UBABE

wa Ndugai dhidi ya CAG kwa faida ya nani?

Rai - - MBELE -

Mwanzoni mwa wiki hii, Spika wa Bunge Job Ndugai, amemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kufika mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge Januari 21, mwaka huu kwa hiari kuhojiwa, la sivyo atapelekwa akiwa amefungwa pingu.

Mwingine anayetakiwa kufika katika kamati hiyo ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema). Ametakiwa kufika mbele ya kamati hiyo Januari 22, mwaka huu.

Kauli hiyo ya Spika katika mkutano na waandishi wa habari, inakuja siku chache baada ya CAG kusema ofisi yake inajitahidi kutoa ripoti za ukaguzi kila mwaka, lakini matokeo yake hayaonekani kwa wananchi.

Prof. Assad aliyasema hayo katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, New York Marekani wiki iliyopita.

Katika video iliyosambaa kwenye mitandao wa kijamii, Profesa Assad anasikika akisema: “Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu, halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge.

“Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapo onekana kuna matatizo, basi hatua zinachukuliwa. Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti.

“Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo tunaamini muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa tunahishi kwamba Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.

Sitaki kuwa labda nasema hili kwa sababu linahusisha watu fulani, lakini ninachotaka kusema ni kuwa Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata huu udhaifu unaoonekana utapungua” anasema Profesa Assad.

Kauli hii ya CAG inaungwa mkono na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ambaye katika mahojiano na vyombo vya habari, amekiri kiri kuwa Bunge ni dhaifu.

“Tumeshuhudia Bunge dhaifu, mimi ni Mbunge nasema sisi ni wadhaifu. Siwezi kukwepa lawama kwa kusema mimi nikiwa kule nakomaa, hakuna mtu wa kukomaa, hii ni ‘collective responsibility, (uwajibikaji wa pamoja), mimi ni Mbunge, Bunge ni dhaifu.

Mbaya zaidi nimekuwa Mbunge vipindi vitatu nikiwa viti maalumu, na jimbo ‘I can see the difference’—naweza kuona tofauti” anasema Mbunge huyo.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Spika Ndugai anazitafsiri kauli hizi kama udhalilishaji wa Bunge na kudai kuwa kama ni upotoshaji, CAG na ofisi yake ndiyo wapotoshaji.

“Huwezi kuisema nchi yako vibaya unapokuwa nje ya nchi, na kwa hili hatuwezi kufanya kazi kwa kuaminiana,” anasema Spika Ndugai.

Ni katika kipindi hiki hiki pia Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, kupitia waraka aliouandika pamoja na mambo mengine, alilalamika kuhusu Bunge kususia gharama za matibabu yake pamoja na fedha za kujikimu.

Mbunge huyo wa Singinda Mashariki (Chadema), anayeendelea na matibabu nchini Ubeligiji baada ya kushambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017, anadai kuwa licha ya Spika Ndugai kutamka kwamba angefika kumjulia hali duniani, bado hajafanya hivyo.

“Hadi ninapoandika maneno haya, bado Spika Ndugai hajatimiza ahadi yake hiyo. Na hadi sasa, hakuna mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge, au afisa yeyote wa Bunge, aliyefika hospitalini kuniona na kunijulia hali,” ilisomeka sehemu ya waraka wa Mbunge huyo.

Pamoja na kauli hiyo ya Spika kwa CAG, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 143 ibara ndogo ya 6, inaeleza kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali.

“Lakini maelezo hayo ya ibara hii ndogo hayatazuia Mahakama nayo kutumia madaraka yake kwa ajili ya kuchunguza kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ametekeleza majukumu yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au sivyo,” inasomeka shemu hiyo ya Katiba. Kauli ya Spika yakosolewa Kama alivyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari, Spika Ndugai kukasirishwa na kitendo hicho na kwamba hakutegemea msomi aina ya Profesa Assad, angeweza kutoa maneno ya kudhalilisha Bunge lililojaa wasomi zaidi ya mabunge yote tangu uhuru.

Wito huo wa Spika kwa CAG umekosolewa na wadau mbalimbali, akiwamo aliyekuwa Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Alberto Msando; Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa instagram, Msando ambaye kwa sasa ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alinadika:

“Twende taratibu Spika. Taratibu

Tumeshuhudia Bunge dhaifu, mimi ni Mbunge nasema sisi ni wadhaifu. Siwezi kukwepa lawama kwa kusema mimi nikiwa kule nakomaa, hakuna mtu wa kukomaa, hii ni ‘collective responsibility, (uwajibikaji wa pamoja), mimi ni Mbunge, Bunge ni dhaifu.

kabisa. Umesema unapeleka suala hilo kwenye kamati ya maadili, ili wakushauri na walishauri Bunge, lakini hapo hapo unasema CAG aende mbele ya kamati akajieleze, asipoenda mnaweza kumtia pingu.

