Wabunge wetu hawana tena uwezo wa kujinasua

Rai - - MAKALA -

Kuna Mwandishi mmoja anaitwa George Orwell aliwahi kuandika kitabu kinachoitwa “Animal farm”, katika kitabu chake ndipo panapopatikana nadharia (Falsafa) ya ‘Animalism’.

George Orwell katika kitabu chake hicho anaonyesha jinsi wanyama tofauti tofauti walivyokutana na kukubaliana kuondokana na mateso ya binadamu aliyekuwa anawafuga “Mr Jones”

Wanyama hawa kupitia kwa kiongozi wao aliyefariki muda mfupi baada ya mkutano huo wa wanyama (Old major) walikubaliana kwa pamoja kuwa ni kweli kwamba binadamu ndiye adui yao mkubwa ambaye huwatumikisha wanyama kwa kiwango kikubwa na wanapofikia kuzeeka binadamu huwatumia wanyama hao kama kitoweo.

Old Major katika mkutano huo alionyesha namna binadamu anavyouza mayai ya kuku, maziwa, anavyowachinja Nguruwe nk.

Baada ya Old Major (Kiongozi wa wanyama) kufariki mpango wa mapinduzi ya Mr. Jones kama adui mkubwa unaongozwa na wanyama wawili ambao ni nguruwe wadogo walioitwa Snowball na Nepoleon. Mikakati ya kumpindua Mr. Jones unasukwa vizuri na Snowball na Neopolion na hatimaye wanafanikiwa kumwondoa Mr. Jones kwenye shamba na wao wanakuwa huru.

Baada tu ya mapinduzi yale Snowball na Neopolion kwa pamoja wanaitisha mkutano wa wanyama wote na kuwekeana sheria saba ambazo zitafuatwa na wanyama wote na sheria hizo ndizo zitakazowatofautisha hao na binadamu pamoja na dhuluma zake ..... katika sheria hizi ndipo palipozaliwa nadharia ya “Animalism”. Sheria zenyewe zilikuwa ni :1. Kiumbe chochote kinachotembea na miguu miwili ni adui yao.

2.Mwenye miguu minne au ana mabawa ni rafiki yao.

3. Sheria ya tatu inasema hakuna mnyama atakayeruhusiwa kuvaa nguo.

4. Sheria ya nne hakuna mnyama atakayeruhusiwa kulala kitandani.

5. Sheria ya tano hakuna mnyama atakayeruhusiwa kunywa pombe.

6. Sheria ya sita hakuna ruhusa ya mnyama kumuua mnyama mwingine na

7. Sheria ya saba wanyama wote ni sawa.

Kwenye mwendelezo wa kitabu hiki Snowball na Neopolion wanakuja kutengana kupigana na hatimaye Neopolion anashinda vita ile.

Neopolion akaanza kuishi maisha kama aliyokuwa akiishi binadamu na sheria zote saba walizojiwekea akashindwa kuzifuata akaanza kulala kitandani, akaanza kunywa pombe akaanza kushirikiana na wanyama wenye miguu miwili na hata akafikia mahali akashirikiana na binadamu Mr. Fredrick aliyekuwa anamiliki shamba lingine la wanyama na alikuwa akiitesa wanyama sana. Kufikia hapo Neopolioni akashindwa kujitofautisha na binadamu.

NATAKA KUWAAMBIA NINI

Mwaka 2015 viongozi wetu walikuja wakatuahidi mambo mengi sana. Palipokuwa na mbunge CCM tuliambiwa bila kuwachagua wapinzani hakuna maendeleo mtakayoyapata.

Palipokuwa na mbunge wa upinzani tuliambiwa kama tusipoichagua CCM tumekwenda na maji na hatutapata maendeleo.

Wananchi tukaamini na tukafanya kama walivyotuambia.

Wabunge wetu walipofika bungeni cha kwanza walikopa wakanunua Ma V8 ili afanane na hadhi ya Mheshimiwa. Waliokuwa hawajajenga wakakopa wakajenga, wengine wakajenga hotel.

Leo ni mwaka 2019 shida ya maji aliyoombea kura mbunge wako ipo pale pale, tatizo la ajira lipo pale pale, matatizo ya wamachinga yapo pale pale, mitaa yetu ina umaskini ule ule nk.

Wamebakiza mwaka mmoja watarudi kuja kuomba kura. Tunawaomba wabunge wetu fedha badala ya maarifa na nyenzo. Na hata ukiwaomba maarifa hawana.

Kwa sasa wanakimbizana na madeni waliyokopa, hawana fedha hivyo hata majimboni hawaonekani. Wanajua wakija mtawaomba fedha na hawana fedha.

Ninaposema wabunge wetu hawana fedha ninamaanisha. Siku Lisu anashambuliwa na wasiojulikana walishindwa kujichanga ili wakodishe ndege badala yake waliikopa.

Kulipa ilikuwa ni mbinde haswa. Tufanye nini mwaka 2020? Hili ndio swali la msingi ambalo tunatakiwa tujiulize. Kofia, kanga na pombe zisitumike kuwapata viongozi.

Waliotuahidi mema wameenda kuishi maisha yale yale ambayo tulikubaliana kuyaacha na kukimbizana na shida za wananchi. Tulichagua kina Snowball na Neopolion.

Watu wanafikiri tatizo ni kubadili aina ya uongozi kwa kutumia vyama. Hapana tatizo lipo kwenye fikra .... tubadili watu kifikra kuanzia viongozi wetu.

Maisha ya viongozi wetu ambao wanajinasibu kuwa ni viongozi wa wanyonge yanalingana na maisha yao?

Kwa kifupi maisha yaliyobadilika ni ya viongozi wetu na sio ya wananchi.

Rais wa Uruguay Jose Mujica almaarufu ‘Pepe”. Mujica anatajwa kama Rais maskini kuliko wote duniani na ambaye ameisaidia sana Uruguay kuwa na uchumi walionao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.