Ndoto ya Ufaransa kuitawala dunia ilivyoshindwa

Rai - - MAKALA - NA MBWANA ALLYAMTU

WIKI iliyopita tulidadavua historia ya Taifa la Ufaransa lakini pia tukagusia kidogo mapinduzi ya nchi hiyo yaliyomuisha matukio muhimu ya siasa kwa kipindi cha miaka 10, tangu 1789 hadi 1799, yaliyobadilisha uso wa Ufaransa na utamaduni wa Ulaya kwa jumla, kiasi cha kuhesabiwa kati ya matukio makuu ya historia yote.

CHIMBUKO LA MAPINDUZI

Mwaka 1789 Mfalme Louis XVI alilazimishwa kuitisha Bunge la taifa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 170. Sababu yake ilikuwa kwa kiasi kikubwa cha madeni ya serikali yaliyosababishwa na matumizi makubwa ya mfalme pamoja na gharama za vita vya uhuru vya Marekani vilivyosaidiwa na Ufaransa dhidi ya Uingereza.

Tangu Louis XIV (1643–1715) wafalme walitawala Ufaransa bila Bunge, lakini kisheria mfalme hakuwa na madaraka ya kuongeza kodi bila idhini ya Bunge, na Louis XVII hakuwa tena na nguvu ya kutosha kupuuzia utaratibu huo. Bunge la Ufaransa lilikuwa na wawakilishi wa matabaka matatu: koo za makabaila, wawakilishi wa Kanisa Katoliki na wawakilishi wa tabaka la tatu yaani raia waliolipa kiasi fulani cha kodi. Maskini na wanawake hawakuwa na wawakilishi.

Wawakilishi wengi wa tabaka la tatu walidai kupewa nafasi kubwa zaidi kuliko matabaka mengine. Baada ya matatizo ya kutoelewana, wawakilishi wa tabaka la tatu walijitangaza kuwa na Bunge la taifa hata bila ya wawakilishi wa waungwana waliotetea haki zao za kale. Kutokana na vurugu za kisiasa na mfumuko wa bei za chakula, wananchi wa Paris waliasi, wakashambulia gereza la Bastille na kulibomoa. Mfalme aliyedhoofika hakutaka kukandamiza uasi huo na bunge la taifa liliendelea kubadilisha sheria kwa kufuta haki za pekee za waungwana. Mashambani wakulima walianza kuasi na kukataa ulipaji kodi katika mikoa mbalimbali.

Mfalme alipoona ya kwamba madaraka yake yanapungua zaidi na zaidi alijaribu kuondoka kwa kukimbia nchi lakini alikamatwa na kurudishwa kama mfungwa mwaka 1791. Mwelekeo mkali kati ya wabunge ulipata ushindi na mwaka 1792 Ufaransa ulitangazwa kuwa jamhuri. Mfalme alishtakiwa kuwa msaliti wa taifa akapewa hukumu ya kifo na kukatwa kichwa pamoja na mke wake tarehe 21 Januari 1793.

Wafalme wa nchi jirani waliamua kushambulia Ufaransa na kulipiza kisasi kwa kifo cha mfalme. Katika joto la vita watu wa vikundi vikali vilipata kipaumbele wakaanzisha kipindi cha udikteta chini ya kamati ya bunge lililoongozwa na Robespierre. Watu wengi (16,000-40,000) walishtakiwa kuwa wasaliti wakauawa hadi upinzani ndani ya Bunge ulipofaulu kuwakataa viongozi wakali na kuwaua. Kipindi kilichofuata kilikuwa na serikali zilizochaguliwa na bunge. Zililenga kurudisha utaratibu nchini na kutetea taifa katika vita vilivyoendelea hasa dhidi ya Uingereza na Austria. Katika vita hivyo jenerali Napoleon Bonaparte alikuwa kiongozi aliyeweza kushinda Austria akawa shujaa wa taifa.

Mwaka 1799 kwa tishio la kijeshi alilazimisha bunge kubadilisha katiba akaingia serikalini na kuwa mtawala pekee kwa kibali cha bunge lisilokuwa na njia nyingine isipokuwa kumkubali. Tangu hapo Napoleon alitawala kwa cheo cha “konsuli wa kwanza”. Baada ya mabadiliko mengine ya katiba alichukua cheo cha Kaisari wa Ufaransa mwaka 1804.

SABABU ZA MAPINDUZI

Kabla ya mapinduzi Ufaransa ulitawaliwa na wafalme. Mfalme Louis XIV aliwahi kuunganisha mamlaka yote ya dola mikononi mwake akifaulu kukandamiza upinzani wote wa waungwana na malodi. Utawala wake huo wenye madaraka yote uliendelea chini ya waaandamizi wake. Kila azimio lilitegemea mapenzi ya mfalme bila njia yoyote ya upinzani.