Moja, kamati imeshakushauri wewe na Bunge kwamba CAG aitwe ajieleze? Pili anayepaswa kufikia uamuzi na kutoa wito wa kumuita CAG ni wewe au kamati? Unamwita CAG kwa press conference na kumtishia kwa pingu, marehemu babu yangu aliwahi kunionya kwamba kufanya jambo kwa haraka, ni kiashiria cha udhaifu,” Alisema.

“Alichosema CAG ni kwamba kazi ya ofisi yake ikishakamilika, analikabidhi Bunge lichukue hatua. Anadhani Bunge halichukui hatua kwa sababu ni dhaifu, unamjibu kwamba siyo dhaifu kwa kumtishia pingu!

Hiyo siyo kazi ya Bunge, wala njia ya kuonyesha Bunge siyo dhaifu. Kwa hili ni lazima uangalie upya kuhusu mamlaka ya Bunge, taratibu za kumhoji CAG kikatiba, na njia bora za kiuongozi” analiandika Msando.

Katika kufafanua jambo hilo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kupitia taarifa yake iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Anna Henga, ilieleza kuwa CAG anawajibika kwa Rais siyo Bunge na Bunge hupewa taarifa ambayo imetoka kwa Rais.

Pia halazimiki kufuata maagizo ya mtu yeyote na kwamba Mahakama ina uwezo wa kuchunguza kama ametekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ama sivyo.

Taarifa hiyo inafafanua zaidi kuwa CAG ataondoka kazini kwa kustaafu, kuugua au kwa tabia mbaya au kwa kuvunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kwamba kuondolewa kazini kwa CAG ni mchakato unaoanza kwa Rais kuteua tume maalumu ambayo itakuwa na mwenyekiti na wajumbe wasiopungua wawili.

Suala la msingi la kujiuliza ni je, Spika halitambui hili? Na ikiwa analitambua, je, amefanya makusudi? Nadhani busara ilipaswa kutumika zaidi kuliko hatua ya haraka iliyochukuliwa na kiongozi huyo mkuu wa Bunge.

Ikiwa hata Mdee ambaye pia ni Mbunge wa katika Bunge hilo hilo, anakiri kuwa wao (Wabunge) ni dhaifu, kuna haja ya kujitafakari kwa nini watu wadai Bunge ni dhaifu kuliko kuchukua hatua za haraka zinazoweza kuzua mvutano usiyo wa lazima kati ya CAG na Spika.

Kwa kawaida, mtu hawezi kuona kasoro zake mwenyewe, bali kwa kutazamwa na watu wanaomzunguka. Ndiyo maana pale mwanadamu anapotaka kuondoa kasoro iliyo katika uso wake, hulazimika kutumia kioo, ili kuondoa kasoro hiyo.

Kwa mantiki hiyo, CAG amesimama kama kioo kuonesha yale ambayo yeye binafsi ameyaona kama kasoro katika chombo hicho muhimu cha kutunga sheria, na kinachowawakilisha wananchi.

Mtu ama taasisi, inapoambiwa kuwa ni dhaifu, haina maana kweli ni dhaifu, ila kwa mtazamo wa huyo aliyesema. Hivyo jukumu la yule anayeambiwa hivyo, ni kutimiza yale anayopaswa kutimiza kwa vitendo na si kumshurutisha ama kumtishia aliyesema hayo.

Binafsi naamini CAG hajatenda kosa kwa sababu ametumia vema haki yake ya kikatiba ya uhuru wa kujieleza kama ilivyotajwa katika ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Kwa waumini wa dini ya Kikristo, katika Mithali 31:8-9 imeelezwa: “Fumbua kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu, uwatetee watu wote walioachwa peke yao, fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; uwapatie maskini na wahitaji haki yao.”

Vile vile uko mstari katika Biblia unaaosema: ‘Msiposema mawe yatasema.’ Kwa maana hii, Profesa Assad amekataa kungoja mawe yaseme, badala yake ametimiza wajibu wake.

Kwa kutumia malalamiko ya Lissu dhidi ya Ofisi ya Bunge kushindwa kumjulia hali kwa kipindi chote akiwa kwenye matibabu, unaweza kukubaliana na udhaifu unaotajwa na CAG.

Huenda Spika kwa nafasi yake, ameshindwa kufanya hivyo kutokana na sababu mbalimbali na kukabiliwa na majukumu mengi ya kiofisi, lakini haina maana kwamba lazima aende yeye, bali hata kwa kutuma mwakilishi kutoa pole kwa kiongozi huyo wa upinzani.

Najaribu kujiuliza hatua iliyochukuliwa na Spika Ndugai je, ni ubabe? Na kama ni ubabe, unamnufaisha nani? Kwa sababu Bunge ni chombo kinachoundwa na watu wengi na tangu kutoka kwa kauli ya CAG hatujasikia Wabunge wakijitokeza kulalamika kuhusu hilo.

NA LEONARD MANG’OHA

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.