mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku tano mkoani humo, alisema mwenendo huo unakwamisha shughuli za maendeleo.

Samia alishangaa baadhi ya watendaji kutuma ujumbe kwa Rais kushtaki mambo madogo madogo ambayo kimsingi alisema yanaweza kumalizwa ndani ya mkoa huo chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka.

Akitolea mfano wa baadhi ya mambo hayo, alisema ni pamoja na maelewano mabaya kati ya Mkuu wa Wilaya ya Busega na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo.

Samia alishangaa masuala hayo ambayo yanaweza kutatuliwa na Mkuu wa Mkoa yanapelekwa kwa viongozi wa juu jambo ambalo alisema linafanya utendaji wa kazi kuwa mgumu.

“Utakuta viongozi ndani ya eneo moja la utawala kama vile Mkuu wa Wilaya ya Busega na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo wanatofautiana, lakini hata suala halijapelekwa kwa mkuu wa mkoa tayari jambo hilo linapelekwa kwa Rais.

“Rais ana mambo mengi sana ya kitaifa ambayo anapaswa kuyashughulikia, hivyo haya mengine ya tofauti kati ya DC na DED au ya mbunge kutotumia mashine ya EFD katika vituo vyake vya mafuta, yamo ndani ya uwezo wa mkoa na si kumsumbua Rais, ni vizuri mkafuata utaratibu wa ngazi kwa ngazi na si kurukia ngazi ya juu zaidi,” alisema.

Matukio

Kilimanjaro ndio mkoa ambao umetia fora katika mvurugano huo kati ya wateule hao wa Rais jambo ambalo pia limetafsiriwa kuwa limetokana na Mghwira kuteuliwa kutokea upinzani kushika wadhifa huo.

Licha ya Mghwira kuhamia CCM, hali bado iliendelea kuwa mbaya jambo lililolazimu kufanyika kikao cha suluhu kilichowahusisha wakuu wa wilaya za Moshi, Hai, Same, Rombo, Mwanga na Siha za mkoa Kilimanjaro.

Aidha, mawaziri wawili kuwaweka kikaangoni wateule hao wa rais, bado hali imeendelea kuwa tete baada ya Januari 7 mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Aron Mbogho kuamuru kuwekwa mahabusu kwa saa 24, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo (DED), Zefrin Lubuva akimtuhumu kufanya makosa mbalimbali.

Mbali na Lubuva, adhabu hiyo ilimkumba pia kaimu mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mwanga, Justine Valentino.

“Ni kweli huyo mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga na kaimu mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Mwanga wako mahabusu hivi tunavyoongea,” alisema Mbogho.

Mkuu huyo wa wilaya alishawahi kuwaweka mahabusu viongozi wengine pia akiwamo Katibu Tawala wa Wilaya ya Mwanga (DAS), Yusuph Kasuka Agosti mwaka jana.

Mwingine ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mwanga, Jaffary Kandege ambaye alimwekwa mahabusu Mei, mwaka jana.

Mbogho alimtuhumu Kandege kufanya uchochezi na kusababisha maofisa wa Serikali waliokuwa wakipambana na uvuvi haramu kushambuliwa na wananchi.

ARUSHA

Tukio lingine lililovuta hisia za wachambuzi wa masuala ya utawala ni la hivi karibuni ambapo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Gabriel Daqaro, walitofautiana juu ya ubora wa mabati ambayo yametumika kuezekwa kituo kipya cha afya Murieti katika Jiji la Arusha.

Kutofautiana kwa viongozi hao kulibainika baada ya kuvuja, kipande cha video ya kikao cha viongozi hao na watendaji wa Jiji la Arusha ambacho kilifanyika Desemba 2018 siku chache baada ya ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais –Tamisemi, Josephat Kandege katika kituo hicho.

Katika video hiyo, mkuu huyo wa mkoa alidai kuwa mkuu wa wilaya, Daqaro aliyekuwa amekaa pembeni yake alitoa taarifa za kutilia shaka ubora wa mabati hayo na kueleza ameagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuchunguza.

Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya alipinga taarifa ya RC Gambo, kumtaja yeye kutoa taarifa na kueleza uamuzi wa kuchunguza mabati hayo ulitolewa na Naibu Waziri Kandege.

Kipande hicho cha video pia kinamwonyesha DC Daqaro akimweleza RC Gambo kueleza ukweli huku akitumia mikono kufafanua jambo lililomfanya mkuu huyo wa mkoa kunyamaza.

Wakati Gambo alipokuwa amesimama, Daqaro alizungumza akiwa amekaa na baadaye anaonekana mtu mmoja ambaye anakwenda hadi alipokuwa amekaa mkuu huyo wa wilaya na kuonekana kama akimtaka atulie.

Aidha, mvutano wa aina hiyo unadaiwa pia kutokea mwaka 2016 ambapo Mkuu wa mkoa alimtimua kwenye kikao aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Arumeru ambaye kwa sasa ni mkuu wa Mkoa Manyara Alexander Mnyeti.

SIMIYU

Katika mkoa wa Simiyu nako kulielezwa kutokea maelewano mabaya kati ya Mkuu wa Wilaya ya Busega na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo.

Makamu wa Rais Samia Suluhu alieleza hayo alipofanya ziara mkoani huko na kukemea tabia ya viongozi hao kushtakiana kwa Rais Magufuli.