Ufaransa haikuwa na bunge la kudumu, palikuwa na mabunge ya kimkoa ambako wawakilishi wa waungwana na makasisi wakuu wa Kanisa Katoliki (iliyokuwa dini pekee halali kisheria) walikutana, wakati mwingine pamoja na wawakilishi kadhaa wa tabaka la tatu lililojumlisha watu wengine wote wenye mali. Bunge la taifa lililokuwa na madaraka ya kuamua juu ya sheria za kodi hasa liliwahi kualikwa mara kadhaa na wafalme lakini tangu Louis XIV ayachukuwe madalaka halikukutana tena.

Mwaka 1789 utawala huo ulishikwa na machafuko. Wafalme walitumia pesa vibaya na nchi ilikuwa na madeni makubwa. Madeni hayo yalisababishwa na vita, matumizi makubwa kwa

maafisa wa serikali na gharama za familia ya kifalme, kwa mfano ujenzi wa majumba ya kifalme na sherehe za mfalme. Katika jamii ya Ufaransa vikundi viwili vilikuwa na haki nyingi, yaani familia za waungwana na makasisi wa Kanisa Katoliki. Hao hawakulipa kodi ingawa walikuwa na mashamba makubwa yaliyolimwa na wakulima waliopaswa kuwalipia mchango wa mavuno. Kodi zote za nchi zililipwa na wakulima au wafanyabiashara wa mjini.

Mwaka 1788 ulikuwa na mavuno mabaya na wakulima wengi hawakujua jinsi ya kulipa kodi zao. Ghala za waungwana na za makanisa zilijaa kutokana na mavuno ya miaka ya nyuma, lakini kwa jumla bei ya nafaka ilipanda pamoja na bei ya mkate uliokuwa chakula kikuu cha Wafaransa. Viongozi wa serikali chini ya mfalme waliona haja ya mabadiliko lakini matabaka tawala ya waungwana na viongozi wa Kanisa hawakuwa tayari kukubali mabadiliko yoyote.

Kuibuka kwa Bunge la matabaka matatu Mnamo Februari 1789 serikali ilialika mkutano wa wawakilishi wa waungwana na makasisi wakuu ikatafuta kibali chao kwa sheria mpya, eti hata waungwana walipe kodi. Mkutano ulikataa ukidai hauna madaraka ya kubadilisha sheria za kale, lakini ilikuwa wazi kwamba hiyo ilikuwa lugha tu ya kuepukana na kodi. Hivyo serikali ilimshauri mfalme kualika bunge la kitaifa la matabaka yote matatu kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1614. Zamani Bunge hilo lilikuwa na idadi sawa ya wawakilishi kwa kila tabaka yaani 300-300-300 kwa waungwana, makasisi na tabaka la tatu. Tena kila tabaka lilikuwa na kura moja tu, kwa hiyo kila azimio lilihitaji kura zote tatu au kura mbili dhidi ya moja.

Kabla ya mkutano huo wawakilishi wa tabaka la tatu walidai kuongezeka kwa kura zao wakieleza ya kwamba hadi sasa tabaka lao lililipa kodi zote na kuwakilisha zaidi ya asilimia 90 za wananchi. Mfalme alihangaika akakubali tabaka la tatu liwe na wawakilishi 600, isipokuwa alikaa kimya juu ya suala la kura.

Kujitenga kwa tabaka la tatu kuwa bunge la taifa Bunge lilikaa wiki kadhaa bila ya makubaliano juu ya namna ya kupiga kura. Baada ya mwezi mmoja sehemu ya mapadri walijiunga na wawakilishi wa tabaka la tatu kutetea azimio lililopelekwa na kasisi Abbe Siyes tabaka la tatu likajitangaza kuwa linawakilisha asilimia 96 za wananchi likajiita “Bunge la taifa”. Wawakilishi wa waungwana na makasisi wengine walialikwa kujiunga nao kwenye msingi wa kura moja kwa kila mbunge. Makasisi wengi na waungwana wachache walifuata wito huo, lakini kundi kubwa la waungwana walikataa wakadai mfalme aingilie kati. Mfalme Louis XVI alitangaza mkutano mpya chini ya utaratibu wa kale akafunga ukumbi wa mkutano hadi siku hiyo.

Wawakilishi wa bunge la taifa waliamua kukutana mahali penginepo wakaahidiana kutoachana hadi katiba ya taifa itakapokuwatayari.Mfalmealiamuru waondoke lakini mwenyekiti wao alikataa. Mfalme aliandaa vikosi vya jeshi lakini sehemu za waungwana walimwomba asitumie silaha. Mwishowe mfalme alikata tamaa akaamuru matabaka yote yakae pamoja katika bunge la taifa.

