Wanawake wanaoamka mapema rahisi kupata ujauzito

Rai - - AFRIKA - NA HASSAN DAUDI

SI porojo bali ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya elimu yenye jina kubwa huko Marekani, Chuo Kikuu cha Warwick, na uliwahusisha wanawake zaidi ya 100.

Katika idadi hiyo, watafiti walitaka kujua ni wangapi wenye tatizo la kupokea ujauzito na inachangiwa kwa kiasi gani na ratiba yao ya kulala na kuamka.

Ndipo ilipobainika ni wale wasio na utamaduni wa kulala mapema huenda wanajiweka kwenye hatari ya kutoshika mimba katika siku za usoni.

Majibu ya wasomi hao wa Chuo Kikuu cha Warwick yalionesha kuwa ni theluthi tu wanawake waliokuwa wakichelewa kuamka ndiyo walioweza kushika mimba.

Aidha, mwaka jana, utafiti mwingine ulisema wanawake wanaolala ‘usiku mnene’ huwa kwenye hatari ya kutoolewa.

Ni katika utafiti wa safari hii ndipo pia ilipofichuka kuwa hata kama mwanamke anayechelewa kulala atapata ujauzito, mara nyingi huzaa mtoto kabla ya muda ‘njiti’ au mwenye umbo dogo.

Wakiielezea hali hiyo, walisema wanawake wenye kawaida ya kudamka huwa vizuri kiafya, hivyo viungo vyao vya uzazi huwa kwenye wakati mzuri wa kufanya kazi.

Kuliongezea hilo, wataalamu wa masuala ya afya wa Chuo Kikuu cha Colorado Boulder walishawahi kusema wanawake wanaowahi kuamka hujiweka katika mazingira mazuri ya kuepuka msongo wa mawazo kwa kuwa ni moja kati ya kazi za mwanga wa jua wa asubuhi.

Akifafanua, Profesa aliyeongoza timu ya watafiti hao, Geraldine Hartshorne, alisema kuamka mapema, akitolea mfano saa 12:00 asubuhi, huepusha kuongezeka uzito, kisukari na ugonjwa wa moyo, mambo ambayo kwa namna moja au nyingine yanaweza kumzuia mwanamke kupata mimba.

Katika utafiti wao, wanawake waliosema huwa wanachelewa kuamka walisema hulala saa 8 usiku na kuamka saa 4 asubuhi, tofauti na wenzao ambao walisema hukiacha kitanda saa 11.30 asubuhi.

Hii si mara ya kwanza kwa wanawake wanaoamka mapema kutajwa kuwa kwenye kiwango kizuri cha kupata ujazuito kwani madai hayo yaliwahi kuibuliwa na utafiti kutoka Finland.

Hiyo ilikuwa ni kupitia utafiti wao uliowahusisha wanawake 2,600, ambapo asilimia zaidi ya 50 ya wale waliosema huchelewa kuviacha vitanda vyao asubuhi, walionekana kusumbuliwa na tatizo la kushindwa kushika mimba.

Kwa upande wake, Profesa Hartshorne alisema bado watafiti wana kazi ya kufanya, kuchunguza na kuelezea kwa kina uhusiano uliopo kati ya kulala, homoni za mwanamke na mchakato wa utungaji mimba.

Aidha, katika utafiti wao walibaini kuwa mimba za wanawake wenye umri au maumbo makubwa huwa na tatizo kwa kuwa hatua za ukuaji za ‘kiumbe’ huchukua muda kidogo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.