Shinyanga

Mvurugano huo pia ulishuhudiwa katika wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga hali iliyomlazimu Rais Magufuli ‘kumtumbua’ Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga Fadhili Nkurlu. Julai15, 2018 Rais Magufuli alimteua Anamringi Macha kuchukua nafasi ya Nkurlu.

Nkurlu alitimuliwa kazi akiwa katika msafara wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wilayani hapo. Saa chache kabla ya taarifa hiyo ya Ikulu, Majaliwa alikemea kuhusu migogoro ya kiuongozi wilayani hapo akisema watumishi wa umma wanapaswa kubadilika mara moja.

Alisema, “Migogoro niliyoisikia ambayo iko hapa ni kwa sababu ninyi mmeingia kwenye biashara na kutake sides (kuwa na upande). Hapa Kahama, mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa wilaya hamuelewani, mkurugenzi na wakuu wa idara hamuelewani, wakuu wa idara na wasaidizi wao nao pia hawaelewani.”

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu iliongeza: “Hali ya uhusiano hapa Kahama ni mbaya kuliko Kishapu na Shinyanga. Mnachapa kazi vizuri lakini tatizo kubwa kila mmoja anaenda kivyake, hakuna anayemsikiliza mkurugenzi wa halmashauri wala mkuu wake wa idara.

“Serikali haitavumilia kuona watumishi wakifanya mambo ya ovyo. Kahama ni wilaya yenye majaribu na Shinyanga nayo ni wilaya yenye majaribu makubwa. Kwa hiyo watumishi inabidi muwe makini, kuweni waangalifu msije mkaingia kichwakichwa kwenye majaribu haya.” Alisema.

Wasomi: Hakuna semina elekezi, nidhamu

Aidha, baadhi ya ya wasomi na wachambuzi wa masuala ya utawala bora waliozungumza na RAI walibainisha kuwa kutokuwapo kwa semina elekezi kwa viongozi hao pamoja na nidhamu ni moja ya sababu ya kuendelea kushamiri kwa mvurugano huo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo (CEGODETA), Thoma Ngawaiya alisema kiujumla kasi ya Rais Magufuli katika maendeleo ni kubwa zaidi kuliko ya watendaji wake.

‘Nilishawahi kushauri kuwa kuwe na semina elekezi ili waweze kutambua mwenendo anaoutaka Rais Magufuli. Kama wakiitwa viongozi wote wakapewa semina elekezi na kuambiwa taifa linatakiwa liendeje, wote watakuwa na mwendo mmoja, ila sasa kuna baadhi ya wanazubaazubaa na ndio sababu.

“Wakuu wa mikoa wanapata maelekezo kutoka kwa Rais, wanataka yaende chini kwa wakuu wa wilaya, hapo ndipo kunapotokea mgongano labda wanashindwa kuelewa, na kusababisha hata baadhi ya watu kufukuzwa hadharani.

“Sio kwamba hawa wateule si watendaji wazuri hapana, ila tatizo ni suala la kufahamisha kuwa tunaenda kwa njia hii. Hivyo kutolewe elimu pia kuwe na mwongozo wa semina elekezi wa hapa kazi tu, kuwa nini kifanyike kulingana na kasi ya utendaji wa Rais Magufuli,” alisema.

Hoja hiyo pia iliungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu ambaye alisema tatizo kubwa ni nidhamu.

“Nidhamu inaweza kufundishwa pia kunakuwapo na taratibu na kanuni za kufanya jambo. Inaelekea hayo yote mawili hawakupewa ili kujua nidhamu ya kazini, na ya kutumia madaraka. Kiujumla nidhamu haipo.

“Sasa wanaweza kufundishwa, au kufuata taratibu sheria, misingi ya katiba kwa sababu kuna mambo yametokea kwa mfano kwa Makonda mambo mengi amefanya yanaonekana yanapita tu, ila hakuna namna ya kuyakemea haya mambo, badala yake nakumbuka Rais alimwambia Makonda chapa kazi.

“Kwa hiyo labda hawajapata maandalizi mazuri, kwamba wapewe semina kujua mambo ya msingi ya kuendesha serikali na kujua sheria zilizopo,” alisema.

“Kuongoza ni mfano, kwa hiyo Rais anatakiwa kuwa mfano kwani ndio mwajiri wao, sasa hii kutumbuana na mambo mengine, wateule hao wanajaribu kutenda mambo tofauti na wenzao mwisho wa siku wanakwenda kinyume na taratibu labda tu kwa kutafuta umaarufu na mambo mengine,” alisema.

Aidha, itakumbukwa kuwa Katibu mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally aliwahi kutaja mikoa ambayo hakuna mahusiano mazuri ya kiutendaji kati ya viongozi wa chama na Serikali. Aliitaja mikoa hiyo kuwa Mara, Arusha, Dar es salaam na Mbeya.

Hali hiyo pia ilielezwa kusababisha Ofisi ya Rais-Ikulu kupokea malalamiko na barua nyingi kutoka kwa watumishi wa umma na wananchi yanayoshughulikiwa na Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kitendo ambacho ni utovu wa nidhamu na ukiukwaji wa sheria.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi alisema: “Masuala mengi yanayofika Ikulu yalipaswa kushughulikiwa na ngazi za wilaya na mkoa, lakini yanavuka hadi ngazi za taifa ikiwa chanzo ni watumishi kutotimiza wajibu ipasavyo huku baadhi yao hutumia akili binafsi na ubinafsi. Kiutumishi hili jambo halifai”.

Rais John Magufuli

Mrisho Gambo

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.