Baada ya mapinduzi, Ufaransa uliingia katika vita na falme nyingine za Ulaya zilizoona mapinduzi ni hatari kwao. Wapinzani walikuwa hasa Uingereza, Austria na pia Prussia. Kwa jumla jeshi la kimapinduzi lilifaulu kutetea eneo la Ufaransa na kuingia katika sehemu za Ujerumani, Uholanzi na Italia. Katika vita hivyo afisa kijana, kwa jina Napoleon Bonaparte, alipanda vyeo haraka hadi kuingia katika siasa mwaka 1799 alichukua mamlaka yote kwa kutumia cheo cha “Konsuli wa Kwanza” na tangu 1804 alijiita “Kaisari wa Wafaransa”.

Katika vita vya mfululizo aliteka sehemu kubwa ya nchi za Ulaya au kuzilazimisha kumfuata. Baada ya kushinda Prussia na Austria na kutawala Italia pamoja na Hispania alikuwa mkuu wa Ulaya. Lakini vita alivyoanzishwa mwaka 1812 dhidi ya Urusi vilikuwa msingi wa kushindwa kwake. Mwaka 1814 alipaswa kusalimu amri, akapelekwa kwenye kisiwa cha Elba (Italia), aliporudi barani na kujaribu kuwa mkuu wa Ufaransa tena, jeshi lake lilishindwa katika mapigano ya Waterloo mwaka 1815 na Napoleon akawa mfungwa kwenye kisiwa cha St. Helena hadi kifo chake. Baadaye ufalme ulirudishwa kwa msaada wa nchi zilizoshauriana pamoja kwenye mkutano wa Vienna 1815.

Baada ya mapinduzi ya mwaka 1789 Ufaransa yote iligawanywa katika wilaya (far departement) zilizoongozwa na mkuu (prefect) aliyekuwa mwakilishi wa serikali kuu. Tangu mwaka 1964, wilaya ziliwekwa chini ya ngazi mpya ya mikoa (region). Wakati wa marekebisho ya katiba mpya mwanzoni mwa miaka ya 1982 Ufaransa ilianza kutumia mfumo wa ugatuzi na kuipa mikoa, wilaya na kata zake kiwango cha madaraka ya kujitawala.

Katika siasa hasa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia ambako nchi ilivamiwa na Ujerumani ilipata katiba mpya na kujiunga na NATO (1949) na Umoja wa Ulaya (tangu 1951). Ufaransa Ilihesabiwa kati ya nchi washindi wa vita na kupata kiti kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Wakati huohuo utawala wake juu ya ukoloni ulianza kuporomoka, Baada ya kushindwa katika Vita Kuu ya Kwanza ya Indochina mwaka 1954, Ufaransa ulipaswa kukubali uhuru wa Vietnam Kaskazini, Vietnam Kusini, Laos na Kambodia. Laikin Koloni zake nyingi katika Afrika zilipata uhuru bila vita mnamo 1960. Algeria iliyowahi kutangazwa kuwa sehemu ya Ufaransa yenyewe ilipata uhuru wake baada ya vita ya ukombozi ya miaka 1954 - 1962.

Katika kipindi hiki cha mvurugo Jenerali Charles de Gaulle, alichaguliwa kuwa rais chini ya katiba mpya iliyounda mfumo wa rais kama kiongozi wa serikali mwenye mamlaka makubwa. Vyama mbalimbali vilivyoendelea kutetea itikadi ya de Gaulle hata baada ya kifo chake viliendelea kufuata mkondo huu muhimu katika siasa ya Ufaransa na maraisi walichaguliwa ama kutoka mkondo huu (Jaques Chirac, Nicolas Sarkozy) au kutoka Chama cha Kisoshalisti (Francois Mitterand, Francois Hollande).

Tangu miaka ya 1980, chama kipya cha Front National kilianza kupata kura kikipinga uhusiano wa karibu na Umoja wa Ulaya na wahamiaji Waislamu kutoka nchi za Afrika ya Kaskazini. Katika uchaguzi wa raisi wa mwaka 2017 ilitokea mara ya kwanza kwamba wagombea wa vyama vikubwa walishindwa kupata kura nyingi katika awamu ya mwisho wa uchaguzi ambao ilikuwa kati ya mgombea wa kujitegemea Emmanuel Macron na Marie Le Pen wa Front National.

Kabla ya mkutano huo wawakilishi wa tabaka la tatu walidai kuongezeka kwa kura zao wakieleza ya kwamba hadi sasa tabaka lao lililipa kodi zote na kuwakilisha zaidi ya asilimia 90 za wananchi. Mfalme alihangaika akakubali tabaka la tatu liwe na wawakilishi 600, isipokuwa alikaa kimya juu ya suala la kura.

Napoleon Bonaparte

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.